TANGAZO


Saturday, November 30, 2013

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif awa mgeni rasmi mahafali ya Shule ya Daarul Arqam, amuhani Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula

Baadhi ya wahitimu wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Daarul Arqam, iliyoko Kigamboni, Dar es Salaam, wakiwa katika mahafali yao hayo leo. (Picha zote na Salmin Said, OMKR)
Baadhi ya wahitimu wa Shule ya Maandalizi ya Daarul Arqam iliyoko Kigamboni, Dar es Salaam, wakiwa katika mahafali yao hayo. 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Daarul Arqam iliyoko
Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika ya pamoja na uongozi wa Shule ya Sekondari ya Daarul Arqam pamoja na baadhi ya wahitimu wa shule hiyo, iliyoko Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akitia saini kitabu cha maombolezo, kufuatia kifo cha mtoto wa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bara), Peter Philip Mangula.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akimpa pole Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, alipofika nyumbani kwake Ostabey Dar es Salaam leo, kufuatia kifo cha mtoto wake, Peter Philip Mangula.
 
 
Na Hassan Hamad, OMKR
 
Dar es Salaam  
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema shule binafsi zina mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu nchini.

Mhe. Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika sherehe za mahafali ya kumi na moja ya shule ya Kiislamu ya Daarul Arqam, iliyoko Kigamboni Dar es Salaam.

Amesema mchango unaotolewa na skuli binafsi unapaswa kuungwa mkono, ili kuhakikisha kuwa sekta ya elimu inapata maendeleo makubwa mijini na vijijini.

Ameipongeza skuli hiyo kwa kuwa na malengo ya kutaka kuiendeleza hadi kufikia Chuo Kikuu, hatua ambayo itasaidia kunyanyua kiwango cha elimu nchini, sambamba na kuwaondoshea usumbufu wanafunzi wa maeneo hayo.

Amefahamisha kuwa katika kuimarisha ubora wa elimu, ni vyema mtaala wa elimu ukaangaliwa upya, ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu itayowasaidia baada ya kuhitimu masomo yao.

Amesema mtaala wa sasa bado haujatoa kipaumbele kwa mafunzo ya amali, na kwamba wakati umefika kufikiria kwa umakini jambo hilo, ili wanafunzi wanaohitimu waweze kujiajiri wenyeye, na kuacha kutegemea ajira kutoka serikalini ambayo haitoweza kuajiri wahitimu wote.

Amewashauri kutilia mkazo masomo ya sayansi na mawasiliano ya habari (ICT), ili kwenda sambamba na mahitaji ya wakati huu wa sayansi na teknolojia, na kuweza kukabiliana na soko la ajira.

Katika hatua nyengine Mhe. Maalim Seif amewakumbusha wahitimu hao kuendeleza maadili mema waliyoyapata shuleni hapo, na kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya.

Pia ametumia fursa hiyo kuuasa uongozi wa skuli hiyo kutilia mkazo elimu ya uhifadhi wa mazingira, ili kudhibiti uharibifu wa mazingira ambao umekuwa miongoni mwa changamoto kubwa za dunia.

Aidha amewataka waislamu wenye uwezo kuwekeza katika elimu, ili kuwaendeleza vijana  kitaaluma na kuwajengea misingi imara ya maisha yao ya baadae.

Amewashauri wazazi na walezi kuwaondoshea vikwazo watoto wa kike vikiwemo biashara na kuwaozesha waume wakiwa wadogo, ili kuwaandaa vyema kukabiliana na hali ya maisha.

Mapema Maalim Seif aliweka jiwe la msingi katika jengo la Maabara ya shule hiyo na kuahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji ili kuendeleza ujenzi huo.

Kwa upande wake Meneja wa Shule hiyo,  Bw. Abdul Aziz Shawwal Msami, amempongeza Makamu wa Kwanza wa Rais kwa juhudi anazozichukua katika kusogeza mbele maendeleo ya elimu nchini.

Ameiomba Serikali kuangalia namna ya kupunguza kodi katika uendeshaji wa taasisi binafsi za elimu, ili kuziwesha kutimiza malengo waliyojiwekea.

Shule hiyo, yenye kitengo cha Maandalizi, Msingi na Sekondari, pamoja na mambo mengine imekuwa ikifundisha lugha za Kigeni, Quran, maadili ya Kiislamu na michezo.

No comments:

Post a Comment