TANGAZO


Friday, October 25, 2013

ICC,"Ruto sharti ashiriki kesi yote"

Naibu Rais wa Kenya William Ruto
Kiongozi huyo amekua the Hague kusikiliza kesi yake iliyoko mbele ya mahakama ya ICC
 
Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC imeamua sharti Naibu Rais wa Kenya William Ruto avihudhurie vikao vyote wakati wa kesi yake ambapo ameshtakiwa kutekeleza uhalifu wa kivita. Viongozi wa mashtaka walipinga uwamuzi wa awali ambapo Bw Ruto angekubaliwa kushiriki vikao vichache tu huku akitumia muda wake mwingi nchini Kenya.
 
Hata hivyo mahakama imesema licha ya uwamuzi huo, huenda akakubaliwa ruhusa ya kutokuwepo baadhi ya siku ikiwa kutatokea sababu maalum. Mawakili wa Ruto waliambia mahakama kwamba kiongozi huyo alistahili kuwepo nchini Kenya baada ya nchi hiyo kushambuliwa na wapiganaji wa AlShabaab ambapo walilenga jumba la biashara la Westgate.

Naibu Rais wa Kenya amekanusha kuhusika na machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/2008 ambapo takriban watu 1,200 walipoteza maisha na wengine laki sita kukimbia makaazi yao.Uwamuzi wa mahakama ya ICC huenda ukazidisha mgogoro kati yake na Muungano wa Afrika ambapo muungano huo umelalamikia ICC kwa kuwalenga viongozi wa Bara Afrika Pekee.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto na mtangazaji Joshua Arap Sang wameshtakiwa kwa kupanga na kufadhili machafuko ya baada ya uchaguzi ambapo watu wasiokuwa na hatia wakiwemo akina mama na watoto walipigwa risasi huku wengine wakikatwakatwa hadi kufa na magenge ya uhalifu.

Kesi dhidi ya Rais Kenyatta inatarajiwa kuanza mwezi ujao wa Novemba na mahakama ya ICC imemkubalia kuhudhuria ufunguzi na siku ya mwisho ya kesi dhidi yake pekee. Wachanganuzi wanasema ICC iko katika njia panda ambapo inakabiliwa na shinikizo za kimataifa kutoutamausha utawala wa Kenya.

No comments:

Post a Comment