TANGAZO


Sunday, October 20, 2013

Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation (BMAF), yapokea msaada wa Tsh mil. 50

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyoya Kiserikali ya Benjamin William Mkapa Foundation (BMAF), Dk. Ellen Senkoro (kulia), akisisitiza jambo wakati wa makabidhiano ya msaada wa kiasi cha Sh. milioni 50 za Kitanzania mbele ya waandishi wa habari na baadhi ya watumishi wa BMAF. Kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya AngloGold Ashanti Geita Gold Mine (GGM), Balozi Richard Mariki. 
Mkurugenzi wa Kampuni ya AngloGold Ashanti Geita Gold Mine (GGM), Balozi Richard Mariki (kushoto), akisisitiza jambo wakati wa makabidhiano ya msaada wa kiasi cha sh. milioni 50 za Kitanzania mbele ya waandishi wa habari na baadhi ya watumishi wa BMAF. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Benjamin William Mkapa Foundation (BMAF), Dk. Ellen Senkoro.
Mkurugenzi wa Kampuni ya AngloGold Ashanti Geita Gold Mine (GGM), Balozi Richard Mariki (kushoto), akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyoya Kiserikali ya Benjamin William Mkapa Foundation (BMAF), Dk. Ellen Senkoro, bahasha yenye nembo ya kampuni GGM, kama ishara ya kupokea msaada wa kiasi cha Sh. milioni 50 za Kitanzania mbele ya waandishi wa habari na baadhi ya watumishi wa BMAF. (Picha zote na Lorietha Lawrence-Maelezo) 

 TAASISI isiyo ya Kiserikali ya Benjamin William Mkapa Foundation (BMAF), imepokea msaada wa kiasi cha Sh. milioni 50 za Kitanzania kwa mwaka 2013 katika kutekeleza mpango mkakati wake wa miaka mitano kwa awamu ya pili kati ya mwaka 2012 hadi 2017.

Makabidhiano hayo yalifanyika hivi karibuni katika Ofisi za Makao Makuu ya taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa BMAF Dkt. Ellen Senkoro na Mkurugenzi wa Kampuni ya AngloGold Ashanti Geita Gold Mine (GGM) inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu Balozi Richard Mariki.

 Dkt. Senkoro alisema kuwa msaada huo kwa taasisis yake utatumika katika mradi wa kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa upande wa ugonjwa wa ukimwi (HIV/AIDS) na huduma kwa akinamama wajawazito na watoto wachanga (MNH) kupitia mpango unaosimamia kuimarisha afya ya rasilimali watu

“Taasisi yetu inaendelea na mpango wa kukusanya rasilimali kwa kuangalia malengo ya muda mrefu kupitia marafiki na wahisani mbalimbali wakiwemo GGM na makampuni mengine makubwa ndani na nje ya nchi.”alisema Dkt. Senkoro

Dkt. Senkoro alisema kuwa BMAF katika kipindi hicho cha miaka mitano inatarajia kukusanya jumla ya Sh. bilioni 12 za kitanzania ambapo lengo ni kukusanya Sh. bilioni tatu za kitanzania kwa mwaka ili kuboresha huduma za afya katika wilaya 15 nchini.

Dkt. Senkoro alisema kuwa lengo ni kufikisha huduma kwenye wilaya 15 nchini ambapo tayari wilaya sita zimeanza kunufaika na mradi huo ambazo ni Kahama, Kishapu (mkoa wa Shinyanga), Sumbawanga vijijini, Kalambo na Nkasi (mkoa wa Rukwa), na Biharamulo (mikoa ya Kagera).

Wilaya nyingine zitakazonufaika na huduma hiyo kwa awamu ya pili zipo tisa ambazo ni Shinyanga vijijini, Meatu, Bariadi, Halmashsuri ya mji wa Sumbawanga,Maswa, Itilima, Busega, Mkoa wa kati-Pemba, na Chake- Unguja vijijini.

Aidha, Dkt. Senkoro alisema kuwa BMAF tayari imewaajiri watoa huduma 30 katika maeneo ya watabibu, manesi na watoa huduma wasaididzi wa maabara ili kufanikisha na kuboresha utoaji huduma na mradi huo kuwa endelevu.

Vivyo hivyo Dkt. Senkoro alisema kuwa BMAF inawhudumu 32 tayari ambao wanatoa huduma katika wilaya zilizoainishwa na itaendelea kuajiri wengine 30 katika Nyanja za kutoa huduma kwa wagonjwa wa ukimwi, huduma ya haraka kwa akinamama wajawazito ambazo ndizo nyenzo mahususi kwa kuokoa maisha ya akinamama hao wanapokuwa na matatizo wakati wa kujifungua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya AngloGold Ashanti Geita Gold Mine (GGM) inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu Balozi Richard Mariki alisema kuwa wanafarijika kuona msaada wanaotoa unatumika kulingana na maelengo yaliyokusudiwa.

Vivyo, Balozi Mariki ameishukuru BMAF kwa kuchagua kushirikiana na GGM katika kutoa huduma kwa jamii na ameahidi kuendelea kushirikiana nao kwani wote wanalenga kumhudumia mwananchi mhitaji.

Katika kutekeleza mpango mkakati wake wa awamu ya pili miongoni mwa wafadhili ambao BMAF inashirikiana nao ni NSSF, PPF, Shirika la Bima ya Afya la Taifa (NHIF), LAPF, kampuni ya SWISSPORT, Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Banki Kuu ya Tanzania, Banki ya NBC, NMB, CRDB, Stanbic, Serikali ya Ireland kupitia mfuko wa Irish na Shirika la ndege la Precision.

No comments:

Post a Comment