TANGAZO


Monday, November 25, 2013

Rais Dk Shein azungumza na Uongozi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili

Baadhi ya viongozi mbalimbali wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, wakiwa katika mkutano wa  utekelezaji wa Mpango wa kazi za wizara hiyo, chini ya Mwenyekiti wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,(hayupo pichani), ukumbi wa mikutano, Ikulu mjini Zanzibar leo. (Picha zote na Ramadhan Othman Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,a kizungumza na Uongozi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, katika utekelezaji wa Mpango wa kazi za Wizara hiyo, ukumbi wa Mikutano, Ikulu mjini Zanzibar leo.Kushoto ni Makamo wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad. 
Waziri wa Kilimo na Maliasili, Suleiman Othman Nyanga, akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wizara yake katika mkutano maalum na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ikiwa ni kawaida ya kila Wizara kufanya hivyo, ukumbi wa mikutano, Ikulu mjini Zanzibar leo.


Rais Dk. Shein aipongeza Wizara ya Kilimo na Maliasili

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Wizara ya Kilimo na Maliasili kwa kuweza kutekeleza kwa mafanikio makubwa Mpangokazi wa Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Pongezi hizo amezitoa wakati akizungumza katika kikao cha kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na Taarifa ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2013/2014 kilichofanyika Ikulu leo.
Dk. Shein alibainisha kuendelea kuungwa mkono na washirika wa maendeleo kwa programu mbalimbali zinazobuniwa na Wizara hiyo ni uthibitisho wa umakini wa wizara katika kubuni na kutekeleza majukumu yake ya kuimarisha kilimo nchini.

Hata hivyo Mheshimiwa Rais ameitaka wizara hiyo kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya programu zake mbalimbali ili ziweze kupata mafanikio zaidi.
Alitoa mfano mradi wa udhibiti wa Nzi wa matunda ambapo alieleza kuwa  pamoja na jitihada zinazofanyika aliitaka wizara kutoa elimu ya kutosha itakayowawezesha wananchi kuwatambua vyema aina hiyo ya Nzi na hatua nyingine za kukabiliana nao ukiachia mitego inayotolewa sasa.
“Chapisheni vijarida kwa lugha nyepesi kusaidia wananchi kuwafahamu Nzi hawa na kuwaelekeza umuhimu wa kuyafukia matunda yaliyoathirika badala ya kuyatupa tu kitendo ambacho hakisaidii vita dhidi ya Nzi hao” Dk. Shein alifafanua.

Sambamba na hatua hiyo ameitaka Wizara hiyo kuipitia upya Sheria ya udhibiti wa mimea na mazao kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya biashara na uwekezaji.
Kuhusu suala la lishe hasa unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto Rais aliitaka Wizara kuelekeza pia programu zake katika maeneo ya mijini badala ya kuweka mkazo zaidi maeneo ya vijijini kama ilivyo sasa.
“Mijini kuna watu wengi kwa mfano mkoa wa Mjini Maghribi una watu wengi zaidi ya nusu milioni na wanawake wengi wa mijini hawayonyeshi watoto wao wakati wote kwa sababu mbalimbali”Alieleza Dk. Shein na kutaka jitihada zifanywe   kutoa elimu kwa kinamama hao.
Awali akitoa maelezo katika kikao hicho Waziri wa Kilimo na Maliasili Suleiman Othman Nyanga alieleza kuwa katika kipindi kilichopita Wizara yake imeweza kuchukua hatua mbambali za kuimarisha kilimo kwa kuzingatia mipango mikuu ya maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Katika mwaka wa fedha 2012/2013 alisema wizara ilichangia asimilia 30 ya pato la Taifa ambapo ilikadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi walitegemea sekta za Kilimo na Maliasili kwa ajira na mapato.
Kwa upande wa mwaka wa fedha 2013/2014 Waziri Nyanga alisema  wizara yake imejiwekea malengo 11 ili kuimarisha kilimo na maliasili ikiwemo kuimarisha mifumo ya Kisera na Sheria kwa kuzipitia na kutayarisha Sera 2, Sheria 2 na tafiti mbili za kiuchumi na kijamii kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Malengo mengine ni kisimamia ukulima wa ekari 35,000 za mpunga,kuotesha na kusambaza kwa wakulima miche milioni moja ya mikarafuu, miche milioni moja na nusu ya misitu  na matunda, kuanzisha na kuendeleza tafiti 17 za mbegu mpya za uzalishaji wa mazao makuu ya chakua na biashara.
Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji ya Wizara Katibu Mkuu Affan Othman Maalim alieleza kuwa katika kipindi kilichopita Wizara iliweza kukamilisha Rasimu  ya Sheria ya Hakimiliki za Wagunduzi wa aina za mbegu za mimea pamoja na Rasimu ya Mpango wa Utekelezaji Sera ya Masoko.
Kikako hicho kilihudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

No comments:

Post a Comment