TANGAZO


Friday, July 19, 2013

Kituo cha Kuhifadhi Kumbukumbu za Kiswahili kuanzishwa


Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na mdau wa lugha ya Kwaswahili, Mohammed Seif Khatibu akitoa maoni kueleza umuhimu wa Kituo cha Kuhifadhi Kumbukumbu za lugha ya Kiswahili katika mkutano wa wadau wa Kiswahili uliofanyika Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam jana Alhamisi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mwakumbusho ya Taifa, Eliwasa Maro akizungumzia umuhimu wa Kituo cha Kuhifadhi Kumbukumbu za lugha ya Kiswahil.
Mwanazuoni na Mtaalamu wa Lugha ya Kiswahili, Profesa Mugyabuso Mulokozi naye alikuwa mmoja wa waliotoa maoni yao juu ya kuanzishwa kituo hicho. 
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Manedeleo ya Utamaduni Lilian Bereko akichangia jambo katika mkutano wa kujadili kituo hicho.
Kuanzia kulia Aliyekuwa Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na mdau wa lugha ya Kwaswahili, Dk. Mohammed Seif Khatibu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kuanzisha Kituo cha Kuhifadhi Kumbukumbu za Lugha ya Kiswahili Boniface Sanjura , Mkurugenzi Mkuu wa Mwakumbusho ya Taifa, Eliwasa Maro, Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Bao Tanzania, Monday Lukwepa na Afisa Utamaduni Habibu Msami waki, wakiwa wamesimama kumkumbuka marehemu Sijiana Saleh Mandevu aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha Ushairi Tanzania (UKUTA), aliyefariki Mei mwaka huu kwenye mkutano huo.
Mtaalamu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Aldin Mutembei akitoa maoni na kueleza umuhimu wa kituo hicho.Pia ameteuliwa kuandika mapendekezo juu ya kuanzishwa kituo hicho.
Wadau wa Kiswahili wakifuatia kwa makini mkutano wa kujadili Kituo cha Kuhifadhi Kumbukumbu za lugha ya Kiswahili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kuanzisha Kituo cha Kuhifadhi Kumbukumbu za Lugha ya Kiswahili Boniface Sanjura wa kwanza kushoto, akitoa maelezo kuhusu chumba kilichopo kwenye Makumbusho ya Taifa kilichotolewa kwa lengo la kuanzisha Kituo cha Kuifadhi Kumbukumbu za lugha ya Kiswahili. (Picha zote na Hussein Makame-MAELEZO)  


Na Hussein Makame, MAELEZO
MWANYEKITI wa Kamati ya Kuanzisha Kituo cha Kuhifadhi Kumbukumbu za Lugha ya Kiswahili Boniface Sanjura  amewataka wadau wa Kiswahili nchini kuwajibika katika kulinda kumbukumbu muhimu za Taifa ikiwemo lugha ya Kiswahili.
Mwenyekiti Sanjura alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam, wakati akiwatambulisha wadau wa Kiswahili chumba kilichotolewa na Kituo cha Makumbusho kwa lengo la kuhifadhia kumbukumbu za Kiswahili.

Alisema kituo hicho kitatumika kuhifadhi kumbukumbu muhimu za lugha ya Kiswahili ikiwemo vitabu, machapicho, picha za magwiji wa lugha hiyo na kazi za Kiswahili na kuwaomba wadau washiriki katika kufanikisha lengo kwa kukusanya kumbukumbu hizo.
Akizungumza kuhusu kituo hicho, mwenyekiti Sanjura alisema kituo hicho kitatumiwa wananchi ikiwemo wanafunzi kutoka ngazi zote za elimu kupata taarifa muhimu kuhusu lugha ya Kiswahili.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mwakumbusho ya Taifa, Eliwasa Maro alisema makumbusho yaliamua kutoa eneo hilo kwa ajili ya kituo hicho ili kuzifanya kumbukumbu muhimu za lugha ya Kiswahili kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho ikiwemoku kuwasaidia watafiti na wanafunzi.

Aliwaomba wadau wa Kiswahili kuhakikisha wanathamini mchango wa kituo cha Makumbusho kwa kufanyia kazi eneo walilopewa na iwapo hawatakitumia ofisi yake inaweza kuwakabidhi watu wengine wanaohitaji.

Akichangia juu ya uanzishwaji wa kituo hicho aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Micheo na Mtaalamu wa lugha ya Kiswahili Dk. Mohammed Seif Khatibu, alipongeza wazo la kuanzisha kwa kituo hicho kwani Kiswahili ni kitambulisho cha Watanzania na lugha ya ukombozi wa nchi za Afrika.

Dk Aldin Mutembei alisema nchi zote zinazojali historia na kuenzi maendeleo ya jamii, huweka kumbukumbu na kuwajulisha watu wajue wanapotoka, walipo na wanapoelekea kwani asiyejua anapokwenda huweza kupotea njia.

Alisema ameshuhudia vituo kama hicho katika nchi mbalimbali ikiwemo Uholanzi, Ujerumani, Denmark, Norway na Marekani katika jiji la Washington DC  ambako kuna kituo kikubwa inachokusanya taarifa za lugha na simulizi duniani.

Alisema kituo hicho ambacho yeye ameteuliwa kushughulikia uanzishwaji wake, kitasaidia kuhifadhi kumbukumbu za lugha ya Kiswahili na kwamba kuna utafiti unaofanywa kuhusu maandishi ya Waafrika kabla ya ujio wa Waarabu unaofanyika hapa Tanzania.
“Wakoloni wana kumbukumbu nyingi kuhusu maishayetu, hivi vituo nilivyovitaja, ukienda Berlin kuna kumbukumbu nyingi kuhusu Kiswahili kuliko tulizonazo hapa Afrika Mashariki, kwa hiyo kituo kama hiki kitawasiliana na vituo hivyo ili kurudisha kumbukumbu hizo muhimu tulizozipoteza wakati wa Ukoloni” alisema Dk. Mutembei.
Kwa upande wake Profesa Mugyabuso Mulokozi alisema wanahitaji kutafuta njia za kupata nyenzo ili kituo kifanye kazi na kwa kuwa lugha ya Kiswahili ni lugha ya Taifa na kuhifadhi amali zake linatakiwa liwe jukumu la Serikali.

Wazo la kuanzishwa kwa kituo hicho limekuja kutokana na kukosekana kwa sehemu ya kuhifadhi kumbukumbu muhimu za lugha ya Kiswahili katika kituo cha makumbusho ya Taifa. 

No comments:

Post a Comment