Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo la kuipongeza na kuiunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa Bungeni hivi karibuni pamoja na masuala ya kuimarisha bandari na ushirikiano wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Kushoto ni Mkurugenzi wa Blue Gurds Taifa, Khamis Hassan.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo la kuipongeza na kuiunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa Bungeni hivi karibuni pamoja na masuala ya kuimarisha bandari na ushirikiano wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Kushoto ni Mkurugenzi wa Blue Gurds Taifa, Khamis Hassan na kulia ni Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Abdul Kambaya.
Baadhi ya waandishi wa habari, wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, wakati alipokuwa akizungumza nao kwenye mkutano huo, jijini Dar es Salaam leo.
Profesa Ibrahim Lipumba akifafanua jambo kwa waandishi wa habari katika mkutano huo.
Profesa Ibrahim Lipumba akijibu moja ya maswali ya waandishi wa habari katika mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wakiwa katika mkutano huo, wakifurahia jambo.
Taarifa ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba katika mkutano huo.
Ndugu waandishi
wa habari,tarehe 7 Novemba 2013 Rais Kikwete alilihutubia Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Madhumuni makubwa ya hotuba hiyo ilikuwa kuelezea msimamo
wa Tanzania kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya Kenya, Uganda na Rwanda
kukutana mara tatu bila kuihusisha Tanzania. Katika mikutano ya viongozi wakuu
wa nchi hizo ambayo iliishirikisha Sudan ya Kusini kujadili na kufikia maazimio
kuhusu mambo ambayo kimsingi na kiitifaki yanapaswa kujadiliwa katika vikao vya
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
CUF – Chama Cha
Wananchi kinaunga mkono msimamo wa Rais Kikwete kuwa pamoja na vitimbi
vilivyofanywa na Kenya, Uganda na Rwanda dhidi ya Tanzania na Burundi, Tanzania
haitajitoa na wala haitakuwa chanzo cha kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. CUF inalaani vikali vitimbi vya kuitenga Tanzania vilivyofanywa na
Kenya, Uganda na Rwanda. Tunatoa wito kwa Watanzania wote kushikamana kwa
dhati, kujenga umoja wa kitaifa, kujenga na kuimarisha miundombinu ya nchi yetu
na kuongeza ushindani wetu wa kiuchumi ndani ya Jumiya ya Afrika Mashariki na
Ulimwengu kwa ujumla.
Tarehe 24-25
Juni 2013, siku chache kabla Rais Obama hajatua Dar es Salaam, Marais wa Kenya,
Rwanda na Uganda walikutana kuimarisha uhusiano wao wa kibiashara na
kurahisisha usafiri baina ya nchi hizo tatu. Kwa kawaida masuala haya ya
kuimarisha biashara na usafiri baina ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki huzungumzwa
kwa pamoja na nchi zote wanachama wa Jumuiya hii. Inaelekea Kenya, Rwanda na
Uganda wameamua kuwaacha kando Tanzania na Burundi. Mimi nilidhani ziara ya
Rais Obama Tanzania ilielekea kutowafurahisha baadhi ya jirani zetu ambao
wangependa Rais Obama nchi zao badala ya Tanzania. Kenya walisusia Mkutano wa
Rais Obama na Wafanyabiashara wa Africa (Business Leaders Forum) ambao
uliandaliwa na Corporate
Council on Africa.
Uhusiano kati
ya Rwanda na Tanzania umezorota baada ya Rais Kikwete kuwapa ushauri viongozi
wenzake katika kikao cha Umoja wa Afrika, Addis Ababa kuwa njia muhimu ya
kumaliza migogoro ya kisiasa na kiusalama na kuleta amani katika Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo ni kwa nchi jirani za Kongo, ikiwemo Rwanda na Uganda ni
kuzungumza na kufikia muafaka wa kisiasa na mahasimu na waasi wao waliokimbilia
Kongo. Ushauri wa Rais Kikwete umetafsiriwa visivyo nchini Rwanda na
kusababisha kuzorota kwa uhusiano kati ya nchi zetu mbili.
Wachambuzi wa
mambo ya uhusiano wa kimataifa wanaamini ushauri wa Rais Kikwete umechukuliwa
kama kisingiziyo. Tatizo kubwa ni Tanzania kukubali kupeleka wanajeshi wake
Kongo kama sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa la kuleta amani Mashariki ya
Kongo. Wanajeshi wetu ndani ya Brigedi Maalum ya Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
(MONUSCO) inayoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa JWTZ
imefanya kazi nzuri na kufanikisha kulisaidia Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo kulisambaratisha jeshi la waasi la M23 ambao viongozi wake wa juu
wamekimbilia Uganda.
Tarehe 28
Agosti, 2013 viongozi wa Kenya, Uganda na Rwanda walikutana mjini Mombasa,
Kenya ambapo walishiriki katika sherehe maalum ya Rais Kenyatta kuzindua gati
jipya la kuegesha meli ili ziweze kupakuliwa kwa haraka na kuongeza ufanisi.
Lengo la Mamlaka ya Bandari ya Kenya ni kuifanya Mombasa kuwa bandari
inayoongoza kwa kuhudumia siyo tu Kenya, bali Tanzania ya Kaskazini, Uganda,
Rwanda, Burundi, Kongo, Sudan ya Kusini, Ethiopia na Somalia.
Mkutano wa tatu
wa Marais wa Kenya, Uganda na Rwanda ulifanyika tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini
Kigali, Rwanda. Rais Kikwete ameeleza kuwa Mambo yapatayo manane ya
msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo.
(1) Kujenga
reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
(2) Ujenzi
wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3) Kujenga
Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4) Kuanzisha
Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kutekeleza vipengele vyote;
(5) Kuharakisha
Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya
Katiba ya Shirikisho.
(6) Kuharakisha
uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single
East African Community Tourist Visa);
(7) Kuandaa
utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi
zao; na
(8) Kuongeza
uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Katika mambo
haya manane, manne yanatawaliwa na itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mambo hayo manne ni Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote, Kuharakisha Shirikisho la
Afrika Mashariki, Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya
taifa kama hati ya kusafiria.
Katika haya
manne Rais alieleza kuwa mawili yalifanyiwa uamuzi wa pamoja na hana matatizo
nayo. “Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria
na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama
zilizokuwa tayari waanze.”
Katika masuala
ya kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory)
na Shirikisho la Afrika Mashariki Kenya, Uganda na Rwanda wamekiuka uamuzi wa
pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais alieleza
Katika Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28
Aprili, 2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha
Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory). Kwa mujibu
wa mapendekezo hayo kila nchi mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha
na kukusanya mapato yake kama ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa
zinazopitia nchi moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa
mapato utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia.
Mapato hayo yatawasilishwa kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa
zilivuka mpaka. Wakuu wa Nchi
waliagiza Baraza la Mawaziri kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa
utaratibu wa utekelezaji wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa
kutolewa katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda
tarehe 30 Novemba, 2013. Kabla hata ya kupokea taarifa ya kikoso kazi,
Kenya, Uganda na Rwanda wameamua kutekeleza Single Customs Territory nje ya
taratibu za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwezi Agosti
Chama cha Wasafirishaji wa Mafuta Tanzania (Tatoa) walitoa taarifa kwenye
Kamati ya Kudumu ya Bunge inayosimamia mambo ya Bajeti kuwa ifikapo Septemba
mwaka huu Rwanda na Uganda watasitisha kutumia bandari ya Dar es Salaam kupitisha
mizigo yao. Serikali ilikanusha taarifa lakini inaonekana kuwa Rwanda na Uganda
wameamua kuwa watasita kutumia bandari ya Dar es Salaam na kwa hiyo wanaweza
kuanzisha taratibu za Single Customs Territory na Kenya bila kuishirikisha
Tanzania.
Taarifa kuhusu
Rwanda na Uganda, kutotumia Bandari ya Dar es Salaam lisitazamwe kisiasa.
Bandari ya Dar es Salaam ina udhaifu mkubwa unaolalamikiwa na wafanyabiashara
wa ndani na nje ya nchi. Siyo Rwanda na Uganda tu ndiyo wanaoilalamikia bandari
ya Dar es Salaam, bali Kongo, Zambia na Malawi pia wanalalamika. Bandari ya Dar
es Salaam ina sifa ya ucheleweshaji wa kupakua shehena za mizigo toka kwenye
meli, wizi wa mizigo, yakiwamo makontena na vifaa vya magari kama vile taa na
redio; uchakachuaji wa mafuta; urasimu na ucheleweshaji wa mizigo kutoka
bandarini; ukubwa wa tozo za bandari na barabara; na ugumu wa magari ya mizigo
kufika na kutoka bandarini, taratibu za kutoaa mizigo zisizotabirika na rushwa
bandarini na barabarani.
Asilimia 90 ya
biashara yote ya Tanzania na nchi za nje inapita katika bandari ya Dar es
Salaam. Nchi sita za jirani – Malawi, Zambia, Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda
ambazo hazina bandari zinaitumia bandari ya Dar es Salaam. Hata hivyo bandari
ya Dar es Salaam inakabiriwa na ushindani mkubwa kutoka bandari ya Mombasa
inayofanya kazi kwa ufanisi mzuri zaidi. Bandari ya Beira Msumbiji ina
ushindani mkubwa kwa mizigo inayoenda Malawi, Zambia na hata Kongo.
Bandari ya Dar
es Salaam haifanyi kazi kwa ufanisi. Utafiti wa Benki ya Dunia unaonyesha kuwa,
ikiwa bandari ya Dar es Salaam itafanya kazi kwa ufanisi kama bandari ya
Mombasa, pato la taifa la Tanzania litaongezeka kwa dola bilioni 1.8 kila mwaka
sawa na asilimia 7 ya pato la taifa la sasa. Nchi jirani zinazotumia bandari ya
Dar es Salaam zitaongeza mapato yao kwa dola milioni 800. Utendaji mbovu wa
bandari zetu unatokana na ombwe la uongozi, ufisadi na menejimenti mbovu.
Tanzania
inaweza kukuza uchumi wake kwa asilimia 10 kila mwaka na kuongeza ajira kwa
wingi ikiwa itatumia fursa za jiografia zikiwemo bandari zake kuwa kituo cha
usafirishaji, viwanda na biashara kwa nchi sita zinazopakana na Tanzania na
ambazo hazina bandari.
Serikali
inaelewa wazi utendaji wa bandari ya Dar es Salaam ni mbovu na hauridhishi.
Hata hivyo, kwa sababu ya ombwe la uongozi, serikali inasuasua kufanya
mabadiliko yanayohitajika kuongeza tija na ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam.
Uzembe wa
utendaji wa bandari ya Dar es Salaam unasababisha msongamano wa meli zenye
mizigo ya kushusha bandarini. Ukisafiri kwa ndege kati ya Zanzibar na Dar es
Salaam unaweza kuhesabu meli zaidi ya ishirini zilizoweka nanga zikisubiri
kupewa ruhusa ya kwenda gatini kushusha mizigo. Katika mwaka 2012 muda wa meli
kusubiri kupata gati la kushushia mizigo bandari ya Dar es Salaam ilikuwa siku
10 ukilinganisha na chini ya siku moja bandari ya Mombasa. Hata baada ya
makontena kupakuliwa inachukua muda mrefu – wastani wa siku 10 au zaidi
kushusha mizigo na kupata kibali cha kuisafirisha toka bandarini.
Ukilinganisha
na bandari ya Mombasa gharama za bandari ya Dar es Salaam ni za juu kwa
asilimia 22 kwa kila kontena. Gharama za tozo na ushuru mbalimbali za bandari
ya Dar es Salaam ni za juu kwa asilimia 74 ukilinganisha na bandari ya Mombasa.
Kwa kila dola 100 za gharama ya kushusha mizigo Mombasa, gharama ya kushusha
mizigo hiyo hiyo Dar es Salaam ni dola 174. Katika hali hii tusistaajabu nchi
jirani kuikimbia bandari ya Dar es Salaam.
Utendaji wa
Shirika la Reli umeporomoka sana. Shirika la Reli lilisafirisha mizigo ya tani
15400 mwaka 2012 ukilinganisha na tani 1446000 mwaka 2002. Kuanguka kwa
shirika la reli pia kunachangia uharibifu mkubwa wa barabara kwani mizigo
mizito inayostahiki kusafirishwa kwa garimoshi inasafirishwa kwa malori yenye
uzito zaidi ya viwango vya barabara. Ikiwa reli ya kati itanya kazi kwa ufanisi
na tija ya hali ya juu. Nchi za Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda wanaweza
kutumia reli ya kati kusafirisha mizigo yao kwenda na kutoka Dar es Salaam.
Reli ya TAZARA
haijatumiwa kwa kadri ya uwezo wake. TAZARA ilisafirisha mizigo ya tani 259,000
mwaka 2012 ukilinganisha na tani 677,000 mwaka 2002. Kwa kawaida usafiri wa
reli ni wa gharama za chini ukilinganisha na usafiri wa barabara. Tuna wajibu
wa kuimarisha utendaji wa Shirika la Reli na TAZARA ili kuongeza ushindani wa
kibiashara na kukuza uchumi wetu.
Kuhusu
Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki Rais alieleza kuwa “Katika Mkutano wa
14 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012,
Nairobi, tulipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka
kuanzishwa kwa Shirikisho. Mkutano huo uliagiza nchi wanachama
kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia Shirikisho la Kisiasa na mpango
wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu.
Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri litawasilisha mapendekezo ya majadiliano
hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi mwezi Novemba, 2013. Iweje leo
wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika
Mashariki.”
Rais Museveni
amekuwa mstari wa mbele kuharakisha kufikia Shirikisho la Kisiasa. Wachambuzi
wa siasa za Uganda wanaamini ana lengo la kuwa Rais wa kwanza wa Shirikisho la
Afrika Mashariki. Tanzania imekuwa kikwazo kwani Watanzania wengi wanaamini
haraka haraka haina baraka. Wanataka ushirikiano wa Afrika Mashariki ufuate
hatua zilizoanishwa katika Mkataba ulioanzisha Jumuiya ambazo ni Umoja wa
Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Sarafu na Fedha, na hatimaye Shirikisho la
kisiasa litakalopigiwa kura ya maoni na kila nchi.
Katika suala la
soko la pamoja Tanzania imesita kuruhusu masuala ya ardhi, ajira na uhamiaji
yaingizwe mara moja katika soko la pamoja la Afrika Mashariki. Nchini Kenya
suala la ardhi linaendelea kuleta mvutano mkali. Ni muhimu kwa serikali kuwa
makini sana katika sera ya ardhi, wananchi wasiporwe ardhi yao.
Hata hivyo
tusiwe na wasiwasi Shirikisho la Kisiasa la Kenya, Uganda na Rwanda ni ndoto ya
mchana. Katika karne ya 21, shirikisho la kisiasa lazima lijikite katika mfumo
wa demokrasia. Kenya imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa demokrasia lakini
bado hawajafanikiwa kujenga umoja wa kitaifa. Mpaka hivi sasa Rais Kenyatta
anasuasua kufanya ziara kamili Kenya ya magharibi. Rwanda na Uganda ni utawala
wa kidikteta. Rais Museveni alibadilisha katiba na kuondoa kipengere cha ukomo
wa mtu mmoja kuchaguliwa kuwa Rais. Kipindi cha mwisho cha Rais Kagame
kinamalizika mwaka 2017 na tayari kuna kauli kuwa wananchi wa Rwanda wanataka
aendelee kuwa Rais baada ya 2017.
Kitendo cha
kuvunja taratibu na itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kinaonyesha
wazi kuwa viongozi hawa hawaaminiki. Ikiwa hawakuheshimu makubaliano ndani ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaweza pia baadhi yao wasiheshimu makubaliano
baina yao.
CHANGAMOTO KWA
TANZANIA
· Tujenge umoja
wa kitaifa wa dhati unaojikita katika kuheshimu hakimu na kujenga misingi imara
ya demokrasia. Tuendelee kuhakikisha mchakato wa kupata katiba mpya unakuwa
shirikishi.
· Tuimarishe
miundombinu na ushindani wa kiuchumi wa Tanzania
· Tujenge uchumi
unaotumia vizuri rasilimali za nchi na ukuaji wa uchumi unaongeza ajira na
kuwanufaisha wananchi wote
·
Tuimarishe vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viwe na
maadili ya juu na vifanye kazi kwa weledi
Imetolewa na Prof.LipumbaMwenyekiti CUF-Chama cha wananchi

No comments:
Post a Comment