TANGAZO


Monday, June 10, 2013

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar, Omar Yussuf atoa mwelekeo wa Bajeti ya Zanzibar

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee akizungumza na waandishi wa habari, kuhusiana na Bajeti ya Serikali atakayoiwasilisha katika Baraza la Wawakilishi siku ya Jumatano 12/06/2013, mkutano uliofanyika ofisini kwake, Vuga mjini Zanzibar. (Picha zote na Yussuf Simai-Maelezo, Zanzibar)

Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria katika mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee kuhusiana na Bajeti ya Serikali atakayoiwasilisha katika Baraza la Wawakilishi siku ya Jumatano 12/06/2013, wakiwa katika mkutano uliofanyika ofisini kwake, Vuga mjini Zanzibar leo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee akisisitiza jambo, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusiana na mwelekeo wa Bajeti ya Serikali, atakayoiwasilisha katika Baraza la Wawakilishi, siku ya Jumatano 12/06/2013, mkutano uliofanyika ofisini kwake, Vuga mjini Zanzibar leo.



Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kutumia jumla ya shilingi bilioni 658.5 katika mwaka wa fedha utakaoanzia Julai mwaka huu.

Akitoa muhtasari wa bajeti kwa waandishi wa habari afisini kwake Vuga mjini hapa Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema bajeti hiyo ni ni ongezeko la wastani wa shilingi bilioni 45  ikilinganisha na ya mwaka unaomalizika.

Alisema hali hiyo imetokana na ongezeko la mahitaji ya wananchi na kuimarika kwa pato la taifa ambalo limefikia  wastani wa shilingi Milioni moja kwa mwaka kwa kila mwananchi na kupungua kwa mfumko wa bei toka asilimia 14.9 mwaka 2011 hadi asilimia 9 mwaka 2012.

“Serikali inawajibika kutoa huduma za jamii katika hali iliyo bora, kwa kuzingatia hilo na kutokana na kukua kwa hali ya uchumi na kuongezeka kwa pato la taifa tumelazimika kuongeza bajeti ukilinganisha na ya mwaka uluiopita ili kuleta ufanisi katika mipango ya serikali”, alisema.

Alizitaja sekta zilizopewa kipaumbele katika bajeti hiyo ni za afya, maji, kilimo  na elimu ambazo amesema zina mchango mkubwa na wa moja kwa moja katika uchumi na ustawi wa jamii.

“Sote tunajua matatizo yaliyopo katika upatikanaji wa maji safi na salama na dawa katika hospitali zetu, hii ndio sababu bajeti hii ikaziweka sekta hizi kuwa ndio kipaumbele chetu”, alisisitiza Waziri Yussuf na kuongeza kuwa serikali inatarajia kujitegemea yenyewe katika suali la upatikanaji wa dawa muhimu baada ya konekana viashiria vya kukoma kwa ufadhili wa mfuko wa pamoja wa sekta ya afya unaofadhiliwa na Global Fund.

Aidha alisema katika kuongeza pato la taifa na mwananchi mmoja mmoja serikali itaelekeza nguvu katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa uimarishaji wa mifumo ya umwagiliaji maji ili kukuza uzalishaji wa chakula nchini jambo ambalo amedai litapunguza uagiziaji wa chakula toka nje ya nchi.

“Tutakapozalisha chakula kwa wingi tutapunguza uagiziaji na kuongeza pato la taifa kwani hata nakisi ya bei itakuwa ndogo na kumuwezesha kila mwananchi kupata mahitaji yake muhimu kwa urahisi”, aliongeza Yussuf na kuwataka wananchi kuendeleza hali ya amani na utulivu iliyoko nchini ili kuvutia wawekezaji zaidi ambao watachangia kupunguza tatizo la ajira linaloikabili taifa.

Akizungumzia maslahi ya wafanyakazi katika sekta ya umma Yussuf alisema yataongezeka kama yalivyoahidiwa na Rais katika hutuba ya uzinduzi wa baraza la wawakilishi na Mei Mosi mwaka huu ikiwa na pamoja na kuongeza nafasi za ajira mpya kwa madaktari, mainjinia na kujaza mapengo yaliyowacha wazi na wafanyakazi waliostaafu katia kada mbali mbali.

Kuhusu hali ya uchumi Waziri Yussuf alisema unatarajiwa kukua katika mwaka ujao kutokana na kufanyiwa kwa marekebisho na kuondoshwa kwa baadhi ya kodi na kuimarisha mfumo wa udhibiti wa mapato ya serikali.

“Katika bajeti hii tumependekeza kufanyiwa nmarekebisho, kuondoshwa na kuanzishwa kwa baadhi ya kodi ili kutanua wigo wa ukusanyaji na udhibiti wa mapato ya serikali  jambo ambalo naamini litainua hali za wananchi wetu”, alisema.

Kwa mujibu wa waziri huyo kiasi hicho kinachopendekezwa kutumika katika mwaka huu wa fedha, asilimia hamsini inatokana na mapato ya ndani na kiasi kilichobakia kitatokana na ufadhili wa washirika wa maendeleo jambo ambalo amedai linatokana na mipango ya serikali ya kupunguza utegemezi kwa wafadhili katika bajeti.

Bajeti hiyo inatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano wa nane wa baraza la wawakilishi unaotarajiwa kuanza kesho (Jumatano) ijayo.

No comments:

Post a Comment