Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge, mjini Dodoma leo.
Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge, mjini Dodoma leo. Kulia ni Spika wa Bunge Anne Makinda.
| Rais Jakaya Kikwete, akibadilishana mawazo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, mara baada ya kulihutubia Bunge, mjini Dodoma leo jioni. |
Mheshimiwa
Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi;
Mheshimiwa
Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa
Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa
Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni;
Waheshimiwa
Wabunge;
Mabibi
na Mabwana;
Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu
ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa
uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa
Spika;
Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa
Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo waliodhani kuwa nakuja
kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio ya wiki chache
zilizopita. Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni Tokomeza”. Tena
wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge
waliotoa maoni yao kuelezea kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa
Operesheni hii muhimu. Na wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa
majeshi yetu ya Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa
nchini Kongo.
Mheshimiwa
Spika;
Hayo si makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni
kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika
Jumuiya hiyo. Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja na rai
niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo. Nimeona ni vyema nifanye
hivyo.
Mheshimiwa
Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika
utekelezaji wake. Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa
mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu Katiba
wanayoitaka. Pia walishatoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato
wa Mabaraza ya Katiba. Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili
ya Katiba ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla
ya hapo.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu
yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata. Jambo la
kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho
ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha
utekelezaji wake. Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa
Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike
na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika Kura
ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata Katiba Mpya.
Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya tafakuri na tunachukua hatua za
kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni kufanyika kwa
mafanikio.
Operesheni
Tokomeza
Mheshimiwa
Spika;
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa
sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa maliasili za misitu na
wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia
kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli hali inatisha. Miti inakwisha na ndovu
na faru wanaangamia.
Mheshimiwa
Spika;
Wakati, tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani
350,000. Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika miaka ya
1970 na 1980 ilipofika mwaka 1989 kulikuwa na ndovu
wapatao 55,000 tu. Ilipofikia hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni
Uhai iliyohusisha Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja Jenerali John Walden
(ambaye sasa ni marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na
hatua hiyo na uamuzi wa Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko kwenye
hatari ya kutoweka (CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu duniani,
idadi ya ndovu nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka
2009.
Tumewaomba
Fankfurt Zoological Society ambao ni wabia wetu katika uhifadhi wa wanyama pori
kwa miaka mingi wafanye sensa maalum ya ndovu katika Hifadhi ya Selous na kote
nchini ili tujue hali halisi ikoje. Kazi hiyo inaendelea hivi
sasa.
Mheshimiwa
Spika;
Baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua
ndovu na faru nchini na kwingineko katika Bara la Afrika ambako wanyama hao
wapo. Idadi kubwa ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na yanaoendelea kukamatwa
nchini na kwingineko duniani inathibitisha ukweli huo. Kwa mfano, kati ya mwaka
2010 na Septemba, 2013, hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya
pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya pembe
za ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978 vilikamatwa. Aidha,
katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu vilivyotokea
Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797 vilikamatwa nje ya nchi.
Mheshimiwa
Spika;
Kama nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na
faru lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao. Nchi za Gabon,
Kenya, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe, Zambia na
nyinginezo nazo zinakabiliwa na matatizo kama yetu. Tatizo limekuwa kubwa kiasi
cha kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kushtuka na kuamua kuingilia kati kwa namna
mbili. Kwanza kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa ndovu na faru katika nchi
zenye wanyama hao. Na, pili, kuchukua hatua thabiti kudhibiti biashara ya meno
ya ndovu duniani. Ni ukweli ulio wazi kuwa kama hakutakuwepo na wanunuzi wa
meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa
Spika;
Kutokana
na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa.
Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni Uhai ya mwaka 1989 yanatupa
imani kuwa na safari hii pia tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama hii sasa ni
sawa na kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini. Hakika
wanyama hao watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia itatuhukumu
vibaya.
Mheshimiwa
Spika;
Tumeyasikia maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi kuwa tutayafanyia kazi. Serikali
imeahirisha kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa kurekebisha kasoro hizo
na kujipanga upya. Watendaji wasiokuwa waadilifu na wale wasiokuwa waaminifu
wataondolewa. Halikadhalika, kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili
tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe kwa mafanikio
yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa
Spika;
Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo iliyokutwa
kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa wenye
mifugo na mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa taarifa zote hizo zitafanyiwa
kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo. Pamoja na hayo, napenda
kuwakumbusha ninyi watunga sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori
hairuhusu mifugo kuchungwa katika maeneo ya hifadhi.
Naomba
tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza wajiepushe na kufanya hivyo. Ni uvunjifu wa
Sheria za nchi. Naomba pia, wananchi waelimishwe ili wajue kuwa wakifanya hivyo
na kukutwa katika maeneo hayo na mifugo yao kuna adhabu iliyotamkwa kwenye
sheria. Hivyo tusiwalaumu wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu
wabaya. Wanatekeleza Sheria iliyotungwa na Bunge hili. Pale wanapotenda
visivyo tuseme, watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi
la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa
Spika;
Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie kikosi
kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja huo kuongeza
nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lengo
la msingi ni kuiwezesha nchi hiyo kupata amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa
muda mrefu kutokana na kuibuka kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa
Spika;
Tulikubali, kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa tulishakubali maombi
kama hayo yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu. Ni miezi saba
(tangu Aprili) sasa tangu wanajeshi wetu waende Kongo na wamekuwa wanatekeleza
majukumu yao vizuri tena kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu. Sifa hiyo kwa
wanajeshi wetu imekuwa inatolewa na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa,
viongozi wa juu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO) na viongozi wa juu
wa Serikali ya Kongo.
Mheshimiwa
Spika;
Majeshi ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili. Yapo
yanayopewa jukumu la kulinda amani tu. Wanajeshi wake huwa hawapewi majukumu ya
kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa kujihami tu. Kwa kawaida
majeshi yenye jukumu hili hupelekwa mahali ambapo kumekuwepo na makubaliano ya
kuacha mapigano. Wanapelekwa kusaidia kuona Mkataba unatekelezwa ipasavyo.
Aina
ya pili ni ile ya majeshi yanayopelekwa mahali ambapo hakuna amani hivyo
wanapewa jukumu la kuchukua hatua za kufanya amani ipatikane. Majeshi haya
hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya wanaosababisha amani
ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo. Maana yake ni kwamba wanayo ruhusa
kuingia katika mapigano dhidi ya watu au vikundi vinavyovuruga amani. Tofauti
na wenzao wa kundi la kwanza, wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye hatari
zaidi ya kupoteza maisha au kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao
wameuawa na kujeruhiwa.
Mheshimiwa
Spika;
Wanajeshi
wetu wamekwenda Kongo chini ya utaratibu huu wa pili ambao unahusu kuingia
kwenye mapigano dhidi ya waasi kama hapana budi kufanya hivyo. Wametekeleza
majukumu yao vyema na kwa ujasiri mkubwa na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya
tumepoteza vijana wetu watatu shupavu. Daima tutawakumbuka na tutawaenzi
ipasavyo mashujaa wetu hawa. Tuzidi kuwaombea kwa Mola awape mapumziko mema.
Ameen.
Wakati
huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Rais Joseph
Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio ya kihistoria
waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa M23. Tunamtakia yeye na wananchi wa
Kongo kila la heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya kujenga upya eneo hilo
na kujenga mahusiano mapya miongoni mwa watu wa Kongo. Pia nawapongeza sana
wanajeshi wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya
iliyowezesha mafanikio kupatikana. Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini,
Tanzania na Malawi wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa
JWTZ.
Jumuiya
ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa
Spika;
Kama nilivyosema awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu nilipoomba
kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wetu. Nimeyachomekea tu kwa sababu ya
umuhimu wake katika jamii kwa wakati tulio nao. Jambo lililonileta hapa leo ni
kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na nafasi ya
Tanzania katika Jumuiya hiyo. Nimeona nifanye hivyo kutokana na maswali mengi
ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia matukio ya hivi karibuni ya viongozi wa
nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda, Rwanda na Kenya
kukutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi. Viongozi wenzangu
hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe,
Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na tarehe 28 Oktoba, 2013
mjini Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa
Spika;
Naomba kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili wanachama au zaidi
hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo mbalimbali.
Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna hiyo na nchi zote wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini, nchi wanachama zinatakiwa kufanya hivyo
kwa yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba hayamo
katika Mkataba au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au
taasisi za Jumuiya kuyashughulikia. Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo
ambayo yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo
yote iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi
nyingine.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa mujibu wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano
hiyo, kuna mambo yapatayo manane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi
hizo kwa lengo la kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
(1) Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
(2) Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3) Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4) Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
(5)Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6) Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa);
(7)Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8)Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
(1) Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
(2) Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3) Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4) Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
(5)Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6) Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa);
(7)Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8)Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa
Spika;
Ni dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na
yale yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo
manane hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au
kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni uzalishaji na
usambazaji wa umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya pamoja
ya nguvu ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado jukumu la
kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe kuamua.
Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango
ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni
wanachama?
Jambo
la pili, ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda. Hili si suala
la Jumuiya bali la nchi ya Uganda kuamua yenyewe peke yake au kwa kushirikiana
na wadau wengine. Rais Yoweri Museveni alituarifu mpango huo na sote tuliupokea
kwa furaha kwamba sasa tutapata mafuta karibu na nyumbani. Alitualika
kushiriki katika ujenzi wake sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo
muhimu.
Mheshimiwa
Spika;
Jambo
la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini na
Uganda. Hili si jambo linalobanwa na masharti ya Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi
tatu kuamua kufanya ili kuwezesha mafuta yao kufika kwenye masoko. Hata hivyo,
nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi
Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike Tanzania kupitia upande wa Kaskazini
Magharibi mwa Tanzania. Inaelekea mpango huo sasa haupo maana hatujausikia
kutajwa katika ujenzi wa bomba hilo.
Mheshimiwa
Spika;
Jambo
la nne ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali –
Bujumbura. Hili nalo hatuna tatizo nalo. Si mradi wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, ni jambo lililo chini ya mamlaka ya nchi wanachama husika. Hata
hivyo, ni vyema kutambua ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa
anga na majini kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya
kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa na Jumuiya yetu. Jumuiya hutengeneza
mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna East African Railway Masterplan, tuna
East African Road Network, na tuna Lake Victoria Development Programme kwa ziwa
Victoria.
Kwa
ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli ya kutoka Mombasa hadi Kigali na Juba ingekuwa
na tawi linalounganisha reli hiyo na reli ya Tanzania kama ilivyo reli ya Moshi
– Voi – Taveta aliyotuachia mkoloni. Tulitegemea hivyo kwa minajili ya
kuunganisha soko la Afrika Mashariki ambapo naamini Tanzania ni mdau muhimu.
Lakini inaelekea kwa maoni ya wenzetu hivyo sivyo.
Mheshimiwa
Spika;
Lazima
nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini wenzetu
wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013
na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha
utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa
Spika;
Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa
utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno nayo. Mambo
hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na Visa ya
Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari
waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha
(Single Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu
wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa
Spika;
Katika Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28
Aprili, 2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha
Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory). Kwa mujibu wa
mapendekezo hayo kila nchi mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na
kukusanya mapato yake kama ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa zinazopitia nchi
moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa mapato utafanyika
katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia. Mapato hayo yatawasilishwa
kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka.
Mheshimiwa
Spika;
Kutokana
na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la Mawaziri kuunda Kikosi Kazi cha
kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi
kazi inatakiwa kutolewa katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika
Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba, 2013. Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue
peke yao kuanza kutekeleza? Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo?
Mheshimiwa
Spika;
Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki hadithi yake inafanana na hii
ya Himaya ya Forodha. Katika Mkutano wa 14 wa Wakuu wa Nchi wanachama
uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea taarifa ya hatua
iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho. Mkutano huo
uliagiza nchi wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia
Shirikisho la Kisiasa na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa
na Timu ya Wataalamu. Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri litawasilisha
mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi mwezi
Novemba, 2013. Iweje leo wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa
kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa kweli huwa najiuliza maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini
kinachoendelea kufanywa na viongozi wenzangu watatu na kwa nini! Nakosa majibu
ya uhakika. Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika Mashariki na je
wanataka kuunda yao? Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia
vitimbi tutoke! Au sijui wanachuki na mimi! Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa
Wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu
hapa). Tupo na tutaendelea kuwepo!
Mheshimiwa
Spika;
Tanzania haijafanya jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote
mwanachama. Na ukweli ni kwamba ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu
kwa Jumuiya. Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu kwa Jumuiya na kushiriki kwa
ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Sabahu ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu
peke yao kwa kweli haieleweki.
Mheshimiwa
Spika;
Tunasikia
eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema kuwa wao
wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga. Yaani wana Umoja wa
Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing). Hivi ni nani hayuko tayari (who is
not willing?) Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai
kuwa wao ndiyo wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao
hatuko tayari. Madai hayo hayana ukweli. Ni vyema waseme ukweli. Kama
walitualika tukakataa ndiyo wanaweza kusema hayo.
Mheshimiwa
Spika;
Kumekuwepo
na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba Tanzania haina moyo wala
dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano wa Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo
inasemekana eti nchi yetu imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki na kwamba Tanzania tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka.
Wanadai kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika Mashariki ingekuwa mbali kwa
maendeleo. Maneno hayo yamekuwa yanarudiwa au kujirudia mara nyingi kiasi cha
kuwafanya baadhi ya watu wa Afrika Mashariki na hata kwingineko duniani waamini
hivyo.
Mheshimiwa
Spika;
Napenda
kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo hayana ukweli wo wote.
Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha ukweli wake hazina mashiko.
Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na Watanzania walivyo. Tanzania ni muumini
wa dhati wa umoja na utengamano wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika.
Tumethibitisha hivyo kwa vitendo kwa kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee
uliodumu kwa muda mrefu kuliko yote Afrika.
Mheshimiwa
Spika;
Tanzania
ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maana ya kutekeleza
Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao na
taasisi za Jumuiya. Kama lipo jambo ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa
ni kwa sababu za msingi na siyo kwa sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana
Jumuiya na tumeipa kipaumbele cha juu. Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya
muda wetu, fedha zetu na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na
kuifikisha Jumuiya hapa ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza kutokuipenda na
kudhoofisha maendeleo na ustawi wake. Ni maneno ya kushangaza na wala hayaingii
akilini. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.
Mheshimiwa
Spika;
Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi,
ajira, uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea hisia zisizokuwa sahihi juu yetu.
Mimi siamini kama kuna mengine. Hata hivyo, napata taabu kuamini kwamba
kutofautiana kwa mawazo katika mambo hayo kutapelekea baadhi ya wenzetu
wasipende hata kushirikiana nasi kwa mambo ambayo hayana matatizo na tumekuwa
tunashirikiana vizuri.
Mheshimiwa
Spika;
Tanzania
imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge Jumuiya yetu hatua moja baada
ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hatuna tatizo la kuongeza kasi ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo
yote. Tusiende kasi ya kupindukia. Mkataba unaelekeza tunaanza na Umoja wa
Forodha, inafuatia Soko la Pamoja kisha Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho
la Kisiasa.
Mheshimiwa
Spika;
Ni
kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya
kukamilisha baadhi ya hatua. Na, tulifanya hivyo kwa nia njema ya kutaka
Shirikisho lijengwe juu ya msingi imara. Na, msingi huo si mwingine bali
utengamano wa kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa
Kifedha zilizojengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo na kunufaisha wanachama
wote sawia.
Mheshimiwa
Spika;
Lazima tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa cha nchi
kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kama mambo ya kiuchumi
yakipangika vizuri na kila nchi ikanufaika sawia, unajenga msingi imara kwa
Shirikisho la Kisiasa kustawi na kudumu. Kama ngazi hizi tatu za awali
hazitashughulikiwa vizuri na nchi wanachama zikahisi hazinufaiki ipasavyo,
Shirikisho litayumba au kuyumbishwa hivyo kudumu kwake kutakuwa kwa
mashaka.
Mheshimiwa
Spika;
Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa utengamano
zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja. Kwa msimamo na
mtazamo wetu, Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho. Na huo siyo msimamo wangu
au wa Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa Watanzania walio
wengi.
Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa
Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika kila nchi kukusanya maoni ya wananchi
kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa hapa nchini Kamati hiyo
iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake, Kamati ilieleza
kuwa asilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho
lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa
kwake.
Mheshimiwa
Spika;
Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu hisia za Watanzania, kuhusu kuwepo kwa
Shirikisho na kasi ya utekelezaji wake. Watanzania wengi sana wanaunga mkono
kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka jambo hilo lisifanywe
haraka haraka. Wanataka lifanywe kwa umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua
kama ilivyoainishwa katika Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa
Spika;
Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakwenda
sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana tumeafiki mapendekezo ya
Kamati ile ya mwaka 2004 iliyoongozwa na Mheshimiwa Amos Wako wakati ule
akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya. Kamati hiyo iliundwa kupendekeza namna ya
kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa utengamano wa Afrika
Mashariki.
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamka muda wa kutekeleza ngazi ya
Umoja wa Forodha lakini uko kimya kuhusu ngazi zilizofuata. Ili kuondoa kasoro
hiyo na kwa nia ya kuharakisha Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni
na mapendekezo juu ya namna ya kufanya hivyo. Kamati ilifanya kazi nzuri ya
kupata maoni na hisia za watu wa makundi mbalimbali katika nchi wanachama kuhusu
ujenzi wa Jumuiya na utengamano.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa upande wa Tanzania kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako ilitambua hisia
za Watanzania kuhusu ardhi na ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo yabaki
kwenye mamlaka ya nchi wanachama kuamua. Kuhusu mchakato wa utengamano Kamati
ilipendekeza kwanza kwamba mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka
ufike ukomo wake wa miaka mitano. Baada ya hapo muda wa kutekelezwa ngazi
zinazofuata unaweza kupunguzwa. Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya
kuunda Soko la Pamoja yaanze hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika
mwisho ili mara wakati huo ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze. Hivyo hivyo mara
baada ya ngazi hiyo kuanza matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha
yanaanza. Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho ya kuunda Shirikisho yanaanza.
Kamati pia imetoa mapendekezo ya namna ya kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho
kwamba wananchi wa nchi wanachama wataamua kwa kura. Tukifuata mapendekezo ya
Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama tufanyavyo sasa Tanzania haina
matatizo nayo.
Mheshimiwa
Spika;
Baada ya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi
wa Jumuiya yao inasikitisha kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano
kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa kazi na kuamuliwa. Tunapata taabu zaidi pale
watu wanapobagua wenzao na wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa Jumuiya
na Itifaki zake. Kwa kweli kama mwenendo huu hautabadilika sijui mambo
yatakuwaje mbele ya safari.
Mheshimiwa
Spika;
Nchi
yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo imara na
iliyo endelevu. Jumuiya ambayo inaendeshwa vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi
zote wanachama na watu wake wananufaika nayo, na hivyo wanaifurahia. Tanzania
haina tatizo na kuharakisha mchakato wa utengamano, lakini tunapata taabu kuruka
baadhi ya hatua kabla hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika
kila hatua tunayochukua. Bila ya kufanya hivyo, Jumuiya yetu itakuwa
imejengeka katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto
nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.
Mheshimiwa
Spika;
Napenda
kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia
matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake. Tutafanya
kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo
itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala
kichocheo chake. Ndiyo maana, hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha
kuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki inaendelea kustawi.
Tutaendelea
kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza
kubomoa. Tutakumbushana umuhimu wa kuheshimu matakwa na masharti ya Mkataba
ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za
Jumuiya. Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi
kustawi na kunufaisha nchi wanachama na watu wake kama yalivyo malengo na
madhumuni ya kuundwa kwake.
Mungu
Ibariki Afrika
Mungu
Ibariki Tanzania
Idumu
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa
Spika na
Waheshimiwa
Wabunge;
Asanteni sana kwa kunisikiliza

No comments:
Post a Comment