Ofisa Habari wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Emmanuel Mluga (kushoto), akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) na kuwataka kuuelimisha umma juu ya umuhimu wa vijana kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wakati wa mkutano, uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Ofisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO), Frank Mvungi. (Picha zote na Hassan Silayo - MAELEZO)
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Luteni Kanali Juma Sipe (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari, Idara ya Habari, Maelezo, Dar es Salaam leo, wakati alipokuwa akielezea Mpango wa Serikali kupitia Wizara hiyo, kuendelea kuboresha mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria. Kulia ni Ofisa Habari wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Emmanuel Mluga.
WIZARA ya Ulinzi na JKT itaendelea kuboresha
mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria. Hatua hii inafuatia kurejeshwa upya kwa
mafunzo hayo kama Serikali ilivyokuwa imeahidi.
Mafunzo hayo yaliyoanza
mapema 2013 yanatarajiwa kuwahusisha vijana 41,341 waliomaliza kidato cha sita
katika shule mbali mbali nchini.
Katika awamu ya kwanza vijana
5,000 (12%) walitakiwa kuhudhuria
mafunzo kwa muda wa miezi mitatu kuanzia mwezi Machi 2013 hadi Juni 2013.
Awamu ya pili ya mafunzo
hayo iliyoanza mwezi Juni JKT ilitarajiwa kuchukua vijana 10,000 (24%) na kumaliza mafunzo yao mwezi Septemba
2013. Katika awamu ya tatu
itakayoanza mwezi Oktoba 2013 JKT itachukua vijana 15,000 (37%). Aidha, awamu ya nne JKT itachukua
vijana 11,341 (27%) mwanzoni mwa Januari 2014 na vijana hao watamaliza mafunzo
mwezi Aprili, 2014 na hivyo kukamilisha idadi ya vijana waliomaliza kidato cha
sita kwa mwaka 2013.
Utoaji wa mafunzo haya
kwa miezi mitatu mitatu unafuatia maagizo ya Serikali kwani kwa muda wa miezi
sita iliyokusudiwa wakati wa kurejesha mafunzo hayo ni wazi vijana wengi
wasingepata fursa hiyo adhimu.
Changamoto kubwa zinazolikabili
JKT ni pamoja na hofu wanayokuwa nayo wazazi kutokana na visingizio wanavyopewa
na vijana baada ya kuwasili makambini. Tunawaasa wazazi kutojengewa hofu kwa
taarifa zisizo rasmi wanazopewa na watoto wao kwani Wizara ilizifanyia kazi
hofu zilizoelezwa na vijana na kubaini kuwa hazina ukweli. Kwa mfano, mtoto
anadai kuwa anaumwa na hapati matibabu, lakini tunapofuatilia tunamkuta yupo
kwenye gwaride (mzima wa afya. Chakufurahisha baadhi ya vijana hao hao wakati
wa kumaliza mafunzo wamekuwa hawana haraka tena ya kuondoka makambini!
Pili, lipo tatizo la
kukwepa mafunzo (dodging). Mfano katika awamu ya kwanza tulitarajia kupokea
vijana 5,000 lakini waliojitokeza ni 4,712 (vijana 288 wakiwa wamekwepa
mafunzo). Katika awamu ya pili kati ya vijana 10,000 ni vijana 9,510 tu ndio
waliojitokeza, (watoro 490). Tunapenda kuwahakikishia wote wanaokwepa mafunzo
kuwa wataendelea kufuatiliwa na mara watakapopatikana hatua za kuwarejesha
katika mafunzo zitachukuliwa.
Changamoto ya tatu ni
kutopatikana kwa huduma za mtandao (internet) makambini. Wizara inatambua
umuhimu wa mtandao na hivyo juhudi zitafanyika siku za usoni kuyaunganisha
makambi kwa kadri mkonga wa Taifa unavyozidi kuenea nchini. Hata hivyo, kijana
anayekuwa mafunzoni kwa miezi mitatu atajikuta hana muda wa kutumia huduma hiyo
kutokana na majukumu aliyonayo. Kwa wanaoomba nafasi vyuo vya elimu ya juu upo
utaratibu wa kuwaruhusu kutumia huduma zilizo nje ya makambi.
Aidha, JKT linakabiliwa
pia na changamoto ya kutoa mafunzo kwa muda mrefu zaidi kutokana na maombi ya
vijana wanaomaliza na pia maombi ya waheshimiwa wabunge. Hii ni ishara njema ya
kuona umuhimu wa mafunzo yanayotolewa na kwa kadri makambi yatakavyoongezeka
nchini suala la muda wa mafunzo pia litaangaliwa.
Changamoto nyingine ni
miundombinu michache ikilinganishwa na idadi kubwa ya vijana wanaotarajiwa
kumaliza kidado cha sita na vyuo kila mwaka. Suluhisho la jambo hili
litapatikana baada ya kupanuliwa kwa makambi ya JKT.
Wizara inaendelea kushirikiana
na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kuwa na mpango utakaohakikisha
vijana wanaofaulu vizuri wanapata mafunzo mapema na kuwawezesha kujiunga na
vyuo vya elimu ya juu kwa wakati. Kwa wale wanaojiunga sasa na ambao tayari
wamedahiliwa, Wizara imewasiliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili
kupata orodha yao na hatimaye kuwawekea utaratibu wa kujiunga na mafunzo hayo
baada ya kumaliza masomo yao.
Imetolewa na Luteni
Kanali Juma Nkangaa Issa Sipe,
Msemaji, Wizara ya
Ulinzi na JKT,
No comments:
Post a Comment