*Serikali yatoa wito kwa wadau wa michezo kuendelea kuwekeza katika sekta hiyo
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diana Melrose, akipiga mpira kuashiria kuanza kwa Bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililohusisha vijana kutoka katika vituo 19 vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu vya jijini Dar es salaam. Kulia anayeonekana kudaka mpira huo ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diana Melrose (kulia) akikagua timu ya mpira ya FC Kigamboni kutoka Kituo cha kulelea watoto walio katika mazingira magumu cha Kigamboni kabla ya kuanza kwa michuano ya kuwania kombe katika bonanza lililovihusisha vituo 19 vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu vya jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Ubalozi wa Uingereza, British Council, Baraza la Michezo Tanzania na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo yakiendelea katika Viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Kibasila leo, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa British Council nchini Tanzania, Richard Sunderland akikagua timu ya mpira ya kituo cha kulelea watoto walio katika mazingira magumu cha Dogodogo leo, katika Viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Kibasila.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (kulia), akimvisha medali kijana Juma Abdul wa kituo cha kulelea watoto walio katika mazingira magumu cha Kigamboni leo, jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diana Melrose (kushoto), akizungumza jambo na Arafa Abdul kutoka kituo cha mpira wa miguu cha Twalipo (Twalipo Camp Soccer Foundation) leo, jijini Dar es salaam. Arafa Abdul alikua mmoja wa waamuzi wa Bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililohusisha vijana kutoka katika vituo 19 vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu vya jijini Dar es Salaam.
Washindi wa jumla wa Bonanza hilo, timu kutoka kituo cha kulelea watoto walio katika mazingira magumu cha Dogodogo wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi kutoka Wizara ya Habari, Ubalozi wa Uingereza, Baraza la Michezo Tanzania, Right to Play Tanzania mara baada ya kunyakua Kombe na medali mbalimbali.
Washindi wa jumla wa Bonanza hilo, timu ya mpira wa miguu kutoka kituo cha kulelea watoto walio katika mazingira magumu cha Dogodogo Centre, wakifurahia ushindi mara baada ya kutangazwa leo, jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diana Melrose (kulia), akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo mara baada ya kumalizika kwa Bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililohusisha vijana kutoka katika vituo 19 vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu vya jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa British Council nchini Tanzania, Richard Sunderland. (Picha zote na Aron Msigwa - MAELEZO)
Na Aron Msigwa -MAELEZO.
Dar es salaam.
SERIKALI imetoa wito kwa wadau
mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kuendelea kuwekeza katika sekta ya
michezo , kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana walio katika maeneo mbalimbali
nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabrile ametoa wito huo
leo jijini Dar es salaam wakati wa Bonanza la mchezo wa mpira wa miguu
lililowahusisha vijana kutoka katika vituo 9 vya kulelea watoto walio katika
mazingira magumu na shule zilizo jirani na vituo hivyo jijini Dar es salaam.
Prof. Elisante ameeleza kuwa
Tanzania kwa sasa ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya michezo na
kuongeza kuwa serikali kwa kuliona hilo inaendelea kuwezesha na kushirikiana na
wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa sekta hiyo inapiga hatua kutokana na mchango
wake katika katika kudumisha amani na upendo, kukuza ajira ,uzalendo na
ushirikiano.
“ Sekta ya michezo nchini sasa
inapiga hatua kwa kuwahamasisha vijana wengi kushiriki katika mashindano
mbalimbali na kutumia fursa zilizopo kujiajiri na serikali tutaendelea kutoa
msukumo kwa wadau mbalimbali kuingia katika juhudi hizi za kusaidia vikundi
mbalimbali vya michezo vilivyopo nchini” amesema Prof. Elisante.
Kuhusu Bonanza la mchezo wa mpira wa
miguu kwa vijana wanaoishi katika vituo vya kulelea watoto walio katika
mazingira magumu lililofanyika leo jijini Dar es salaam amesema wengi wa vijana
hao walikua wamekata tama kutokana na wengi wao kukosa wazazi kutokana na sababu
moja au nyingine na kuwataka vijana hao ambao wengi sasa wamefanikiwa kuendelea
na masomo yao katika ngazi mbalimbali kuzitumia fursa walizopata ili
kutowakatisha tama wafadhiri.
Amewataka vijana waliofanikiwa na
kupiga hatua kimasomo kuwasaidia wenzao ambao bado wanahitaji msaada walio ndani
ya vituo hivyo na wale ambao bado wako mitaani.
Kwa upande wake Balozi wa Uingereza
nchini Tanzania Bi. Diana Melrose ameeleza kuwa kufanyika kwa bonanza hilo
jijini Dar es salaam ni ishara kubwa ambayo imeonyesha kuwa vijana wengi walio
katika mazingira magumu wakipewa fursa wanafanya mambo makubwa.
Amewapongeza vijana hao kwa kuonyesha
mfano wa kushiriki katika bonanza la mashindano hayo ambapo washindi pamoja na
mambo mengine wamekabidhiwa medali huku kombe likienda kwa timu ya mpira wa
miguu ya kituo cha dogodogo cha jijini Dar es salaam.
Naye mratibu wa mashindano hayo
kutoka “British Council” Bi. Malula Nkanyemka ameeleza kuwa lengo la kuanzishwa
kwa mashindano hayo mbali na kuibua vipaji na kuwajengea uwezo vijana hao
kimichezo yanalenga kuwafanya vijana hao kujitambua na kuzitumia haki zao,
kucheza na kubadilisha tabia.
Mashindano hayo yaliyoratibiwa kwa
ushirikiano na Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, British Council, Rotary
Club, Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Right lo Play, Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo na wenyeji wa bonanza hilo shule ya sekondari Kibasila
yamefanyika katika viwanja vya michezo vya shule ya sekondari Kibasila
na
kuzishirikisha nyumba 9 za kulelea watoto walio katika mazingira magumu.
No comments:
Post a Comment