TANGAZO


Monday, October 28, 2013

Tullow yasitisha uchimbaji Turkana, Kenya

 





Kampuni ya Tullow inashirikiana na Afrika Oil kuchimba mafuta baada ya kuyagundua mwaka 2012

Shughuli ya uchimbaji mafuta katika jimbo la Turkana Kaskazini Mashariki mwa Kenya, imesitishwa baada ya totafuti kuibuka kati ya wenyeji wa eneo hilo na wakuu wa kampuni iliyopewa kandarasi ya kuchimba mafuta ya Tullow.
Tullow imesema imefunga visima vyake viwili vya mafuta kwa sababu ya hofu ya usalama kufuatia maandamano ya wenyeji wakitaka kupewa nafasi zaidi za kazi katika sehemu wanakochimba mafuta.

Kampuni hiyo kupitia kwa vyombo vya habari ilisema kuwa imesitisha Shughuli hizo kwa kipindi kisichojulikana hadi utulivu utakapororejea katika eneo hilo.
Wenyeji wa eneo hilo walifanya maandamano mnamo siku ya Jumapili kulalamikia hatua ya kampuni hiyo kutowapa ajira katika shughuli za uchimbaji na badala yake kuwaajiri watu wasio wenyeji wa eneo hilo.
Shughili ya uchimbaji ilianza mwaka huu baada ya Tullow kugundua visima vya mafuta mwaka 2012 na inachofanya sasa ni kuangalia thamani ya mafuta ikiwa yanaweza kuleta mapato kwa nchi.
Aidha Tullow ilisema kuwa kumekuwa na maandamano ya mara kwa mara na kutatiza shughuli zake kuchimba mafuta. Baadhi ya viongozi katika eneo hilo wanaluamu wanasiasa kwa kuwachochea wakaazi kufanya maandamano na kuwa kwa sasa yamegeuka na kuwa ya vurugu pamoja na kutishia usalama.
Hata hivyo kampuni hiyo imesisitiza kuwa inashauriana na jamii za eneo hilo kuleta utulivu kwa njia ya amani kwani cha muhimu sasa ni kuhakikisha kuwa wafanyakazi wake hawadhuriki kwa vyovyote.
Wakaazi wa Kusini na Mashariki mwa Turkana walifanya maandamano kwa kile wanachosema ni kampuni hiyo kukosa kuwapa ajira na hata kandarasi katika shughuli nzima za uchimbaji.
Wakaazi hao walioongozwa na viongozi wao ikiwemo wabunge wakiituhumu kampuni hiyo kwa kuwahadaa na kuwanyima fursa za kazi huku wakikosa kutimiza ahadi yao ya kuhakikisha kuwa wakaazi hao wanapewa nafasi za kujiimarisha kiuchumi.
Hatua ya wakaazi ilikwamisha shughuli katika visima vya mafuta ambavyo viligunduliwa mwaka jana kuwa na uwezo wa kuzalisha viwango vikubwa vya mafuta. Wanataka kampuni hiyo kushughulikia kilio chao cha kuwapa nafasi za kazi.

No comments:

Post a Comment