TANGAZO


Monday, October 7, 2013

Wizara ya Sheria na Katiba yaelezea utekelezaji wa programu ya maboresho ya sekta ya Sheria

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Katiba na Sheria, Farida Khalfan, akielezea kwa waandishi wa habari, mpango wa Serikali wa kuongeza fursa za upatikanaji na utoaji wa haki kwa wote, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO), Frank Mvungi. (Picha na Fatma Salum-Maelezo)

Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Katiba na Sheria, Emmanuel Mayeji, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu hatua za utekelezaji wa Program ya Maboresho ya Sekta ya Sheria, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), jijini Dar es Salaam leo.

WIZARA ya Katiba na Sheria inatekeleza na kuratibu Maboresho ya Sekta ya Sheria chini ya Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuboresha na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma za kisheria za usimamiaji na utoaji wa haki kwa wote na kwa wakati.
Lengo la programu hii ni kuboresha miundombinu iliyopo na kuongeza fursa za upatikanaji na utoaji haki kwa wananchi wote hasa wanyonge.
Maboresho haya yamejikita katika maeneo makubwa matatu moja ni kuongeza ufanisi na kusimamia ubora wa huduma ya kutoa haki kwa wote. Nia kubwa ya Serikali katika lengo hili ni kuboresha mazingira ya utendaji kazi ili kuongeza ufanisi wa kusimamia utoaji wa huduma za kisheria na kusimamia haki nchini, ili kutekeleza lengo hili  kuna mikakati iliyopangwa ambayo ni kuboresha miundombinu ya majengo na mifumo ya kupokea na kutunza kumbukumbu na nyaraka za mashauri katika idara ya Mahakama hasa Mahakama Kuu.
Eneo lingine katika uboreshaji wa sekta ya sheria ni kuboresha ujuzi na kuimarisha taaluma ya Uanasheria nchini. Serikali ina lengo la kuboresha taaluma ya sheria inayotolewa kwa wanafunzi wa sheria hasa elimu ya vitendo ili kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati. Ili kutimiza lengo hili Serikali imejenga chuo cha Uanasheria kwa vitendo  na kuweka miundombinu ya kudumu pamoja na vitendea kazi vitakavyosaidia ufundishaji wa vitendo kwa wanafunzi hao ikiwemo mahakama.

Serikali pia imeongeza wigo na kuboresha mazingira ya fursa za upatikanaji wa haki nchini kwa kuboresha mazingira ya upatikanaji wa haki kwa wananchi wote kwa kusogeza huduma za kisheria karibu na wanannchi kwa kujenga mahakama za mwanzo na kuanzisha chombo cha kuratibu huduma za msaada wa kisheria wa wananchi wasiokuwa na uwezo.
Aidha, tangu kuanzishwa kwa programu hii mafanikio mbalimbali yamepatikana yakiwemo, kutenganishwa kwa shughuli za upelelezi na zile za uendeshaji wa mashitaka, kuanzisha ofisi za Mkurugenzi wa Mashitaka Mikoani na Wilayani ambapo hadi sasa ofisi hizo zipo katika Mikoa kumi na tano na Wilaya kumi na saba.
Mfumo wa usafirishwaji wa mahabusu  na wafungwa, Ukarabati na ujenzi wa Mahakama 10 katika ngazi mbalimbali na uanzishwaji  na ujenzi wa Taasisi ya Mafunzo yaUanasheria kwa vitendo ni miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kupitia programu hii.
Mbali na mafanikio hayo kuna changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa programu zikiwemo ucheleweshwaji wa utolewaji wa fedha kwenye mfuko wa pamoja kwa upande wa wadau wa maendeleo na Serikali kushindwa kutimiza ahadi kwa wakati na kwa kiasi kilichokubaliwa.
Kwa kiasi kikubwa Serikali inajitahidi kuboresha miundombinu na mifumo yake ya kiutendaji kwa lengo la kutoa huduma bora za utoaji haki  kwa wananchi wake. Pia wanachi wanahimizwa kutafuta haki zao pale wanapoona wanaonewa.
Imetolewa na:
Wizara ya Katiba na Sheria,

No comments:

Post a Comment