TANGAZO


Saturday, November 30, 2013

Rais wa Zanzibar, Dk. Shein akutana na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Daniel Ole Njooley, alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kumuaga Rais leo, baada ya kuteuliwa  kushika nafasi hiyo. (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dk. Ali Mohamed Shein, akiagana  na  Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Daniel Ole Njooley,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar  leo, baada ya kuteuliwa  kushika nafasi hiyo.
 
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo, amekutana na Balozi Mpya wa Tanzania nchini Nigeria Balozi Daniel Ole Njoolay.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ofisini kwake Ikulu Dk. Shein alimueleza Balozi Njoolay kuwa watanzania wana matumaini makubwa kuona uhusiano kati ya Tanzania na Nigeria unaimarika kwa kupanua maeneo ya ushirikiano hasa kwa kuzingatia Sera ya Nje ya Tanzania ya Diplomasia ya Kiuchumi.

Alisema kuwa uhusiano wa Tanzania na Nigeria umekuwa wa miaka mingi na wananchi wa nchi mbili hizo wamekuwa karibu kwa kushirikiana katika nyanja mbalimbali hivyo wakati akiiwakilisha Tanzania nchini humo jukumu kubwa kuangalia namna bora ya kuongeza ushirikiano huo na kuwakweka watu wa nchi hizo karibu zaidi.

Dk. Shein alimueleza Balozi Njoolay kuwa kuiwakilisha Tanzania nchini Nigeria ambako kunajumuisha kuiwakilisha nchi yetu katika nchi nyingi za ukanda wa Afrika Magharibi ikiwemo Ghana kunampa fursa kuitangaza Tanzania katika eneo hilo kubwa na muhimu la Afrika.

Alimtaka Balozi Njoolay kutumia fursa hiyo kukaribisha wawekezaji kutoka Nigeria kwa kuwa katika nchi hiyo wapo wananchi wenye uwezo mkubwa wa kuwekeza katika sekta mbalimbali na baadhi yao wameanza kufanya hivyo huko Tanzania Bara.
Alifafanua kuwa Zanzibar hivi sasa inafanya jitihada za kuvutia wawekezaji katika uvuvi wa bahari kuu na kwa kuwa wako wawekezaji wakubwa wa viwanda vya samaki nchini Nigeria alimtaka Balozi kutumia fursa hiyo kuwahamasisha kuwekeza humu nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyataja maeneo mengine ya ushirikiano na Nigeria kuwa ni ushirikiano katika masuala ya utafiti wa mazao ya kilimo kikiwemo kilimo cha muhogo ambacho Nigeria imepiga hatua kubwa katika utafiti na usarifu wa matumizi ya muhogo.
Eneo jingine alilitaja kuwa ni elimu ambapo mbali ya ushirikiano uliopo wa kusaidia walimu wa sekondari kwa masomo ya sayansi na Hisabati Zanzibar lakini alihimiza ushirikiano katika taasisi za elimu ya juu hasa katika masuala ya utafiti ili kukiongezea uwezo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar- SUZA.
Alieleza kuwa angependa ushirikiano kama huo katika sekta ya elimu ungefufuliwa tena na nchi ya Ghana ambayo huko nyuma ilikuwa ikishirikiana kwa karibu na Zanzibar.

Dk. Shein aliongeza kuwa ushirikiano katika ufundishaji wa lugha ya Kiswahili ni suala jingine ambalo angependa Balozi Njoolay alisimamie kwa kuwa wananchi wengi wa Nigeria wanapenda kujifunza lugha hiyo na uzoefu unaonyesha hivyo kwa miaka mingi sasa.
Kwa upande wake Balozi Njoolay alimuhakikishia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa amejiandaa vyema katika kutekeleza kwa vitendo Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi ambayo inahimiza diplomasia ya Uchumi. 
Alieleza kuwa ametumia ujio wake hapa Zanzibar kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali na pia ametembelea Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar-ZIPA ambapo mbali ya kufanya mazungumzo na uongozi wa mamlaka hiyo lakini pia amekabidhiwa vipeperushi vya kuitangaza Zanzibar kwa wawekezaji.
Baada ya mazungu mzo hayo na Mheshimiwa Rais, Balozi Daniel Ole Njoolay kwa ushauri wa Rais alitembelea kituo cha utafiti wa kilimo cha Kizimbani ili kupata taarifa zaidi kuhusu kituo hicho na namna kinavyoweza kushirikiana na taasisi za utafiti za Nigeria.

No comments:

Post a Comment