TANGAZO


Friday, July 26, 2013

Serikali kupambana na ukosefu wa ajira kwa Wahitimu wa vyuo vikuu nchini



059
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Wizara ya Kazi na Ajira Ridhiwan Wema, akieleza kwa waandishi wa habari juu ya mpango wa Serikali kupitia wizara hiyo kukuza ajira kwa vijana wahitimu wa vyuo vya Elimu ya Juu katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa.
066
Afisa Kazi toka Wizara ya Kazi na Ajira Omari Hamisi, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu sheria mbalimbali za kazi zinazohitaji kutekelezwa na waajiri, katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo leo, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari,  Zamaradi Kawawa.
070
Mkurugenzi wa Ajira wa Wizara ya Kazi na Ajira Ally Ahmed, akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari juu ya mpango wa Serikali kupitia wizara hiyo, juu ya kukuza ajira kwa vijana wahitimu wa vyuo vya Elimu ya Juu katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari leo, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini wa wizara hiyo, Ridhiwan Wema. (Picha zote na Hassan Silayo)


Na Hassan Silayo- Maelezo
SERIKALI kupitia wizara ya Kazi na Ajira imepania kuondoa tatizo la ajira nchini kwa vijana wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu kwa kuanzisha mpango maalum utakaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu nchini,Taasisi za fedha na wabia wa maendeleo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo Ridhiwan Wema wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam. 

“Kutokana na tatizo la ajira nchini hasa  kwa wahitimu vyuo vikuu, Serikali kupitia Wizara ya Kazi na Ajira tumeamua kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu nchini,Taasisi za fedha na wabia wa maendeleo ili kuweza kukabiliana na changamoto hii” alisema Ridhiwan.
 
Katika kuhakikisha serikali inatekeleza azma hii tayari Wizara imeanzisha Idara ya kilimo, uchumi na Biashara katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (DAEA-SUA) na tayari Serikali imefanya makubaliano  na Benki ya CRDB kuanza utoaji wa mikopo kwa vijana mara  utekelezaji wa mpango huu utakapoanza.
 
Mpango huu ambao utatekelezwa kwa awamu tatu utaweza kuwawezesha vijana 30000 kupitia miradi 1000 inayolengwa kuanzishwa katika awamu zote.

Aidha Ridhiwani aliongeza kuwa uanzishwaji wa miradi hii inalenga kuwanufaisha wengi kwani miradi hiyo itawezeshwa na kuzalisha ajira kwa vijana wengine zaidi ya 26000 na hii ikiwa ni lengo la serikali kutimiza azma yake ya kuondoa tatizo la ajira kwa vijana nchini. 

Ridiwani aliongeza kuwa Jumla ya shilingi bilioni 54.451 zitahitajika kwa kipindi cha miaka 3 ya utekelezaji wa programu ambapo shilingi Bilioni 50 zitawekwa dhamana na shilingi bilioni 4.451 zitatumika katika mafunzo na kuwaandaa vijana ili waweze kukopesheka.
 
Utaratibu wa ukopeshaji ni wastani wa shilingi milioni 50 hadi 300 kulingana na mradi na Utaratibu wa utekelezaji na viwango vya riba utaainishwa katika mpango kazi wa utekelezaji program.

No comments:

Post a Comment