TANGAZO


Monday, November 25, 2013

Iran washangilia mkataba kuhusu nyuklia

 


Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif
 

Umati mkubwa wa watu nchini Iran ulikusanyika kuwapokea wajumbe walioshiriki mazungumzo yaliyofanikisha kupatikana kwa mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa sita makubwa duniani, huku Israel ikiuita mkataba huo kuwa "kosa la kihistoria".
 
Rais Barack Obama alimpigia simu waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, akitafuta kumhakikishia mafungamano ya kweli ya Marekani kwa Israel.

 
Mkataba uliofikiwa Jumapili mjini Geneva ulisababisha kuporomoka kwa bei za mafuta ya petroli katika masoko, Jumatatu.
Iran imekubali kuzuia baadhi ya shughuli zake za kinyuklia ili kuweza kuondolewa vikwazo vya uchumi vyenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni Saba.

Akizungumza katika kipindi cha televisheni ya ABC,'This Week', waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema: "Israel itakuwa salama zaidi, eneo la Mashariki ya Kati, litakuwa salama zaidi."
Mamia ya watu wanaounga mkono mpango huo nchini Iran, waliwalaki wajumbe wa Iran walioshiriki mazungumzo ya mpango wa nyuklia, wakirejea mjini Tehran, Jumapili. Wajumbe hao wa Iran walifikia mkataba wa muda kuhusu mpango huo wa nyuklia na mataifa ya Marekani, Urusi, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani.
Wakiwa wamebeba maua na bendera za taifa la Iran katika uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran, walimpongeza waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, kuwa "balozi wa amani" na kuimba Hatutaki Vita, Hatutaki vikwazo, hatutaki kusalimu amri na hatutaki kutukanwa".

Akizungumza kupitia televisheni ya serikali ya Iran katika uwanja wa ndege, Bwana Zarif amesema Iran ilikuwa imejiandaa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha mkataba unafikiwa. Lakini amesema, mkataba huo wa muda, wa miezi sita uliotiwa saini mjini Geneva unaweza kusitishwa na Iran katika hatua yoyote ya utekelezaji wake:
"Hatua zote tutakazochukua, hatua za kujenga kuaminiana, zinaweza zikasitishwa na zinaweza kusitishwa haraka. Bila shaka, tunatumaini kwamba hatutakiwi kufanya hili."

Mtazamo kuhusu Iran

Mapema, Rais wa Marekani,Barack Obama alipongeza mkataba huo, akisema utasaidia kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia".
Benjamin Netanyahu: "Ni kosa la kihistoria"
Lakini Bwana Netanyahu amesema Israel haifungwi na mkataba huo, akisema kuwa ana wajibu wa kuzungumza hilo".

"Hatuwezi na hatutaruhusu utawala ambao unataka kuiangamiza Israel kupata njia za kutekeleza lengo hili."

Kauli yake imekuja wakati ilipobainika kuwa Marekani na Iran zilikuwa na mfululizo wa mazungumzo ya ana kwa ana katika miezi ya hivi karibuni, ambayo yamesaidia kuwepo kwa mazungumzo kati ya Iran na mataifa sita makubwa duniani.

Mazungumzo ya Marekani na Iran yalifanyika kwa siri, na hata nchi washirika walifichwa kuhusu mazungumzo hayo.
Mataifa makubwa duniani yanashuku kwamba mpango wa nyuklia wa Iran unalenga kutengeneza bomu la nyuklia, madai ambayo Iran imeendelea kukanusha.

No comments:

Post a Comment