Safari za ndege za ndani ya nchi nchini Kenya zinatarajiwa kurejea kama kawaida baadaye leo baada ya moto mkubwa kuteketeza sehemu ya uwanja rasmi wa kimataifa wa ndege nchini humo JKIA.
Msemaji wa ikulu ya rais, Manoah Esipisu alisema kuwa ndege za mizigo zitaanza kusafiri lakini akaongeza kuwa serikali haiwezi kusema bayana ni lini safari za kimataifa za ndege zitarejea kama kwaida.
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta awali leo ulikua umefungwa baada ya moto mkubwa kutokea katika uwanja huo mjini Nairobi. Moto huo hata hivyo ulidhibitiwa"Tunatarajia kuwa safari za ndege ndani ya nchi zitaweza kurejea kama kawaida baadaye leo, '' alisema Esipisu.
Hakuna ripoti zozote za majeruhi .
Mwandishi wa BBC katika uwanja huo amesema kuwa kulikuwa na moshi mkubwa uliotoka katika eneo la kuondokea na kuingilia wageni.
Baadhi ya safari za ndege kutoka uwanja huo pia ziliahirishwa wakati zengine zikielekezwa kwenda Mjini Mombasa.
Mwishoni mwa wiki jana baadhi ya wenye maduka ya Duty Free katika uwanja huo walifurushwa baada ya serikali kusema kuwa leseni za wenye maduka zilikuwa zimepitwa na muda.
Huu ni moto mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika uwanja wa Jomo Kenyatta wenye kutumiwa na wasafiri wengi zaidi katika eneo la Afrika mashariki na kati .
Taarifa za awali zilionyesha kuwa moto huo ulianzia kwenye eneo la uhamiaji katika kitengo cha kupokea wageni kabla ya kusambaa hadi maeneo ya ushuru na mizigo ya abiria.
Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana , lakini maafisa wa ngazi ya juu wa serikali wakiongozwa na rais Uhuru Kenyatta walitembelea uwanja huo na kutoa wito uchunguzi ufanyike mara moja. Hata hivyo hawakutoa ishara yoyote ni lini uwanja huo utafunguliwa tena .
Shirika la ndege la kenya -Kenya Airways, ambalo ni kubwa zaidi katika kanda ya Afrika limefuta safari zake zote na kuelekeza ndege zinazoingia nchini katika mji wa Mombasa . Tayari hisa za ndege zimeshuka kwa kiwango cha asilimia 2 . Ndege za kimataifa ambazo zilitakiwa kuondoka leo asubuhi ziliruhusiwa kuondoka bila wasafiri.
No comments:
Post a Comment