TANGAZO


Sunday, October 6, 2013

Marekani yaingia Barawe na Tripoli


Anas al Libi
Waziri wa Mashauri ya nchi za Nje wa Marekani, John Kerry, amesema kuwa mashambulio yaliyofanywa na wanajeshi wa kikosi maalumu cha Marekani nchini Libya na Somalia yanaonesha dhamira ya serikali ya Marekani kuwasaka wale wanaohusika na ugaidi.
Akizungumza nchini Indonesia, Bwana Kerry alisema Marekani haitasita katika vita vyake dhidi ya ugaidi.
Jumamosi makamando wa Marekani walishambulia nyumba mjini Barawe, Somalia, ambayo inadaiwa kutumiwa na kiongozi mmoja wa kundi la al-Shabaab aliyehusika na shambulio la kigaidi katika jumba la maduka la Westgate mjini Nairobi.
Baada ya mapambano makali ya risasi kikosi hicho cha Marekani kiliondoka.
Shirika moja la habari linamnukuu afisa mmoja wa Marekani akisema ilishindikana mjini Barawe kumteka au kumuua kiongozi huyo wa al-Shabaab anayesakwa.
Masaa machache baadae makamando wa Marekani walimkamata kiongozi wa al-Qaeda katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Anas al Libi alikuwa anasakwa kwa kuhusika na mashambulio dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania miaka 15 iliyopita.
Inaarifiwa kuwa Anas al Libi sasa anazuwiliwa nje ya Libya.

No comments:

Post a Comment