Meneja Mifumo ya Uchambuzi ya Kompyuta wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Bw. Mohamed Mashaka akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) utaratibu wa kuweka majina kwenye mbao za matangazo ya vituo vya usajili ili wananchi waweze kuhakiki usahihi wa majina yao.Kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhifadhi Hati toka Mamlaka hiyo Bw. Thomas Willium.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhifadhi Hati wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Thomas Willium akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) ,kifaa cha kuchukulia alama za vidole (mobile enrolment unit). Wakati wa mkutano uliofanyia katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo Jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Hassan Silayo-MAELEZO)
Uchukuaji
alama za kibailojia waendelea Dar
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea
na zoezi la uchukuaji alama za kibailojia katika mkoa wa Dar es Salaam.
Zoezi hili linafanyika kiwilaya, hadi sasa NIDA
imefanikiwa kumaliza wilaya ya Temeke na ipo katika hatua za mwisho za
kukamilisha zoezi hili katika wilaya ya Ilala. Baada ya hapo itafuatia wilaya
ya Kinondoni.
Mamlaka inatambua kwamba
wapo waliokosa fursa ya kujiandikisha kwa wakati uliopangwa hivyo, imefungua
ofisi zake Kigamboni na Chang’ombe katika wilaya ya Temeke ili watu hao waweze
kupata huduma hiyo. Aidha, Mamlaka itafungua ofisi zake katika wilaya za Ilala
na Kinondoni kuhakikisha
huduma inasogea karibu zaidi na wananchi.
Mbali ya uandikishaji ofisi hizi pia zitahusika kutoa
huduma nyingine kama uchukuaji alama za kibaiolojia, kupokea na kutatua
malalamiko na matatizo mbalimbali ya wananchi yanayohusu Vitambulisho vya
Taifa.
Hatua inayofuata baada
ya kukamilika kwa zoezi la uchukuaji wa alama za kibailojia ni kupokea maoni ya
wananchi yanayohusu maombi ya vitambulisho yaliyopokelewa na baada ya hapo
ugawaji wa vitambulisho utaanza.
Ugawaji wa Vitambulisho
vya Taifa unatarajia kuanza Desemba 2013 kwa waombaji waliokamilisha hatua
zote.
Waombaji wanatakiwa kufika kwenye vituo vya usajili
kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni na nyaraka halisi za kuthibitisha
uraia na umri mathalan, cheti cha kuzaliwa, pasipoti, vyeti vya elimu ya msingi
na sekondari, leseni ya udereva, kitambulisho cha bima ya afya au kitambulisho
cha mpigakura.
Majina ya waombaji na tarehe ya kuchukuliwa alama za
vidole na picha yanabandikwa kwenye mbao za matangazo katika vituo vya usajili.
Kwa ajili ya ubora na mwonekano mzuri wa picha kwenye
kitambulisho, mwombaji anashauriwa kutovaa nguo nyeupe, kijivu au bluu mpauko
na kofia anapokuja kupiga picha.
Kitambulisho cha Taifa ni haki ya msingi ya kila raia,
mgeni mkaazi na mkimbizi halali mwenye umri wa miaka 18 na zaidi. Aidha, hakuna
malipo yoyote atakayotozwa mwombaji katika zoezi hili.
Imetolewa na Kitengo cha
Mawasiliano na Hifadhi Hati,
Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa-NIDA

No comments:
Post a Comment