Na Mwandishi wetu, Zanzibar
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SMZ), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema atagombea urais hadi nguvu zitakapomuishia katika maisha yake.
Mbali na hilo amesema kuwa ataendelea kutetea nafasi yake ya Ukatibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), wakati uchaguzi mkuu wa chama hicho utakaoanza, Novemba Mosi mwaka huu.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alielezea miaka mitatu ya utendaji wa SMZ katika Awamu ya saba ya uongozi wa Serikali hiyo.
"Nitastaafu pale nitakapoishiwa nguvu, wengine wanaona Maalim ni kizingiti, aondoke, nasema siondoki ng'o.
Nitaendelea kuwatumikia Wazanzibari na ndiyo ahadi yangu kwao, nasema nikiwa mzima nitagombea urais na ukatibu mkuu wa chama changu.
"Mchakato wa uchaguzi CUF tayari umeanza na utafanyika katika matawi yote Novemba mwaka huu, na uchaguzi mkuu utafanyika mwakani pamoja na mkutano mkuu kati ya Mei na Juni mwakani na Inshaallah nitagombea tena," alisema Maalim Seif.
Akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa na Serikali hiyo ya pamoja inayoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na Chama cha Wananchi (CUF), alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali hiyo, moja ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kupandisha bei ya karafuu.
Alisema hali hiyo imewapa wakulima wa zao hilo ahueni, ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hatua iliyowafanya wananchi wengi hasa katika vijiji vya Pemba kujenga nyumba bora.
Katika sekta ya utalii, alisema Serikali inaendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kiuchumi ambayo imekuwa ikiongezeka, ambapo kwa mwaka jana pekee miradi sita na programu 18 zilianzishwa.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi alisema SMZ imeweza kuboresha maslahi yao kwa kuongeza mishahara ya wafanyakazi pamoja na kupandishwa vyeo ambapo pia mwaka 2011/12, Serikali ilishughulikia suala hilo.
Katiba Mpya
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya, Maalim Seif alisema, mchakato huo unatokana na dhana na fikra za Rais Jakaya Kikwete, ambapo kwa busara zake aliona miaka 50 imepita tangu uhuru, hivyo Watanzania wanahitaji Katiba Mpya ambayo itawashirikisha wananchi wote.
Alisema suala la kutoa maoni limekwisha, ambapo aliwataka watu kujadili rasimu ili kama ina mapungufu yatolewe na si kujadili au kutoa maoni.
"Maoni yalishatolewa, mimi nilitoa yangu nina uhakika yamezingatiwa, chama changu kimekubaliana na maoni yale, sasa kwanini nisimuunge mkono Rais, namwomba Mwenyezi Mungu mchakato huu uishe salama salimini maana wakati mchakato unaendelea wengine wanapinga Katiba isipite.
"Hata hivyo pamoja na azma njema ya kuifanya nchi yetu iwe na Katiba Mpya ifikapo mwakani, lazima tukiri kwamba changamoto nyingi zinaendelea kujitokeza katika suala hili.
"Mtakumbuka mfululizo wa matukio yaliyojiri hasa baada ya Serikali kuamua kuwasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, vurugu zilijitokeza bungeni na kusababisha baadhi ya wabunge wa upinzani wakiwamo viongozi wa kambi hiyo, kulalamika kutotendewa haki na kuamua kutoka nje, mambo ya ajabu kabisa.
"Baada ya yote yaliyotokea, Rais bado akafanya busara ya kukaa meza moja na viongozi wa vyama vyote vya siasa ili kuyajadili kwa upeo wake yanayolalamikiwa, kati ya madai ya msingi ni kwamba Zanzibar haikushirikishwa katika sheria hiyo pamoja na mambo mengine mengi," alisema.
Serikali ya kitaifa
Maalim Seif alisema Serikali ya umoja wa kitaifa itaendelea hadi pale wananchi watakapopiga kura za maoni.
"Wanasiasa wataendelea tu kupiga kelele, ndiyo, si kila mmoja anataka kuongoza, na inshaalah Serikali hii itaimarika zaidi ya hapa.
Hata hivyo, Maalim Seif aliwatoa hofu Wakristo Wakatoliki ambao mapema mwakani wanaadhimisha Jubilei ya miaka 150 ya kanisa hilo tangu kuanzishwa visiwani humo, kuendelea na mchakato wa sherehe hizo kwani Serikali inawalinda.
Tindikali
Maalim Seif alisema suala la matumizi ya risasi za moto na raia kumwagiwa tindikali, ni suala linalompa wakati mgumu.
"Pamoja na mafanikio hayo, lazima tukiri kuwa bado tunazo changamoto ambazo tunapaswa tusizifumbie macho, changamoto ambayo imejitokeza katika siku za hivi karibuni katika nchi yetu ni suala la vitendo vya hujuma, ikiwamo watu kumwagiwa tindikali," alisema.
Elimu
"Zamani darasa moja lilikuwa na wanafunzi 24 na 30, lakini sasa hivi si ajabu kukuta darasa lina wanafunzi 80 hadi 100 ambapo inabidi lisimamiwe na walimu wawili, mmoja anafundisha na mwingine anasimamia nidhamu."
No comments:
Post a Comment