Waziri wa Fedha, Dk. Mgimwa |
DODOMA
6 Juni, 2013
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, kufuatia
taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Uchumi, Viwanda na Biashara, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu
likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2013/14.
2.
Mheshimiwa Spika,
naomba nitumie fursa hii kuishukuru kwa namna ya pekee Kamati ya Kudumu ya
Uchumi, Viwanda na Biashara chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Mahmoud Hassan
Mgimwa (Mbunge wa Mufindi Kaskazini) na Makamu wake Mheshimiwa Dunstan Luka
Kitandula (Mbunge wa Mkinga) kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyoyatoa kwa
Wizara wakati wa kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Fedha. Aidha,
nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti
Mheshimiwa Andrew John Chenge (Mbunge wa Bariadi Mashariki) pamoja na Kamati
nzima kwa ushauri wao makini.
Katika uandaaji wa hotuba hii, Wizara imezingatia ushauri na mapendekezo
ya Kamati hizo pamoja na ushauri na maoni ya hoja mbalimbali zilizotolewa
wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara kwa mwaka 2012/13.
3.
Mheshimiwa Spika,
napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Saada
Mkuya Salum (Mb) na Mheshimiwa Janeth Zebedayo Mbene (Mb). Aidha, napenda kutoa
shukrani za dhati kwa Wakuu wa Idara na Vitengo, Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha
wakiongozwa na Katibu Mkuu, Ndugu Ramadhan M. Khijjah na Naibu Makatibu Wakuu
Dkt. Servacius B. Likwelile, Ndugu Elizabeth J. Nyambibo pamoja na aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu Ndugu Laston T. Msongole kwa kazi kubwa waliyoifanya ya
kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Vile vile, napenda kuwashukuru
Profesa Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Ndugu Harry Kitilya,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na Wakuu wa Taasisi na Wakala wa Serikali,
chini ya Wizara kwa michango yao katika kuboresha utekelezaji wa majukumu ya
Wizara.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA
MWAKA WA FEDHA 2012/13 NA MALENGO YA MWAKA 2013/14
4.
Mheshimiwa Spika,
uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa Mpango na Bajeti
ya Wizara unazingatia mambo yafuatayo: Malengo ya maendeleo ya Milenia 2015;
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025; Awamu ya pili ya Mkakati wa Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Vipaumbele vilivyoainishwa
kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa mwaka 2011/12 - 2015/16;
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010; Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania
(MPAMITA); Mwongozo wa Mpango na Bajeti wa mwaka 2013/14-2015/16; pamoja na
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma - Public Finance
Management Reform Programme (PFMRP).
Usimamizi
wa Uchumi
5.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, Pato la Taifa
liliendelea kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 6.9 ikilinganishwa na
asilimia 6.4 mwaka 2011, ikiwa ni zaidi ya lengo la asilimia 6.8 mwaka
2012. Sekta ya fedha ambayo
inasimamiwa na Wizara ya Fedha ilichangia kikamilifu katika shughuli za
kiuchumi na kukuza Pato la Taifa.
Katika mwaka 2012, sekta hii ya Fedha ilichangia asilimia 1.8 ya Pato la
Taifa ikilinganishwa na asilimia 1.7 mwaka 2011. Ongezeko hili la ukuaji lilitokana na utekelezaji madhubuti
wa Programu ya Maboresho ya Sekta ya Fedha.
6.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho cha mapitio,
Wizara pia ilitekeleza Sera ya Fedha na bajeti kwa lengo la kupunguza ukwasi na
mfumuko wa bei ambapo Benki Kuu ya Tanzania iliongeza mauzo ya fedha za kigeni
katika soko la fedha kama njia mojawapo ya kudhibiti mfumuko huo. Aidha, Benki ilipandisha kiwango cha
chini cha akiba ya amana za Serikali katika mabenki kutoka asilimia 30 hadi
asilimia 40 pamoja na kupunguza kiwango cha kuhodhi fedha za kigeni kulingana
na mitaji yao kwa mabenki kutoka asilimia 10 hadi asilimia 7.5 kuanzia Desemba
2012. Hatua zote zilisaidia
kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei kutoka asilimia 18.7 mwezi Aprili 2012
hadi asilimia 9.4 mwezi Aprili 2013 pamoja na kusaidia kuimarika kwa kiwango
cha ubadilishaji wa shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani. Aidha, katika kuimarisha usimamizi na
maendeleo ya sekta ya fedha, Wizara imerekebisha muundo wake kwa kuanzisha
Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha – Financial Sector Development Division ambayo itasimamia
uandaaji na utekelezaji wa sera za sekta ya fedha na taasisi ndogo za fedha
kama SACCOS na VICCOBA.
Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji wa
Bajeti ya Serikali
7.
Mheshimiwa Spika,
Wizara iliendelea kusimamia uandaaji na utekelezaji wa
bajeti ya Serikali ya matumizi ya kawaida
na miradi ya maendeleo. Wizara imeratibu maboresho ya uandaaji wa bajeti
ya 2013/14 kwa kuzingatia mzunguko mpya wa bajeti. Aidha, Mwongozo wa Mpango na
Bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/14, uliandaliwa kwa kushirikisha wadau
mbalimbali na kusambazwa kwa wakati. Vile vile, Wizara imeandaa na kusambaza
nyaraka muhimu za bajeti ikiwa ni pamoja na vitabu vya bajeti ya Serikali (volume
I, II, III na IV) kama vilivyopitishwa na Bunge na kitabu
kinachotoa maelezo ya Bajeti ya Serikali katika kipindi cha muda wa kati kwa
mwaka 2012/13 - 2014/15. Kitabu hiki kinasaidia kuwajulisha wananchi na wadau
wengine kuhusu matokeo ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita pamoja na
mwelekeo wa bajeti ijayo kwa kipindi cha muda wa kati. Kadhalika, katika
kuboresha uelewa wa bajeti ya Serikali kwa wananchi, Kitabu cha Bajeti Toleo la
Wananchi kwa mwaka 2012/13 kimeandaliwa na kusambazwa kwa wakati na kuwekwa
kwenye tovuti ya Wizara. Kitabu hiki kimesaidia kueleza bajeti kwa wananchi wa
kawaida kwa lugha rahisi na hivyo kuongeza uwazi katika kutoa taarifa muhimu za
kibajeti.
8.
Mheshimiwa Spika,
katika kujenga uwezo wa kuandaa mipango na bajeti kwa Wizara, Idara
zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara ilitekeleza
yafuatayo: kufanya tathmini ya mchakato wa bajeti ya 2012/13 kuhusu namna
bajeti ilivyoandaliwa, changamoto zilizojitokeza na jinsi ya kuzitatua; kuwajengea uwezo maofisa wa bajeti wa
Wizara, Idara, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu
kuandaa bajeti ya 2013/14, maboresho yaliyofanywa kwenye Mfumo wa Kugawa Fedha
za Bajeti - Strategic Budget Allocation System (SBAS)
na kuandaa bajeti inayozingatia utendaji -Performance Based Budgeting;
na kuhuisha Mwongozo wa kuandaa mipango na bajeti, ambao umezingatia mzunguko
mpya wa bajeti. Wizara imeendelea kusimamia malipo ya mishahara ya kila mwezi
kwa ajili ya Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa.
Usimamizi wa Misaada na
Mikopo
9.
Mheshimiwa Spika,
Wizara imeendelea kuboresha usimamizi wa misaada na
mikopo ili kupata matokeo yaliyotarajiwa. Mafunzo ya mfumo wa kutunza takwimu
na kumbukumbu zingine za misaada na mikopo yalitolewa kwa Maafisa kutoka Wizara
21 na Washirika wa Maendeleo wapatao 20. Aidha, mapitio ya utekelezaji wa
Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA), 2006 – 2011 wenye lengo la
kuimarisha usimamizi wa misaada, yalifanyika.
10. Mheshimiwa
Spika, katika kuboresha usimamizi wa
misaada na mikopo ya kibajeti, Wizara
iliandaa mkutano wa Mwaka wa Mapitio ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti - General Budget Support
Annual Review meeting uliofanyika mwezi Novemba 2012.
Matokeo yaliyotokana na Mkutano
huo ni washirika wa Maendeleo kuipatia Serikali misaada ya kibajeti yenye
thamani ya sh. bilioni 1,163.13 fedha ambayo imepangwa kutumika katika bajeti
ya 2013/14. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo
imeimarisha Mfumo wa Mapitio ya Matumizi ya Umma - Public Expenditure
Review (PER)
kwa kuanzisha Sekretarieti ya pamoja yenye wajumbe wa upande wa Serikali na
upande wa Washirika wa Maendeleo pamoja na kuandaa Mpango Kazi wa mwaka.
11. Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara
inatarajia kukamilisha Mfumo mpya wa Ushirikiano wa Kimaendeleo -Development
Cooperation Framework , kati ya Serikali na Washirika wa
Maendeleo. Mfumo huu ndio utakaoongoza usimamizi wa Misaada na Mikopo ya
Kibajeti katika kutekeleza mipango na programu za kitaifa za kukuza uchumi,
kupunguza umaskini na kuleta maendeleo. Aidha, Wizara itaendelea kutoa mafunzo
ya Mfumo wa Kutunza Kumbukumbu za Misaada na Mikopo - Aid Management
Platform kwa Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na Asasi za
Kiraia. Vile vile, Wizara itaendelea kuandaa mikutano ya kila mwaka ya Mapitio
ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti pamoja na Mapitio ya Matumizi ya Umma.
Uhimilivu wa Deni la
Taifa
12. Mheshimiwa
Spika, serikali inasimamia Deni la Taifa kwa
kuzingatia Mkakati wa Taifa wa kusimamia Deni na Sheria ya Mikopo, Dhamana na
Misaada ya mwaka 1974 kama ilivyorekebishwa mwaka 2004. Kwa kuzingatia Sheria
hiyo, mwaka 2012 Serikali ilifanya tathmini ya kuangalia uhimilivu wa Deni la
Taifa na viashiria vyote vya kupima uhimilivu wa deni vilivyokubalika kimataifa
vinaonesha kuwa, deni la taifa ni himilivu katika muda mfupi na muda wa kati.
Mathalani, uwiano wa thamani ya sasa ya Deni la Taifa (Present Value of Debt)
kwa Pato la Taifa (GDP) ni asilimia 18.9 ikilinganishwa na ukomo wake wa
asilimia 50. Hii ni ishara kuwa kiwango cha kukua kwa Deni la Taifa ni kidogo
ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa. Kiashiria kingine muhimu ni
uwiano wa thamani ya sasa ya Deni la Taifa (Present Value of Debt)
kwa thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi (export)
ni asilimia 56.2 ikilinganishwa na kiwango cha cha ukomo ambacho ni asilimia
200. Hii ni ishara nyingine inayotuhakikishia kuwa Deni la Taifa ni himilivu
kwa kuwa kasi ya ukuaji wa Deni la Taifa ni ndogo ikilinganishwa na uwezo wan
chi kulipa deni hilo kwa mapato yanayotokana na mauzo ya bidhaa na humuma nje
ya nchi.
13. Mheshimiwa
Spika, katika mkakati wa kuboresha mfumo wa usimamizi
wa Deni la Taifa serikali inakamilisha taratibu za kuanzishwa kwa Idara kamili
ndani ya Wizara ya Fedha pamoja na kupitia upya Mkakati wa taifa wa kusimamia
madeni wa mwaka 2002 na kuifanyia marekebisho Sheria ya Mikopo, Dhamana na
Misaada ya mwaka 1974 ambayo ilirekebishwa mwaka 2004 na hivyo kuboresha muundo
uliopo wa usimamizi wa Deni la Taifa pamoja na sheria yake.
Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma
14. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha
2012/13, Wizara ilitekeleza yafuatayo: kuboresha Mfumo wa Malipo Serikalini – Integrated
Financial Management System(IFIMS) kutoka mfumo wa toleo la EPICOR 7.3.5 kwenda toleo la EPICOR
9.05
kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma; kukamilisha
zoezi la kutoa mafunzo ya kufanya malipo moja kwa moja benki kwa njia ya
kielektroniki -Tanzania Inter-Bank Settlement System (TISS) kwa watumishi wa Hazina
ndogo zote, Bunge, Mikoa, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI na Idara ya Ushirika,
ikiwa ni maandalizi ya kuunganisha Taasisi hizo kwenye mtandao wa TISS ili
kuboresha usimamizi wa fedha za umma.
15. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi hicho, Wahasibu 200 kutoka
mikoa 25 walipata mafunzo juu ya usimamizi wa fedha za umma; Wahasibu 425
kutoka wizara mbalimbali na Sekretarieti za Mikoa walipata mafunzo juu ya
Viwango vya kimataifa vya kiuhasibu vya kuandaa Hesabu za Serikali – International Public
Sector Accounting Standards
(IPSAS) na watumishi 120 kutoka katika Wizara na Taasisi walipata mafunzo ya
kusimamia Mabadiliko na Kuandaa Mipango Mkakati -Change Management and
Strategic Planning kwa lengo la
kujenga uwezo wa idara za bajeti na Mipango katika kutekeleza maboresho
ya usimamizi wa Fedha za umma.
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha
za Umma – Public Finance Management Reform Programme (PFMRP)
16. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha
usimamizi wa fedha za umma kwa kuendelea kutekeleza Programu ya Maboresho ya
Usimamizi wa Fedha za Umma-PFMRP ambapo Awamu ya Nne ya Programu ilianza
kutekelezwa Julai 2012 na itakamilika Juni 2017. Programu ya PFMRP pamoja na mambo mengine,
imewezesha
Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanza kutumia akaunti sita za benki badala ya
akaunti nyingi zilizokuwepo kwa lengo la kuendelea kuboresha usimamizi wa fedha
za Umma. Aidha, Programu ilitoa fedha za kuwezesha Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kuandaa Mpango Mkakati wake wa Programu ya Usimamizi wa Fedha za
Umma. Vile vile, matokeo ya
tathmini ya utekelezaji wa programu yaliyofanywa kama sehemu ya mapitio ya
mwaka ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti yaliyofanyika mwezi Novemba 2012
yalionesha kuwa utekelezaji wa Programu ulikuwa wa kuridhisha, na uzingatiaji
wa Sheria ya Ununuzi wa Umma katika kufanya ununuzi ulifikia asilimia 74.
17. Mheshimiwa Spika, Wizara
inaendelea kutekeleza Mpango kazi wa miaka mitano wa kuiwezesha Serikali Kuu
kuandaa hesabu kwa Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu –International Public
Sector Accounting Standards (PSAS) accrual basis.
Kwa mara ya kwanza, hesabu za Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na
Sekretarieti za Mikoa kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2013
zitaandaliwa kwa kutumia viwango hivyo. Aidha, Wizara imeandaa miongozo
mbalimbali na kufanya mikutano elekezi ili kuwajengea uwezo na uelewa wahasibu
na wadau mbalimbali. Katika kuimarisha usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali pamoja na utoaji wa taarifa zenye ubora na uwazi,
Wizara imeendelea kusimamia na kuimarisha mtandao wa malipo ya Serikali katika
Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Hazina Ndogo pamoja na Vikosi vya Jeshi.
18. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara itaendelea kusimamia, kuimarisha na kudhibiti mapato na
matumizi ya fedha za Serikali kwa kuboresha mtandao wa malipo wa Serikali.
Aidha, Wizara itatoa ushauri wa kitaalamu na kuunganisha Hazina Ndogo na
Sekretarieti za Mikoa ili kuziwezesha kufanya malipo kwa njia ya ki-elektroniki
(TISS) kupitia Benki Kuu ya Tanzania. Vile
vile, Wizara itaendelea kutoa
mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wahasibu wa Wizara, Mikoa, na Idara za
Serikali ya kuandaa hesabu katika viwango vya kimataifa –IPSAS Accrual basis na kuongeza uelewa wa matumizi ya mtandao wa EPICOR 9.05.
Sera
ya Ununuzi wa Umma
19. Mheshimiwa
Spika, katika eneo la Sera ya Ununuzi wa Umma, Wizara
imetekeleza yafuatayo: kukamilisha rasimu ya Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma;
kukamilisha rasimu ya Kanuni za Ununuzi wa Umma; kuendelea kuhuisha taarifa za
maofisa Ununuzi na Ugavi katika daftari ambapo jumla ya Maofisa 989 wameingizwa
katika daftari hilo. Aidha, Wizara imeendelea na taratibu za kuanzisha kada ya
Ununuzi Serikalini pamoja na kusimamia na kuendeleza kada ya Ugavi nchini.
20. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara imepanga
kufanya yafuatayo: kuanza utekelezaji wa
Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma; kufuatilia na kufanya tathmini ya
mfumo wa Ununuzi wa Umma; na kuendelea kuhakiki daftari la taarifa za maafisa
Ununuzi na Ugavi Serikalini.
Mpango
wa Millenium Challenge Account – Tanzania (MCA-T)
21. Mheshimiwa
Spika, Wizara kupitia MCA-T imeendelea
kusimamia utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia
shirika la Millennium Challenge Corporation (MCC).
Utekelezaji wa miradi hiyo umeendelea vizuri licha ya changamoto ambazo
zimeathiri kasi ya utekelezaji kama vile mvua nyingi kwa mikoa ya Ruvuma na
Rukwa na matatizo ya kiufundi. Ujenzi wa barabara ya Tanga- Horohoro
ulikamilika kwa kiwango cha lami na kukabidhiwa kwa Serikali mwezi Oktoba 2012;
ujenzi wa barabara za ukanda wa Mtwara yaani Songea – Namtumbo na Peramiho –
Mbinga na ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Kisiwa cha Mafia unaendelea. Aidha,
kazi ya kuweka lami katika barabara tano za Pemba ya Vijijini Kaskazini imeanza
na ujenzi wa barabara ya Tunduma – Sumbawanga ambao umegawanywa katika sehemu
tatu; Tunduma – Ikana, Ikana – Laela na Laela – Sumbawanga unaendelea.
22. Mheshimiwa
Spika, Miradi ya kupeleka umeme Zanzibar kupitia chini ya
bahari na ule wa ukarabati wa mtandao wa umeme kwa mkoa wa Dodoma imekamilika.
Utekelezaji wa miradi mingine ya ukarabati wa vituo vya kupoozea umeme,
ukarabati wa mtandao wa umeme kwa mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya,
Mwanza na Kigoma, ikiwa ni pamoja
na mradi wa umeme wa Jua Kigoma, inaendelea. Aidha, miradi ya upanuzi wa
mtambo wa maji Ruvu chini na ukarabati wa mfumo wa maji kwa Manispaa ya
Morogoro nayo pia inaendelea.
23. Mheshimiwa
Spika, kutokana na utekelezaji wa kuridhisha wa miradi,
katika kikao cha Bodi ya MCC kilichofanyika mwezi Desemba
2012, kiliamua kuikubalia Tanzania kuidhinisha maandalizi ya Mpango wa Pili wa
miradi ya MCC (MCC Compact II). Serikali imeshaanza
maandalizi hayo baada ya kuunda
sekretarieti ya uratibu
Ukaguzi
wa Ndani
24. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara imeandaa na
kutoa miongozo ya Usimamizi wa vihatarishi katika Sekta ya Umma pamoja na
Mwongozo wa Uhakiki wa Ubora wa Ukaguzi wa Ndani. Miongozo hii ilizinduliwa
mwezi Machi, 2013. Aidha, Wizara imetayarisha Mwongozo wa Ukaguzi wa Ndani kwa
kuzingatia viwango vya kimataifa na unategemewa kuanza kutumika rasmi mwezi
Julai, 2013. Kadhalika, Wizara imekamilisha Mkataba wa Makubaliano kati ya
Wakaguzi wa Ndani na Wateja wake
na pia kutoa kanuni za maadili ya wakaguzi wa ndani. Miongozo hiyo ina
lengo la kuboresha utendaji kazi wa ukaguzi wa ndani.
Ukaguzi wa Hesabu za Serikali
25. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 Ofisi
ya Taifa ya Ukaguzi iliendelea kutekeleza yafuatayo: kufanya ukaguzi wa hesabu za mafungu yote ya Wizara na
Idara za Serikali, Mikoa ya Tanzania Bara, Halmashauri, Mashirika ya Umma,
Balozi na Wakala wa Serikali; kukamilisha ripoti tano za ukaguzi wa ufanisi -Value
for Money Audit ambapo
taarifa zote hizi zimewasilishwa hapa Bungeni tarehe 11 Aprili 2013;
ukaguzi wa Mashirika 50 ulikuwa unaendelea katika hatua mbalimbali za ukaguzi;
Ofisi imeendelea kukiimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ufanisi kwa kutoa mafunzo
kwa watumishi saba na kukipatia vitendea kazi zaidi. Aidha, ofisi iliendelea
kulipia mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 53 waliopo katika vyuo mbalimbali
na kugharamia mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 400. Vile vile, ujenzi wa
ofisi unaendelea katika mikoa ya Dodoma na Rukwa na unatarajiwa kukamilika
mwanzoni mwa mwaka 2014.
26. Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14, Ofisi itatekeleza shughuli
zifuatazo: kuendelea kutekeleza
mkakati wa kuwaondoa wakaguzi katika ofisi za wakaguliwa; kufanya ukaguzi wa
mapato na matumizi ya vyama vyote vya siasa nchini ili kukidhi matakwa ya
sheria ya vyama vya siasa na kuendelea kufanya mazungumzo na Msajili wa vyama
vya siasa namna ya kutekeleza Sheria ya Gharama za Uchaguzi; na kuziimarisha
Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali – Public Accounts Committee (PAC)
na Local Authorities Accounts Committee (LAAC),
Kamati ya Bajeti na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara kwa kuzijengea uwezo.
27. Mheshimiwa Spika,
shughuli nyingine zitakazotekelezwa ni pamoja na: kuhakiki matumizi ya fedha za
Halmashauri; kushiriki kikamilifu katika jukumu jipya la kukagua Taasisi za
Umoja wa Mataifa ambapo ofisi inaingia mwaka wa pili wa kuwepo kwenye Bodi ya
Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa -UN Board of Auditors; kufanya
kaguzi sita za thamani ya fedha; kuendelea na uunganishaji wa ofisi za Ukaguzi
zilizoko mikoani na makao makuu kwa kutumia Mtandao Mpana -Wide Area Network
(WAN); kuimarisha ukaguzi wa kiutambuzi - Forensic audit; na
kuongeza idadi ya watumishi.
Sheria
na Miswada ya Fedha
28. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara iliendelea
kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali ili kuweka usimamizi mzuri wa kodi na
fedha za umma. Baadhi ya sheria zilizofanyiwa marekebisho ni sheria mbalimbali
za kodi ambazo zilipitishwa kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 - The
Finance Act, 2012 na Sheria ya Udhibiti wa Fedha
Haramu iliyofanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali iliyopitishwa na Mkutano wa Bunge wa mwezi Februari, 2013. Aidha,
marekebisho ya Mkataba wa Cotonou unaohusu ushirikiano baina ya nchi za Jumuiya
ya Ulaya, Afrika na Visiwa vya Caribbean ambapo Tanzania ni mwanachama,
yalipitishwa na Bunge kupitia Azimio la Bunge katika Mkutano wa mwezi Novemba,
2012.
29. Mheshimiwa
Spika, Wizara pia iliandaa kanuni mbalimbali ili kuwezesha
usimamizi na utekelezaji wa Sheria za Kifedha. Baadhi ya kanuni zilizotolewa ni
zile za; kuanzisha credit Reference
Databank ya Utunzaji wa Taarifa za Wateja wa Benki na
Taasisi za Kifedha; Pamoja na Credit Reference System.
Matumizi ya Vifaa vya Kielektroniki katika Ukusanyaji wa Kodi ya Mapato;
Usimamizi wa Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa abiria wa ndege ambao
sio raia wa Tanzania; Kanuni za Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu; na Kanuni
za Sheria ya Uwekaji Stempu kwenye kazi za Wasanii.
30. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara
itaendelea kukamilisha maandalizi
ya kuwezesha kutungwa kwa Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani – Vale
Added Tax (VAT), Sheria ya Utawala wa Kodi - Tax
Administration Act, Sheria ya Hoteli - Hotels Tax Act,
Sheria ya Takwimu, Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Mfuko wa Akiba ya
Wafanyakazi Serikalini - Government Employees Provident Fund (GEPF).
Aidha, Wizara inatarajia kuwasilisha Bungeni mapendekezo ya marekebisho kwenye
Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, pamoja na Sheria ya Mikopo, Dhamana na
Misaada ili kuihuisha kulingana na mazingira ya sasa ya uchumi. Vile vile,
wizara itaandaa kanuni mbalimbali zitokanazo na sheria hizi ili kuwezesha
utekelezaji wake.
Usimamizi
wa Mashirika na Taasisi za Umma
31. Mheshimiwa
Spika, Wizara imeendelea kusimamia utendaji wa Mashirika ya
Umma pamoja na Taasisi zake. Majukumu yaliyotekelezwa kwa kushirikiana na
Shirika Hodhi - Consolidated Holding Corporation (CHC)
ni pamoja na kuendelea na zoezi la urekebishaji wa mashirika yaliyo na matatizo
katika sekta za Usafirishaji, Madini, Mawasiliano, Utalii na Fedha.
32. Mheshimiwa
Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepata ofisi katika jengo
la CHC Mtaa wa Samora na tayari watumishi wamehamia katika ofisi hiyo. Katika mwaka
wa fedha 2013/14, Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa
Hazina inatarajia kutekeleza yafuatayo: kusimamia
utendaji wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma na kuboresha
utawala bora kwa kuingia Mikataba ya Utendaji -Performance Contracts
na Bodi za Mashirika ya Umma; kusimamia mikakati ya kurekebisha Mashirika ya
Umma na uperembaji wa Mashirika ya Umma yaliyobinafsishwa; na kuimarisha
usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma ili kuongeza ufanisi na mapato ya
Serikali.
Mafao ya Wastaafu na
Mirathi
33. Mheshimiwa
Spika, katika kuboresha huduma za pensheni, Wizara imeanza
utaratibu wa kulipa Pensheni kwa vipindi vya miezi mitatu mitatu badala ya
vipindi vya miezi sita sita kuanzia Januari, 2012. Katika utaratibu huu,
Wastaafu wanalipwa Pensheni ya miezi miwili mapema - in advance badala ya miezi
mitano iliyokuwa inalipwa katika utaratibu wa awali. Pensheni inalipwa mwishoni
mwa miezi ya Julai, Oktoba, Januari na Aprili. Aidha, Wizara imeendelea na kazi
ya kuweka kumbukumbu za Wastaafu waliopo kwenye daftari la Pensheni la Hazina
kwenye Mfumo wa Kompyuta ujulikanao kwa jina la SAPERION kwa lengo la
kurahisisha upatikanaji wa taarifa. Hadi kufikia mwezi Aprili 2013, kumbukumbu
za Wastaafu 106,030 ziliwekwa kwenye mfumo wa kompyuta. Zoezi hili litaendelea
kufanyika katika mwaka 2013/14 ili kukamilisha uhifadhi wa kumbukumbu za
Wastaafu wote wanaolipwa kupitia Hazina.
34. Mheshimiwa
Spika, Wizara imeendelea kusimamia na kuratibu shughuli za
mifuko ya pensheni iliyo chini ya Wizara ya Fedha. Mifuko hiyo ni Mfuko wa
Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma
(PPF) na Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF).
Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi
wa Umma - PSPF
35. Mheshimiwa
Spika, hadi kufikia Aprili, 2013 Mfuko wa Pensheni kwa
Watumishi wa Umma ulisajili wanachama 332,067. Katika kipindi hicho, Mfuko pia ulikusanya jumla ya shilingi
bilioni 446.12. Kati ya makusanyo hayo, michango ya wanachama ni shilingi
bilioni 374.76 na mapato yatokanayo na vitega uchumi ni shilingi bilioni 71.36.
Matarajio ni kukusanya jumla ya shilingi bilioni 749.10 ifikapo mwisho wa mwaka
wa fedha 2012/13. Aidha, thamani ya Mfuko hadi tarehe 30 Aprili, 2013 ilifikia
shilingi bilioni 1,112.24 na unatarajiwa kufikia shilingi bilioni 1,226.59
mwezi Juni, 2013. Jumla ya shilingi bilioni 422.16 zilitumika kulipa mafao
ikiwa ni pamoja na mafao ya kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi sawa na
asilimia 93.21 ya lengo la mwaka.
Vile vile, ili kuongeza wigo wa wanachama, Mfuko umeanzisha mpango
maalum wa kuchangia kwa hiyari kwa watumishi wa sekta rasmi na isiyo rasmi.
36. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/14, Mfuko unatarajia
kukusanya jumla ya shilingi bilioni 680.55, kati ya
makusanyo hayo, michango ya wanachama ni shilingi bilioni 539.18, na mapato
yatokanayo na vitega uchumi ni shilingi bilioni 141.37. Aidha, thamani ya Mfuko
inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 1,522.01. Mfuko unatarajia kulipa kiasi
cha shilingi bilioni 522.32 kwa ajili ya mafao mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi, ambapo jumla ya wanachama wapatao
7,647 wanatarajia kustaafu kwa mujibu wa sheria. Vile vile, Mfuko unatarajia
kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 1,211.39 kwenye maeneo mbalimbali ya vitega
uchumi.
Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi
Serikalini - GEPF
37. Mheshimiwa
Spika, hadi kufikia Machi, 2013 Mfuko umesajili jumla ya
wanachama 6,755 wakiwemo wananchi waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo
rasmi. Katika kipindi hicho michango ya wanachama ilifikia kiasi cha shilingi
bilioni 22.74 sawa na asilimia 64.60 ya malengo ya mwaka mzima. Mapato
yatokanayo na vitega uchumi yamefikia shilingi bilioni 11.64 ambayo ni sawa na asilimia 72.75 ya malengo ya
mwaka mzima na thamani ya Mfuko imeongezeka na kufikia shilingi bilioni 190.0
Machi, 2013. Aidha, Mfuko umelipa mafao ya shilingi bilioni 7.13 hadi kufikia
Machi, 2013 na kufungua ofisi katika Manispaa za Temeke, Kinondoni na Ilala kwa
lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.
38. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Mfuko utaendelea na
jitihada zake za kuboresha huduma kwa wanachama, kutanua wigo wa wanachama,
kukuza mapato yatokanayo na uwekezaji na kusajili wanachama wengi zaidi kupitia
Mpango wa Hiari wa kujiwekea akiba ya uzeeni na wa lazima. Aidha, Mfuko
unatarajia kusajili jumla ya wanachama 16,500 na kukusanya michango yenye
thamani ya shilingi bilioni 40.50. Vile vile, mapato ya vitega uchumi
yataongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 19.24 na thamani ya Mfuko
inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 227.
Mfuko wa Pensheni wa Mashirika
ya Umma - PPF
39. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012, Mfuko ulikusanya shilingi bilioni
229.1 kutokana na michango ya wanachama ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia
21.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 188.1 zilizokusanywa mwaka 2011. Ongezeko
hili lilitokana na waajiri kuzingatia sheria kwa kuleta michango kwa wakati na
uandikishaji wa wanachama wapya. Aidha, idadi ya wanachama imeongezeka kutoka
180,049 mwaka 2011 hadi 203,981 mwaka 2012. Mfuko pia ulilipa mafao ya jumla ya
shilingi bilioni 99.4. Mafao hayo ya PPF yalijumuisha na mafao ya elimu ambayo
hulipwa kwa ajili ya kusomesha watoto wasiozidi wanne wa mwanachama aliyefariki
akiwa kazini. Mwaka 2012 mfuko ulisomesha watoto 1,333 kwa gharama ya shilingi
milioni 683 ikilinganishwa na watoto 1,392 waliosomeshwa mwaka 2011 kwa gharama
ya shilingi milioni 573. Watoto hawa husomeshwa kuanzia elimu ya chekechea hadi
kidato cha nne.
40. Mheshimiwa
Spika, mapato yatokanayo na uwekezaji yaliongezeka kutoka
shilingi bilioni 91.4 mwaka 2011, hadi kufikia shilingi bilioni 105.5 kwa mwaka
2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.4. Aidha, thamani ya Mfuko kufikia
Desemba 2012, ilikuwa imeongezeka kufikia shilingi bilioni 1,089.8 ikiwa ni
ongezeko la asilimia 21.8 ikilinganishwa na thamani ya Mfuko ya shilingi
bilioni 894.5 ilivyokuwa Desemba 2011.
41. Mheshimiwa
Spika, Mfuko unatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni
281.7, kuandikisha wanachama wapya 72,000 kutoka sekta ya umma na binafsi,
na kukusanya shilingi bilioni
125.6 kutokana na uwekezaji ifikapo Desemba 2013. Aidha, thamani ya Mfuko
inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 1,302.68.
42. Mheshimiwa
Spika, kumekuwepo na changamoto kadhaa
katika Mifuko ya Hifadhi ya jamii ikiwemo: Wanachama kulalamikia kiwango kidogo
cha mafao kitolewacho na baadhi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pale
wanapostaafu. Vile vile, kuna suala la malimbikizo ya madeni yanayotokana na
Mifuko kugharimia utekelezaji
wa miradi ya Serikali. Aidha, katika kutafuta ufumbuzi wa
changamoto hizo Serikali kupitia Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii
imepanga kutathmini uwezo wa mifuko yote ya hifadhi ya jamii na kupendekeza
viwango vya mafao; na kuhakikisha kwamba, mifuko hiyo inakuwa endelevu. Vile vile, Serikali inaendelea kulipa
madeni ya mifuko ya jamii kwa
awamu na pia imeunda kamati ya
kuchambua na kuhakiki madeni mengine
ya baadhi ya mifuko ili kupendekeza njia endelevu ya kuyalipa.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania - TRA
43. Mheshimiwa
Spika,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kutekeleza Mpango wa tatu wa
Maboresho wa mwaka 2008/09 - 2012/13 ambao umekuwa msingi wa kuongezeka kwa
ukusanyaji wa mapato mwaka hadi mwaka. Katika jitihada za kuongeza mapato ya
ndani, Wizara kupitia TRA imetekeleza yafuatayo: kuanzisha mfumo wa kimtandao
wa kuwasilisha ritani za kodi - tax returns; kufanya
tathmini ya maeneo hatarishi katika Utawala wa Sekta za Umma; kuweka mfumo wa
taarifa wa RADDEX 2 na kutoa mafunzo kwa watumiaji; kusambaza Mfumo wa
Ki-elektroniki wa Ufuatiliaji Usafirishaji Mizigo (Electronic Cargo Tracking
System); na kuboresha mfumo wa utunzaji kumbukumbu na Taarifa za Magari. Aidha,
TRA imekamilisha uandaaji wa Awamu ya Nne ya Mpango wa Maboresho (2013/14 -
2017/18) unaotarajiwa kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2013/14.
44. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara kwa
kushirikiana na TRA itaendelea na azma yake ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato
ya ndani kwa kupanua wigo wa makusanyo na kuchukua hatua mbalimbali za kisera
na kiutawala katika maeneo ya mapato yatokanayo na kodi.
45. Mheshimiwa
Spika, mnamo mwezi Mei 2013 kulitokea tatizo la mlundikano wa makonteina Bandarini
Dar es Salaam kutokana na kutokamilika kwa taratibu za kuyaondoa. Kutokana na
tatizo hili Wizara ilikutana na wadau wote pamoja na wafanyabiashara ili
kuondoa adha hiyo. Katika kikao hicho Mamlaka ya Mapato ilielekezwa
kushughulikia suala hilo kulingana na sheria na taratibu ili wafanyabiashara
waweze kulipia makonteina yao na kuyaondoa bandarini. Tunapenda ieleweke kwamba
katika tatizo hili hakuna kodi yoyote iliyoongezwa kwa makonteina hayo ya
wafanyabiashara na walitakiwa kulipa kodi stahili.
Huduma
za Kibenki
Benki
Kuu ya Tanzania
46. Mheshimiwa
Spika,
katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara kwa kupitia Benki Kuu imeendelea
kutekeleza mabadiliko chanya katika sekta ya fedha ili kuhakikisha kuwa sekta
hiyo inachochea maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi. Mabadiliko ya sekta ya
fedha yamesababisha utendaji mzuri wa Taasisi za Fedha ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya mabenki
kutoka benki 49 mwezi Februari,
2012 mpaka benki 51 mwisho wa mwezi Februari 2013. Aidha, rasilimali za mabenki
zimeimarika zaidi na kufikia shilingi trilioni 17.3 mwezi Februari ambapo
mikopo iliyotolewa kwa sekta binafsi imefikia shilingi trilioni 8.8.
47. Mheshimiwa
Spika,
katika kuendelea na jitihada za kuboresha upatikanaji wa mikopo, Benki Kuu imeanzisha mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa kumbukumbu za wakopaji (Databank)
na utaratibu wa utoaji wa taarifa za wakopaji kwa kutumia kampuni binafsi
(Credit Reference Bureaux). Mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa kumbukumbu za
wakopaji umeshaanza kufanya kazi na mabenki yameshaanza kupeleka taarifa za
wakopaji. Kampuni mbili za utoaji wa taarifa za wakopaji zimeshapewa leseni na
wapo katika maandalizi ya mwisho ili waanze kutoa huduma ya kutoa taarifa hizo.
Mfumo huu utaboresha upatikanaji wa mikopo ya muda wa kati na muda mrefu.
48. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Benki Kuu
imetoa Mwongozo wa Huduma za Kibenki kwa Kutumia Wakala wa Mwaka 2013
(Guidelines on Agent Banking for Banking Institutions, 2013) ambao ulianza
kutumika mwezi Februari, 2013. Kutolewa kwa mwongozo huu ni sehemu ya mpango wa
kuweka mazingira yatakayowezesha kupanua wigo wa huduma za kibenki na
kuhakikisha usalama wa benki mbalimbali zitakazojihusisha na mfumo wa utoaji
huduma za kibenki kwa kutumia mawakala. Mfumo huu utarahisisha upatikanaji wa
huduma bora na nafuu za kibenki.
49. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Benki Kuu
imeunda Kamati ya Kitaifa ya Uthabiti wa Mfumo wa Fedha (Tanzania Financial
Stability Forum) ili kusaidia kuimarisha ushirikiano na kubadilishana taarifa
kati ya wadhibiti wa sekta ya fedha kama msingi imara kwa ajili ya kuhakikisha
uthabiti wa mfumo wa fedha nchini na kupanua wigo wa usimamizi katika mfumo wa
fedha kutoka usimamizi unaolenga taasisi moja moja kwenda usimamizi wa mfumo wa
fedha unaolenga sekta nzima ya fedha kwa ujumla wake. Aidha, taarifa
inayoonesha hali halisi ya uthabiti wa sekta ya fedha inatolewa kila baada ya
miezi sita.
50. Mheshimiwa Spika, Benki Kuu
za Afrika Mashariki zilikubaliana kutengeneza mfumo wa malipo utakaorahisisha
malipo kwa kutumia sarafu za nchi husika. Mfumo huu ujulikanao Kama East
African Cross Border Payment System - EAPS, umefikia hatua ya
majaribio kupitia mifumo ya Malipo Makubwa (Real Time Gross Settlement System –
RTGS) ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Mategemeo ni mfumo huu kuanza
kutumika kwa nchi hizi tatu, ikiwa taratibu zote za kujiunga na mfumo huu
zitakuwa zimekamilika, mwezi Julai 2013. Aidha, Nchi za Rwanda na Burundi
zitakapokuwa tayari zitajiunga na mfumo huo. Kuanza kwa mfumo huu wa malipo
kutarahisisha malipo katika Jumuiya na kukuza shughuli za kibiashara na uchumi.
51. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara kwa
kushirikiana na Benki Kuu itaandaa mapendekezo ya kutunga Sheria ya
kusimamia mifumo ya malipo nchini
(National Payment Systems Act). Aidha, Benki kuu itaendelea
kuandaa sera za kifedha na kusimamia utekelezaji wake. Vile vile, Wizara kwa
kushirikiana na Benki Kuu itafanya
tathmini ya mpango wa utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango
wa Maboresho ya Sekta ya Fedha unaoishia Juni, 2013 na kuandaa mpango wa
utekelezaji wa awamu ya tatu. Kadhalika, Benki Kuu itahakikisha mwongozo wa
kitaifa kuhusu elimu ya masuala ya fedha (Financial Education Framework)
unazingatiwa. Mwongozo huu unalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa
kuweka akiba na kutumia huduma za fedha katika shughuli zao za kila siku.
Benki
ya Maendeleo TIB - TIB Development Bank
52. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/13 Benki ya Rasilimali (TIB)
iliendelea na utekelezaji wa marekebisho ili kuwa benki imara ya maendeleo
tangu Novemba 2012 benki ilibadilisha jina na kuitwa TIB Development Bank ili
kuweka wazi dhana ya benki ya maendeleo. Aidha, mchakato wa uanzishwaji wa
benki ambayo kampuni tanzu inayojishughulisha na shughuli za biashara (TIB
Corporate Bank) ambapo usajili wake upo katika hatua za mwisho. Mara taratibu
zote zitakapokamilika, TIB itafanya kazi katika mfumo wa makampuni mawili
yanayotegemeana moja likijikita kwenye shughuli za maendeleo (TIB Development
Bank) na lingine kwenye shughuli za kibiashara (TIB Corporate Bank). Benki hizi
zitakamilisha muundo wake ifikapo mwezi Septemba, 2013.
53. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/13, Benki ilifungua
tawi mkoani Mbeya na ofisi ya
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hii inafanya benki kuwa na jumla ya matawi
matano na
ofisi tatu za kanda. Aidha, hadi kufikia Desemba 2012, Benki
ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 242.9 ikilinganishwa na mikopo
ya shilingi bilioni 181.7 Desemba 2011 sawa na ongezeko la asilimia 74.8.
Mikopo mingi ilitolewa kwenye sekta ya kilimo na usindikaji wa mazao ya kilimo
(mikopo hii ni tofauti na ile ya Dirisha la kilimo). Vile vile, mtaji wa benki
ulifikia shilingi bilioni 142.1 baada ya Serikali kuongeza shilingi bilioni 40.
Benki ilipata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 8.6 ikiwa ni ongezeko la
asilimia 48 toka shilingi bilioni 5.8 zilizopatikana mwaka ulioishia Desemba
2011.
54. Mheshimiwa
Spika, Dirisha la Kilimo katika Benki ya Maendeleo TIB
liliendelea kutoa mikopo kwa wakopaji mbalimbali kwa riba nafuu. Tangu kuanza
kwa dirisha mwaka 2010 hadi kufikia Desemba 2012, maombi yenye thamani ya
shilingi bilioni 40.1 yaliidhinishwa ambapo shilingi bilioni 20.0 (asilimia
49.9) zilikopeshwa kwa makampuni; shilingi bilioni 5.7 (asilimia 14.2) kwa
taasisi ndogo za fedha zinazokopesha wakopaji wadogo; na shilingi bilioni 14.4
(asilimia 35.9) kwa vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) ambavyo pia
vinafaidisha wakopaji wadogo. Hii inamaanisha asilimia 50.1 ya mikopo imetolewa
kwa wajasiriamali wadogo. Aidha, kuanzia Julai, 2013 Dirisha la Kilimo lililopo
TIB litahamishiwa katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania.
55. Mheshimiwa
Spika, hadi kufikia Desemba 2013, mikopo inayotolewa na
Benki ya Maendeleo TIB katika sekta mbalimbali inatarajiwa kufikia shilingi
bilioni 379.2 na faida kabla ya kodi inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 16.6.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo - TADB
56. Mheshimiwa
Spika, Wizara imeendelea na utekelezaji wa Mpango Kazi wa
kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania – TADB. Lengo la kuanzisha
benki hiyo ni kutoa mikopo ya muda mfupi, wa kati na mrefu katika sekta ya
kilimo inayojumuisha uvuvi na mifugo. TADB ilisajiliwa BRELA chini ya Sheria ya Kampuni
ya mwaka 2002 kwa jina la Tanzania Agricultural Development Bank Limited
(TADB Ltd). Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 90.0 kati ya lengo
la shilingi bilioni 100 kimeshatolewa kama kianzio cha Mtaji. Vile vile, Muundo wa benki ya kilimo na
majukumu ya wafanyakazi katika nafasi mbalimbali umeandaliwa. Mwenyeketi na
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wameteuliwa na ajira za maafisa waandamizi wa
benki hiyo inatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Katika
mwaka 2013/14, shilingi bilioni 10 zimetengwa ili kukamilisha lengo la mtaji wa
kuanzia wa shilingi bilioni 100.
Twiga
Bancorp
57. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi kinachoishia Desemba
2012 Taasisi iliendelea kupanua shughuli zake kwa
kufungua tawi moja mkoani Dodoma na kuifanya taasisi kuwa na matawi matano.
Katika kipindi hicho, amana za wateja zilifikia shilingi bilioni 58.41 ikilinganishwa
na shilingi bilioni 54.2 Desemba 2011 sawa na ongezeko la asilimia 7.8. Aidha,
mikopo iliyotolewa ilifikia shilingi bilioni 39.43 ikilinganishwa na shilingi
bilioni 35.9 kwa mwaka ulioishia Desemba 2011 sawa na ongezeko la asilimia 9.8.
Vile vile, Taasisi iliwekeza shilingi bilioni 4.7 kwenye Dhamana za Serikali na
Amana katika Benki zingine ikilinganishwa na shilingi bilioni 19.0
zilizowekezwa katika kipindi kama hicho mwaka 2011.
58. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka unaoishia Desemba, 2013, amana za wateja
zinatarajiwa kufikia shilingi bilioni 73.25 kutoka shilingi bilioni 58.41 za
Desemba, 2012; mapato kutokana na shughuli mbalimbali za kibiashara yanatarajia
kufikia shilingi bilioni 12.66 ikilinganishwa na shilingi bilioni 9.56
zilizokusanywa Desemba, 2012; na mtaji ghafi wa Benki (Owners’ Equity)
unatarajiwa kukua kutoka shilingi bilioni 5.81 hadi shilingi bilioni 7.24
ifikapo Desemba 2013. Aidha,
thamani ya mikopo kwa wateja inatarajia kufikia shilingi bilioni 49.10 na
uwekezaji katika Dhamana za Serikali na Amana za Muda Maalum kwenye mabenki
unatarajia kufikia shilingi bilioni 16.80. Vile vile, Taasisi inatarajia kupata
faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 0.48.
Benki
ya Posta - TPB
59. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha mwaka 2012 Benki ilianzisha huduma
mpya ya Platinum Account inayolenga vijana walio katika
Vyuo Vikuu na Taasisi nyingine za elimu ya juu. Manufaa ya huduma hii ni kuwawezesha vijana kujiwekea akiba
na kupitishia mikopo ya elimu. Aidha, Benki iliendelea kupanua mtandao wake kwa
kufungua matawi madogo katika
ngazi ya Wilaya katika vituo vya Shirika la Posta. Vile vile, Benki ilianzisha
huduma ya POPOTE Quick Account, inayomuwezesha mteja
kupata huduma za benki mahali popote kupitia simu ya mkononi kwa lengo la
kuwafikia Wananchi walio wengi wanaoishi vijijini.
60. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012, amana za wateja zimeongezeka
kutoka shilingi bilioni 120.92 mwaka 2011 hadi kufikia shilingi bilioni 144.56
ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.4. Aidha, benki ilitoa mikopo yenye thamani ya
shilingi bilioni 103.34 ikilingalishwa na shilingi bilioni 66.75 mwaka 2011
ikiwa ni ongezeko la asilimia 54.83. Vile vile, uwekezaji katika vitega uchumi
vya Benki ya Posta umeongezeka kutoka shilingi bilioni 117.67 mwaka 2011 hadi
kufikia shilingi bilioni 146.96, ikiwa ni ongezeko la asilimia 24.9. Kadhalika,
Benki imepata faida baada ya kodi ya shilingi bilioni 3.59 ikilinganishwa na
shilingi bilioni 2.58 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia 39.4. Katika
mwaka 2012/13, Serikali iliiongezea Benki ya Posta mtaji wa shilingi bilioni
1.5 na kufanya mtaji wa benki kuwa jumla ya shilingi bilioni 16.82.
61. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013, benki itaendelea na mkakati
wake wa kuimarisha huduma zitolewazo kupitia Shirika la Posta kwa kukarabati na
kuunganisha katika mtandao wa benki vituo 10 vya Posta vilivyoko Temeke,
Tunduma, Kahama, Geita, Masasi, Peramiho, Njombe, Kyela, Simiyu na Kasulu hivyo
kuvipa uwezo wa kutoa huduma za haraka. Vituo hivi vitakuwa ni matawi madogo na
hivyo kufanya benki kufikisha jumla ya matawi 23. Aidha, benki itafunga vifaa vya ki-elektroniki
katika vituo vya mauzo. Vile vile, Benki inatarajia kupanua wigo wa mikopo kwa
kuingia mikataba na Sekretarieti za Mkoa na Jeshi la Kujenga Taifa, na kuongeza
kipindi cha marejesho kutoka miaka mitatu hadi minne. Kadhalika, Benki
inatarajia kupata faida baada ya kodi ya shilingi bilioni 5.11 ikiwa ni
ongezeko la asilimia 25.5 ikilinganishwa na faida ya shilingi bilioni 4.07
iliyopatikana mwaka 2012.
Taasisi
za Kitaalam na Huduma Nyinginezo
62. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara iliendelea
kusimamia taasisi za kitaalam na huduma nyinginezo ambazo ziko chini ya Wizara
ya Fedha ambazo ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS; Bodi ya Taifa ya Wahasibu
na Wakaguzi – NBAA; Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi – PSPTB; na Bodi ya
Michezo ya Kubahatisha. Aidha, huduma nyingine zinajumuisha: Usimamizi wa shughuli za Bima; Masoko ya Mitaji na Dhamana; na huduma
za dhamana ya uwekezaji.
Taasisi
za Mafunzo
63. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/13, Wizara imeendelea kusimamia
taasisi za mafunzo zilizo chini yake. Taasisi hizo ni Chuo cha Usimamizi wa
Fedha – IFM, Taasisi ya Uhasibu Arusha – IAA, Taasisi ya Uhasibu Tanzania –
TIA Chuo cha Mipango na Maendeleo
Vijijini – IRDP, na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC .
CHANGAMOTO
64.
Mheshimiwa
Spika, katika
kutekeleza majukumu yake, Wizara ilikabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo
zifuatazo:-
i)
Kudhibiti
matumizi ya fedha za umma sambamba na kuongeza mapato ya Serikali;
ii)
Kuzingatia kanuni na taratibu zilizoainishwa kwenye Mkakati wa Pamoja
wa Misaada Tanzania (MPAMITA) na upatikanaji wa fedha kutoka kwa wafadhili wa
nje;
iii)
Kuwa na Sera ya Mali ya Serikali.
iv)
Kufikiwa kwa malengo ya ukusanyaji wa mapato
yasiyo ya kodi;
v)
Kuwepo kwa mahitaji makubwa ya fedha nje ya
bajeti;
vi)
Kuwepo kwa mchakato mrefu wa upatikanaji wa
fedha za kugharamia Miradi ya Maendeleo hasa mikopo ya kibiashara
(non-conscessional borrowing); na
vii) Kuongezeka
kwa malimbikizo ya madeni ya ndani katika mafungu mbalimbali ambayo yameshindwa
kuingizwa kwenye viwango vya bajeti.
65. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto
hizo, Wizara itachukua hatua kupitia mipango na bajeti zake ili kuhakikisha
kuwa changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi katika mwaka 2013/14 na kuendelea.
Hatua za ufumbuzi wa changamoto hizi zitaelezwa katika hotuba ya bajeti ya
Serikali itakayowasilishwa Juni 13,
2013.
66. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, majukumu ya Wizara
yalitekelezwa katika mafungu sita ya kibajeti. Mafungu hayo ni Fungu 50 -
Wizara ya Fedha; Fungu 23 - Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali; Fungu 22 - Deni
la Taifa; Fungu 21 – HAZINA; Fungu 13 - Kitengo cha
Udhibiti wa Fedha Haramu; na Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha. Aidha, Fungu
45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, linaombewa fedha Bungeni na Waziri wa Fedha kwa
mujibu wa Sheria.
Fungu
50 – Wizara ya Fedha
67. Mheshimiwa
Spika, Wizara ilitarajia kupata shilingi
bilioni 124.42 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato yasiyo ya kodi kupitia Fungu 50. Vyanzo
hivyo ni pamoja na mauzo ya mali, uuzaji wa nyaraka za zabuni na mapato kutoka
katika Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali yakiwemo Gawio, Michango na
Marejesho ya mikopo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, makusanyo
yalifikia shilingi bilioni 37.27 sawa na asilimia 29.97 ya lengo. Makusanyo
zaidi yanatarajiwa katika robo ya nne ya mwaka wa fedha baada ya Mashirika
mengi kuandaa hesabu za mwaka na
ukaguzi wa hesabu hizo kukamilishwa.
68.
Mheshimiwa Spika,
makadirio ya matumizi
ya Fungu 50 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa
shilingi bilioni 98.41 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi
bilioni 546.51 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili,
2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 70.32 sawa na asilimia
71.46 ya makadirio na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 311.28
sawa na asilimia 56.96 ya makadirio.
Fungu
23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali
69.
Mheshimiwa Spika,
makadirio ya matumizi
ya Fungu 23 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa
shilingi bilioni 75.12 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi
bilioni 6.12 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili,
2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 49.34 sawa na asilimia
65.67 ya makadirio, na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 1.29
sawa na asilimia 21.05 ya makadirio.
Fungu
22 - Deni la Taifa
70. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 makadirio ya matumizi ya Fungu 22 yalikuwa
shilingi bilioni 2,735.91. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013 matumizi
ya fungu hili yalifikia shilingi bilioni 2,226.70 sawa na asilimia 81.39 ya makadirio.
Fungu
21- HAZINA
71. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13,
Wizara kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikadiria kukusanya mapato ya
shilingi bilioni 8,070. Hadi kufikia Aprili, 2013, TRA ilikusanya shilingi
bilioni 6,580 sawa na asilimia 97.84 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni
6,725 katika kipindi hicho.
72.
Mheshimiwa Spika,
makadirio ya matumizi
ya Fungu 21 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa
shilingi bilioni 725.57 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi
bilioni 101.95 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Aidha,
kiasi cha Shilingi bilioni 50.66 kilifanyiwa uhamisho kuongezea katika zoezi la
Sensa ya Watu na Makazi na kufanya makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa mwaka
2012/13 kuwa shilingi bilioni 152.61. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida
yalifikia shilingi bilioni 516.61 sawa na asilimia 71.2 ya makadirio, na
matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 131.95 sawa na asilimia 86.46
ya makadirio.
Fungu 13 – Kitengo
cha Udhibiti wa Fedha Haramu
73.
Mheshimiwa Spika,
makadirio ya matumizi
ya Fungu 13 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa
shilingi bilioni 2.16 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi
bilioni 0.26 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili,
2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 1.01 sawa na asilimia
46.62 ya makadirio, na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 0.04
sawa na asilimia 14.72 ya makadirio.
Fungu
10 – Tume ya Pamoja ya Fedha:
74. Mheshimiwa
Spika, makadirio ya matumizi ya kawaida kwa Fungu hili yalikuwa
shillingi bilioni 1.99, hadi kufikia Aprili, 2013 matumizi yalifikia shilingi
bilioni 1.33 sawa na
asilimia 66.83 ya makadirio.
Fungu
45- Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
75.
Mheshimiwa Spika,
makadirio ya matumizi
ya Fungu 45 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa
shilingi bilioni 55.02 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi
bilioni 9.62 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili,
2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 39.51 sawa na asilimia
71.81 ya makadirio, na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 3.18
sawa na asilimia 33.0 ya makadirio.
MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA
2013/14
76. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, majukumu ya Wizara
yatatekelezwa katika mafungu saba ya kibajeti. Mafungu hayo ni Fungu 50 -
Wizara ya Fedha; Fungu 23 - Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali; Fungu 22 - Deni
la Taifa; Fungu 21 – HAZINA; Fungu 13 - Kitengo cha
Udhibiti wa Fedha Haramu; na Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha na Fungu
7- Ofisi ya Msajili wa
Hazina.
Aidha,
Fungu 45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ambayo inajitegemea litaendelea kuombewa
fedha Bungeni na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa Sheria.
Mapato
77. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara ya Fedha
inakadiria kukusanya mapato yasiyo ya kodi yapatayo shilingi 2,718,102,000
(bilioni 2.72) kupitia Fungu 50 - Wizara ya Fedha
na shilingi 124,013,512,000
(bilioni 124.01) kupitia Fungu 7- Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Maombi ya Fedha
78. Mheshimiwa
Spika, baada ya kueleza kwa kina
utekelezaji wa majukumu na kazi za Wizara kwa mwaka 2012/13 na mpango na
malengo ya bajeti kwa mwaka 2013/14,
sasa napenda kuwasilisha rasmi mapendekezo ya maombi ya fedha kwa mwaka
2013/14 kwa ajili ya matumizi ya Fungu 50, 23, 22, 21, 13, 10, 7, na 45 kama ifuatavyo:-
Fungu 50 – Wizara ya Fedha
79. Mheshimiwa
Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a) Matumizi ya kawaida Shilingi 53,011,091,000 (bilioni 53.01). Kati ya hizo Mishahara
ni shilingi 4,564,609,000 (bilioni 4.56) na matumizi mengineyo shilingi
48,446,482,000 (bilioni 48.45).
(b) Miradi ya Maendeleo Shilingi 233,669,169,000 (bilioni
233.67). Kati
ya hizo:-
(i) Fedha
za Ndani - Shilingi 10,200,000,000 (bilioni
10.20).
(ii) Fedha
za Nje - Shilingi 223,469,169,000 (bilioni 223.47).
Fungu
23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali:
80. Mheshimiwa
Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara
inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a)
Matumizi ya kawaida - Shilingi
80,831,672,000 (bilioni 80.83).
Kati ya hizo
Mishahara shilingi 4,434,410,000
(bilioni 4.43) na matumizi mengineyo shilingi 76,397,262,000 (bilioni
76.40).
(b)
Miradi ya Maendeleo – Shilingi
4,755,547,000 (bilioni
4.76) Kati
ya hizo:-
(i) Fedha za Ndani -Shilingi
400,000,000 (bilioni 0.40).
(ii) Fedha
za Nje -Shilingi 4,355,547,000
(bilioni 4.36).
Fungu
22- Deni la Taifa
81. Mheshimiwa
Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara
inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi
3,319,017,772,000 (bilioni 3,319.02). Kati ya hizo Mishahara
ni shilingi 6,311,772,000 (bilioni 6.31) na matumizi mengineyo ni
shilingi 3,312,706,000,000 (bilioni 3,312.71).
Fungu
21 - HAZINA:
82. Mheshimiwa
Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a)
Matumizi ya kawaida Shilingi 1,378,142,566,000
(bilioni 1,378.14). Kati ya hizo mishahara ni
shilingi 2,632,424,000 (bilioni 2.63) na matumizi
mengineyo shilingi 1,375,510,142,000 (bilioni 1,375.51)
ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya Idara na Taasisi zilizo chini ya Fungu hili,
nyongeza ya mishahara ya Watumishi wa Serikali na matumizi maalum.
(b)
Miradi ya maendeleo ni shilingi 38,190,162,000
(bilioni 38.19).
Kati ya hizo:-
(i)
Fedha za Ndani- Shilingi 7,893,000,000
(bilioni 7.89)
(ii) Fedha
za Nje- Shilingi 30,297,162,000 (bilioni 30.30)
Fungu 13 – Kitengo
cha Udhibiti wa Fedha Haramu:
83.
Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha
fedha kama ifuatavyo:-
(a)
Matumizi ya kawaida - Shilingi
1,944,790,000 (bilioni 1.94).
(b) Miradi ya Maendeleo,
fedha za nje Shilingi 399,985,000 (bilioni 0.39).
Fungu
10 – Tume ya Pamoja ya Fedha:
84.
Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha
Shilingi 2,064,424,000 (bilioni 2.06) kwa matumizi ya kawaida. Kati ya
fedha hizo, shilingi 362,771,000
(bilioni 0.36) ni
kwa ajili ya mishahara na shilingi 1,701,653,000 (bilioni 1.70) ni matumizi mengineyo.
Fungu 7 – Ofisi
ya Msajili wa Hazina:
85.
Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha
fedha kama ifuatavyo:-
(a)
Matumizi ya kawaida - Shilingi
38,088,142,000 (bilioni 38.08).
Kati
ya hizo shilingi 303,192,000 (bilioni
0.30) ni kwa ajili ya mishahara na shilingi
37,784,950,000 (bilioni 37.78) ni matumizi
mengineyo.
(b) Miradi ya Maendeleo - Shilingi 1,665,300,000
(bilioni
1.67) Kati ya
hizo:-
(i) Fedha za Ndani -Shilingi
600,000,000 (bilioni 0.60).
(ii) Fedha
za Nje -Shilingi 1,065,300,000
(bilioni 1.07).
Fungu
45: Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
86.
Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha
fedha kama ifuatavyo:-
(a) Matumizi ya kawaida shilingi 57,406,414,000
(bilioni 57.40). Kati ya hizo mishahara ni shilingi 6,692,935,000 (bilioni 6.69) na matumizi mengineyo
shilingi 50,713,479,000 (bilioni 50.71).
(b) Miradi ya maendeleo shilingi 21,449,100,000 (bilioni 21.45),
kati ya hizo:-
(i)
Fedha za ndani shilingi 15,250,000,000 (bilioni 15.25).
(ii)
Fedha za nje shilingi 6,199,100,000 (bilioni 6.20).
HITIMISHO
87.
Mheshimiwa
Spika, napenda
kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba ya bajeti ya
Wizara inapatikana katika tovuti ya Wizara (www.mof.go.tz) Aidha, naomba hotuba kama ilivyo
kwenye kitabu iingizwe kwenye
“Hansard”.
88. Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment