Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi nchini Thobia Andengenye ambaye alikuwa miongoni mwa wachangiaji wakati wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuhusu mchango wa takwimu katika kufanikisha majukumu ya Jeshi la Polisi nchini.
Naibu Waziri wa Fedha Bi. Saada Mkuya akizungumza na wadau wa sekta mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika leo jijini Dar es salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza kabla ya ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika. Amesema kuwa Ofisi yake pamoja na majukumu mengine inaendelea kuhimiza matumizi ya takwimu kutoka katika vyanzo sahihi kwa mipango ya maendeleo.
Sehemu ya washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika
katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa leo jijini Dar es salaam.
Na Aron Msigwa –
MAELEZO.
IKIWA ni takribani miaka 20 tangu
kuasisiwa kwa Siku ya Takwimu Afrika, Serikali imesema ipo haja ya kufanyika kwa
tathmini ya ufuatiliaji wa takwimu zinazotolewa na mchango wake katika kupanga
mipango ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya
Siku ya Takwimu Afrika yaliyowashirikisha wadau wa sekta mbalimbali leo jijini
Dar es salaam, Naibu Waziri wa Fedha Bi. Saada Mkuya amesema kuwa maendeleo bora
huchangiwa na upatikanaji na matumizi ya takwimu Bora zenye kuelezea uhalisia wa
jamii husika.
Amesema Tanzania ikiwa miongoni mwa
nchi zinazothamini mchango wa takwimu katika maendeleo itaendelea kushirikiana
na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa matumizi ya takwimu sahihi yanapewa
kipaumbele katika kutatua kero mbalimbali nchini zikiwemo za ulinzi wa raia na
mali zao, elimu, Afya, Kilimo na ufugaji.
Bi. Saada amesema kuwa kutoakana na
umuhimu wa takwimu wapo baadhi ya watanzania wanaodhani kuwa takwimu zinatumiwa
na serikali pekee jambo ambalo si sahihi na kuwataka kuondoa fikra hizo kutokana
na umuhimu na mchango wake kuanzia ngazi ya familia.
“Ni vema sote tukaelewa matumizi ya
takwimu sahihi na mchango wake katika maendeleo kuanzia ngazi ya familia pia
kuondoa mtazamo kuwa takwimu zinatumiwa na serikali pekee na kusahau kuwa
takwimu zinagusa maisha ya kila siku ya watu na zina umuhimu mkubwa sana katika
kupanga mipango ya maendeleo” Amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza kabla ya ufunguzi wa maadhimisho hayo
amesema kuwa Tanzania kama zilizvyo nchi nyingine za bara la Afrika huadhimisha
Siku ya Takwimu Afrika kwa kuwa Ofisi yake pamoja na majukumu mengine
inaendelea kuboresha na kuimarisha matumizi ya takwimu nchini.
Dkt. Chuwa amesema kuwa takwimu ni
maisha ya kila siku ya mwanadamu na zina umuhimu katika nyanja zote na kuongeza
kuwa wabunge wanahitaji takwimu ili kupanga mipango ya maendeleo ya majimbo yao,
serikali nayo inahitaji takwimu ili iweze kutekeleza mipango ya maendeleo na
kutoa huduma stahiki kwa wananchi vilevile mashirika mbalimbali yanahitaji
takwimu sahihi ili yaweze kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka
Benki ya Dunia Bw. Thomas Daniel Witz akitoa salam za Benki ya dunia wakati wa
maadhimisho hayo amesema kuwa Benki ya dunia na washirika wa maendeleo
wanatambua na kuthamini mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ukusanyaji na
utoaji wa takwimu nchini Tanzania.
Amesema takwimu zinazotolewa
zinaongeza uwazi na uwajibikaji na kuongeza uwezo wa nchi kupanga mipango ya
maendeleo kwa wananchi wake.
“Napenda kuchukua fursa hii
kuipongeza Tanzania kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa maendeleo na mafanikio
makubwa ya utoaji wa takwimu ambazo sasa zinaiwezesha serikali na wadau kupanga
mipango yao ya maendeleo”
Naye Naibu Kamishna wa Jeshi la
Polisi nchini Thobias Andengenye ambaye alikuwa miongoni mwa wachangiaji wakati
wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi
la Polisi nchini amesema jeshi la polisi linathamini mchango wa takwimu katika
kufanikisha majukumu yake.
Amesema takwimu zinalisaidia jeshi la
polisi kutekeleza majukumbu mbalimbali yakiwemo ya ujenzi wa vituo vya polisi,
kurahisisha mgawanyo wa ajira kufuatana na mahitaji ya wilaya na mikoa,
uimarishaji wa mafunzo kulingana na uhitaji pamoja na kutambua ongezeko la
makosa na namna ya kukabiliana nayo katika maeneo mbalimbali
nchini.
No comments:
Post a Comment