TANGAZO


Wednesday, October 23, 2013

Baraza la Ushindani laelezea kuhusu umuhimu wa baraza kwenye mfumo wa ushindani na udhibiti wa Soko

Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Uchumi wa Baraza la Ushindani (FTC), Nzinyangwa Mchani akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani), ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo, Jijini Dar es Salaam, kuhusu umuhimu wa baraza kwenye mfumo wa ushindani na udhibiti wa Soko pia namna wanavyoshughulikia rufani zinazofikishwa kwenye baraza hilo. Kushoto ni Ofisa wa Sheria Mwandamizi wa Baraza hilo, Hafsa Said. (Picha na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)

Utangulizi
Ndugu Waandishi wa Habari, mada yetu ya leo inahusu nafasi na umuhimu wa Baraza la Ushindani kwenye mfumo wa ushindani na udhibiti wa soko hapa nchini. Katika mada hii tunatarajia kuuelezea mfumo wa ushindani na udhibiti wa soko ulivyoanza hapa nchini, ushindani ni nini, udhibiti unaangalia nini na unazingatia nini, nafasi ya Baraza la Ushindani na umuhimu wake. Hivyo, ili kuweza kuielezea vizuri mada yetu na kuwawezesha kuandika vizuri, mada hii tumeipanga katika sehemu kuu tatu kama ifuatavyo:

  1. Mabadiliko ya kiuchumi ya mwaka 1986;
  2. Kuanzishwa kwa Mfumo wa Udhibiti wa soko; na
  3. Nafasi ya Baraza la Ushindani na umuhimu wake.
Mabadiliko ya kiuchumi ya mwaka 1986
Mwaka 1986, katika jitihada za kuboresha na kuimarisha uchumi, Serikali iliamua kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa uchumi kutoka kwenye mfumo wa uchumi hodhi (planned economy) na kufuata mfumo wa uchumi wa soko (Market Economy). Uamuzi huu ulikuwa hususan kwa ajili ya kuleta kiwango kizuri zaidi cha ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu. Mfumo wa uchumi wa soko unashirikisha kwa kiasi kikubwa sekta binafsi katika kuzalisha na kusambaza huduma na bidhaa sokoni. Wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya mipaka ya nchi hukaribishwa na kuhimizwa kuwekeza kwenye sekta za kiuchumi na kijamii. Wawekezaji wanakaribishwa pia kuwekeza hata kwenye yale maeneo ambayo yalikuwa yanawekezwa na Serikali peke yake. Aidha, Katika mfumo huu huduma na bidhaa sokoni hutolewa na kuuzwa kwa ushindani. Katika mfumo huu wa soko, tofauti na ule wa uchumi hodhi, maamuzi yote makubwa kuhusu uzalishaji na usambazaji wa huduma na bidhaa sokoni hufanywa kwa kutegemea mwelekeo na nguvu ya soko.  
 
Kuanzishwa kwa Mfumo wa Udhibiti wa soko
Sayansi ya masuala ya uchumi kwenye nyanja ya ushindani na udhibiti wa soko inafafanua kwamba; kimsingi ndani ya soko lolote kuna wadau wakuu watatu ambao ni Serikali, Mwekezaji na Mlaji. Wadau hawa wana utashi na maslahi tofauti. Serikali utashi wake mkubwa ni kuona kwamba (i) panakuwepo na huduma na bidhaa bora kwa wingi, (ii) bidhaa salama, (iii) bei nafuu, (iv) bidhaa za kuaminika na; (v) zinazoweza kuwafikia wananchi ikiwezekana wote na pia ikiwezekana zitolewe bure. Aidha, Serikali inataka mapato kwa njia ya kodi ili kujiendesha. Mwekezaji lengo lake la kwanza ni (i) uzalishaji kwa gharama nafuu (ii) kupata faida kubwa kwa haraka iwezekanavyo; na( iii) usalama na uhakika wa mwelekeo wa kisera. Masilahi pamoja na utashi wa Mlaji hayapishani sana na yale ya Serikali. Mlaji anataka (i) pawepo na huduma na bidhaa bora kwa wingi, (ii) bei nafuu hata ikiwezekana bure (iii)  usalama; na ( iv) usiri (privacy).

 

Uzoefu huo wa kisayansi unabainisha kuwa bila kuwa na wadhibiti huru katika sekta zile ambazo ili uzalishe ni lazima uwekeze kwa kiwango kikubwa (hususan za miundombinu, maji, mawasiliano, nishati) haitawezekana kupata uzalishaji wa kuaminika na endelevu. Panatakiwa pawepo chombo chenye nguvu na mamlaka ya kisheria kitakachokaa katikati ili kuweka usawa wa masilahi ya hao wadau wakuu watatu kwenye soko. Katika kuweka usawa wa masilahi hayo hapana budi kutenganisha bayana majukumu ya kisera, ya kiudhibiti na ya kibiashara na pawepo na usahihi wa nafasi na mgawanyo wa majukumu hayo bila ya kuwa na muingiliano.

 

Halikadhalika, kuna sekta ambazo ili uzalishe si lazima uwekeze kwa kiwango kikubwa sana kama zile za miundombinu. Katika sekta hizi ushindani ni mkali sana, nazo zinatakiwa kuwa na muangalizi au msimamizi huru mwenye mamlaka na nguvu ya kisera na kisheria. Msimamizi huyu atasimama kama muamuzi (referee) huru wa  ushindani sokoni ili soko lisiwe huria au holela na kuleta migongano na mivutano ya kimasilahi. Soko likiachwa bila muamuzi kamwe malengo ya kisera yaliyokusudiwa hayatafikiwa. Hivyo, Serikali ikaamua kutenganisha majukumu ya kisera, kiudhibiti na kibiashara ili kuleta ufanisi katika utendaji wa soko.

 

Hali ya soko kuwa huria na holela ilianza kujitokeza hapa nchini katikati ya miaka ya themanini (1980) mwanzoni mwa kipindi cha mara baada ya mabadiliko ya uchumi. Lakini Serikali iliazimia kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa ushindani sokoni pamoja na udhibiti kwenye sekta za miundombinu, huduma za maji, nishati na mawasiliano.  Hivyo kuanzia mwaka 1994 na kuendelea Serikali ilifanya mabadiliko makubwa ya kiudhibiti (regulatory reforms) na kuanzisha mamlaka mbalimbali za udhibiti. Kwa kutumia Sheria zilizopitishwa na Bunge, Serikali ilianzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA), na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA). Aidha mwaka 2003, Bunge lilipitisha Sheria ya Ushindani. Serikali kupitia Sheria hii ya Ushindani Na 8/2003 iliunda vyombo vitatu muhimu ambavyo ni (i) Tume ya Ushindani (FCC), (ii) Baraza la Ushindani (FCT) na (iii) Baraza la Taifa la Utetezi wa Mlaji (NCAC).

 

 

 

 

Madhumuni hasa ya uanzishaji wa vyombo hivi vyote ni kusimamia biashara ili zisifanyike kiholela, kuhakikisha panakuwa na ufanisi katika ugawaji na utumiaji wa rasilimali zilizopo na kuongeza kiwango cha uwekezaji, kukuza ubunifu (inovation), kuongeza tekinolojia, kuhakikisha ustawi wa mlaji na pia kuona kwamba soko na uchumi kwa ujumla vinakuwa na ufanisi. Madhumuni haya ndio yanayotoa maana halisi ya udhibiti wa uchumi wa soko.

 

Nafasi ya Baraza la Ushindani na umuhimu wake

 

Majukumu ya Mamlaka za udhibiti yanatofautiana kulingana na aina ya sekta, lakini kimsingi mamlaka hizo zinaangalia viwango vya mashariti ya uwekezaji, gharama za huduma, viwango vya bei za bidhaa na huduma, viwango vya ubora, usalama, mwenendo wa wawekezaji kulingana na masharti ya leseni pamoja na kutoa au kufuta leseni husika n.k. Tume ya Ushindani (FCC) inasimamia ushindani sokoni na jukumu lake kuu ni kuangalia uzingatiaji wa Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 na Sheria ya Alama ya mwaka 1963 (Mechandise Marks Act of 1963) kuhusiana na uingizaji wa bidhaa bandia sokoni. Kimsingi ushindani unaohusika hapa unaeleweka kama ni ule mchakato ambao wazalishaji au wasambazaji wa bidhaa na huduma mbalimbali wanaufuata kwa kufanya jitihada, kwa uhuru na kwa masilahi yao kuwavutia wateja ili kutimiza malengo yao ya kiuchumi kwa mfano kupata mauzo, faida na sehemu ya soko (market share) la hiyo bidhaa au huduma husika.  Sera ya Serikali kuhusiana na ushindani ni kuwa na ushindani wa dhati na wa haki na kuchukua hatua zinazorekebisha tabia potofu ya vyombo vya kibiashara sokoni.

 

Mfumo wa udhibiti ulioanzishwa unazingatia misingi ambayo ni uhuru na majukumu yasiyo na muingiliano, uwazi, uwajibikaji (accountability), kuaminika (predictability), na ushirikishaji wa wadau. Uwajibikaji unamaanisha kwamba, pamoja na Mamlaka ya udhibiti kuwa huru hainabudi kufanya kazi kwa ufanisi na kuzingatia misingi ya udhibiti. Ufanisi wa udhibiti wa sekta au ushindani kwenye soko unapatikana pamoja na mambo mengine, kwa kuhakikisha kwamba maamuzi au amri za mdhibiti zinapokosa utoshelevu, umakini au kutofuata sheria kwa makini zinaweza kupingwa mbele ya mahakama maalumu iliyo huru kwa njia ya rufaa.

 

Hivyo, Serikali ilianzisha Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal) ikiwa ni mahakama maalumu ya rufaa za maamuzi au amri za Tume ya Ushindani na mamlaka za udhibiti kwenye sekta za miundombinu na matumizi ya mawasiliano zilizotajwa kwenye aya zilizotangulia. Kwa hiyo Baraza la Ushindani ni ngazi ya juu na ya mwisho katika mfumo wa ushindani na udhibiti na umuhimu wake ni:

 

i)       Kuwa ngazi thabiti ya rufaa inayosikiliza kesi kwa haraka   na ufanisi katika mfumo wa ushindani na udhibiti ili uzalishaji na usambazaji wa huduma na bidhaa sokoni usicheleweshwe na milolongo mirefu ya kesi katika mahakama za kawaida;

ii)     Kuwa mahakama maalum (specialized) ambayo itajikita na kuelekeza rasilimali, jitihada na nguvu zake zote  katika kusikiliza na kuamua kesi za rufaa za ushinani na udhibiti tu kwa namna ya kipekee inayopunguza baadhi ya taratibu za kimahakama;

iii)   Kuharakisha mchakato wa usikilizaji wa rufaa za ushindani na udhibiti wa soko kwa kufuata taratibu na ujuzi maalum;

iv)   Kuwa nyenzo ya mwisho ya kurekebisha au kuthibitisha maamuzi na amri za Tume ya Ushindani na mamlaka za udhibiti kwenye sekta za miundombinu na matumizi ya mawasiliano zilizotajwa kwenye hii mada; 

 

v)     Baraza ni alama ya uhakika (provide assurance) wa ulinzi na uteteaji wa ushindani unaozingatia haki na kumlinda mlaji pamoja na mlalamikaji mmoja mmoja.

 

Hivi sasa Baraza limekamilisha maandalizi ya kusikiliza kesi kumi na moja (11) kati ya kumi na sita (16) zilizokamilisha taratibu za usajili. Kesi hizo zinatarajiwa kusikilizwa kwa wiki mbili mfululizo kuanzia tarehe 28 Oktoba 2013, mbele ya Mhe: Jaji Raziabegum Sheikh (Mwenyekiti) na Jopo la Wajumbe wa Baraza Dkt. Malima M.P Bundara, Bw. Gregory Ndanu, Bw Onesmo Kyauke, Bibi Nakazaeli Tenga, Prof. A.F. Mkenda na Bi Salma Maghimbi. Kesi hizo zitakaposikilizwa na kutolewa maamuzi zitachangia katika kurudisha ufanisi wa utendaji wa sekta husika ambao ulikuwa umekwamishwa na vipengele vilivyopingwa mbele ya Baraza, na hivyo kuwezesha sekta hizo kuendelea kutoa mchango wake wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kwa hiyo Baraza linawasihi wadau wake wote, wafanyabiashara na walaji kwamba waikumbuke hiyo nafasi ya Baraza katika mfumo wa ushindani na udhibiti wa soko, watambue umbuhimu wake na wasisite kulitumia pindi wanapohitaji kutatua migogoro yao katika soko kwa ujumla na kwenye sekta zilizotajwa.
Nzinyangwa E. Mchany
MKUU WA KITENGO CHA MASUALA YA UCHUMI
Simu 0754 720007

No comments:

Post a Comment