TANGAZO


Wednesday, October 16, 2013

Dar Rotary Marathon 2013 ilivyofana jijini Dar es Salaam


Mshindi wa wanaume, Alphonce Felix akipongezwa na  Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi akimpongeza mshindi wa kwanza wa mbio za Dar Rotary Marathon kwa upande wa wanawake, Sarah Ramadhani.
Baadhi ya wanariadha wakichuana katika mashindano ya mbio za Dar Rotary Marathon zilizofanyika jijini Dar es Salaam juzi, zilizowashirikisha wanariadha kutoka nchi mbalimbali.
 
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Shirikisho la Riadhaa Tanzania (RT), Tullo Chambo akiweka namba ya mkimbiaji Zhakia Mrisho.  (Na Mpiga Picha Wetu)
 
Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA kutoka klabu ya Holili Youth Athletics Club ya Kilimanjaro, Alphonce Felix na Sarah Ramadhani jana walitamba katika mbio za nusu marathoni za Rotary Dar Marathoni.
 
Ushindi huo umewatoa kimasomaso Watanzania ambao mara nyingi wamekuwa wakivurugwa na Wakenya katika mbio mbalimbali zinazoandaliwa nchini Tanzania.
 
Kwa upande wa wanaume Felix alikuwa wa kwanza kwa kutumia saa 01:03:00:79 wakati Ramadhani alitamba kwa upande wa wanawake kwa kutumia saa 01:13:41:39 na kila mmoja aliondoka na Sh. Milioni 2, saa ya mkononi na medali za dhahabu.
 
Mkenya Daniel Muindi alimaliza wa pili kwa kutumia saa 01:03:34:17 kwa upande wa wanaume wakati kwa upande wa wanawake Mkenya mwingine Eunice Mutie alimaliza wa pili kwa kutumia saa 01:16:29:81.
 
Mary Naali ambaye ni bingwa mtetezi wa mbio hizo alimaliza watatu kwa kutumia saa 01:17:40:64.
 
Washindi wa pili wa mbio hizo kwa wanaume na wanawake kila mmoka aliondoka na Sh. Milioni 1 na watatu Sh. 500,000.
 
Washindi walikabidhiwa zawadi zao na Rais Mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa mgeni rasmi katika mbio hizo ambazo washindi wan ne hadi wa 10 kwa upande wa wanawake na wanaume, kila mmoja aliondoka na Sh. 100,000.
 
Felix akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mbio hizo alisema kuwa, zilikuwa ngumu na alishinda kwa sababu amefanya mazoezi vizuri katika kambi yao ya Holili mkoani Kilimanjaro.
 
Mbio hizo hufanyika kila mwaka Oktoba 14, ambayo ni Siku ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye ni Rais wa Kwanza wa Tanzania.
 
Mwinyi akizungumza baada ya kukabidhi zawadi hizo alisema kuwa, Watanzania lazima waenzi fikra za mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa akipiga vita sana ubaguzi wa rangi, dini, ukabila na mambo mengine yanayopinga amani.

No comments:

Post a Comment