Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
SEREKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza kuwa inaendelelea kufuatilia na kuchukua hatua za tahadhari za kiulinzi na usalama kwa kuanzisha operesheni maalum katika maeneo yote yanayotiliwa mashaka ya kuweza kutokea kwa mashambulio ya kigaidi.
Akijibu swali leo katika mkutano wa kumi na mbili wa Baraza la Wawakilishi ulioanza jana mjini Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed alisema pamoja na hatua hizo serikali pia ilikaa na kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mikoa yote kujadili tishio hilo na kukubaliana kuendeleza elimu juu ya dhana ya ulinzi shirikishi na polisi jamii katika vijiji vyote vilivyopo kando kando ya bahari ya hindi.
Aidha alisema kwa kuwa Zanzibar inategemea kwa kiasi kikubwa mapato ya utalii jeshi la polisi kwa kushirikiana na vikosi vya serikali ya Zanzibar na wananchi wameendeleza doria katika maeneo mbali mbali ya ili kukabiliana na aina zote za uhalifu unaojitokeza hususani katika maeneo ya fukwe.
“Jeshi la polisi kwa kushirikiana na vikosi vya SMZ na wananchi wanaendelea na wajibu wao wa kulinda raia na mali zao katika maeneo mbali mbali ya nchi yakiwemo ya fukwe na baharini kwa kutumia boti maalum”, alisema Waziri Aboud na kuongeza kuwa ujenzi wa vituo vya polisi katika maeneo ya Kiwengwa, Fumba, Nungwi na Nungwi.
Swali hilo lililoulizwa na mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na tishio la ugaidi kufuatia taarifa ya uwezekano wa kutokea kwa mashambulio hayo katika ukanda wa Afarika Mashariki iliyotolewa na jeshi la polisi mnamo mwezi April mwaka huu.
Aidha akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi huyo juu ya mpango wa serikali ya Zanzibar kuwajengea uwezo watendaji wa jeshi hilo na kuondokana na kufanya kazi kwa kubahatisha waziri Aboud alisema kuwa pamoja na kuwa kikatiba jeshi la polisi linahudumiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano bado Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inasaidia katika utendaji wa kazi za jeshi hilo kwa kulipatia nyenzo na vifaa mbali mbali hususan katika utekelezaji wa mpango wa uimarishaji wa jeshi hilo kwa lengo la kuleta ufanisi na kufanya wajibu wao kwa kuzingatia utaalamu.
Kuhusu swali kama serikali haioni umuhimu wa kuvitumia vikosi vya SMZ kwa ulinzi wa maeneo yalipo mahoteli ya kitalii kama moja ya njia ya kuhakikisha usalama wa watalii na utekelezaji wa dhana ya utalii kwa wote lililoulizwa na Mansour Yussuf Himid mwakilishi wa jimbo la Kiembe samaki - CCM, Aboud alisema tayari serikali kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya utalii imeunda kikosi maalum cha ulinzi na mipango inafanywa ili kukiwezehsa kikosi hicho kwa lengo la kuleta tija katika sekta ya utalii na uchumi wa Zanzibar na watu wake.
ZAO LA MWANI
Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Mhe. Thuwaiba Edington Kisasi |
WIZARA ya biashara, viwanda na masoko kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimekusudia kufanya utafiti kwa lengo la kuangalia uwezekano wa kusarifu bidhaa zinazotokana na zao la mwani ili kuongeza kipato cha wakulima wa zao hilo.
Naibu Waziri wa wizara hiyo Thuwaiba Edington Kisasi ameliambia Baraza la Wawakilishi kuwa serikali inatambua juhudi kubwa zinazochukuliwa na wananchi wake katika uzalishaji wa zao hilo ambazo hazilingani na tija wanayoipata kutokana na kuwa bei ya bidhaa hiyo kuporomoka siku hadi siku.
“Tunatambua juhudi za wakulima wetu na matatizo yanayowakuta na wizara katika kulitafutia ufumbuzi jambo hili ilifanya ziara katika nchi zinazosafirisha mwani kama Zanzibar ili kubadilishana uzoefu katika masoko ya zao hilo na kuona namna gani tutaweza kuinua maslahi ya wananchi wanaojishughulisha na kilimo hicho”, alisema Kisasi.
Aliongeza kuwa ili kuinua mapato ya wakulima hao kwa sasa wizara yake imeona umuhimu wa kuanzisha viwanda vya kuusarifu mwani na kuuongezea thamani badalaya kuusafirisha kama kama bidhaa ghafi.
Awali akiuliza swali la msingi na jengine la nyongeza mwakilishi wa Viti Maalum Wanawake Bikame Yussuf Hamad alitaka kujua iwapo serikali inatambua usumbufu unaowapata wanawake wanaojishughulisha na kilimo cha mwani kutokana na kutokuwepo kwa uhakika wa soko la bidhaa hiyo kiasi cha kuwasababishia hasara na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na tatizo hilo.
Akitoa majibu ya nyongeza Waziri wa wizara hiyo Nassor Ahmed Mazrui kufuatia swali la nyongeza la mwakilishi wa viti maalum wanawake Asha Bakari Makame aliyeuliza juu ya sababu za kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo alisema, hali hiyo imechangiwa na ongezeko la uzalishaji wa bidhaa hiyo kuliko mahitaji katika soko la dunia.
Aidha aliongeza kuwa aina ya mwani unaozalishwa nchini na ubora wake kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia kutokuwa na soko la uhakika na bei nzuri.
“Tanzania inasafirisha wastani wa tani 15,000 za zao hili kwa mwaka lakini kutokana aina ya mwani unaozalishwa kuwa na na bei ya kiwango cha chini kuliko aina zingine ndio chanzo cha kutokuwa na soko la uhakika linalopekekea tija kwa wakulima wetu”, alisema Mazrui na kuwataka wakulima kuendelea na uzalishaji na mawakala kuendelea kununua kwa bei ilyopo wakati serikali inafanya jitihada za kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo.
JUMLA ya vijana 58 walioamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya wanaoishi katika nyumba za kurekebisha tabia (sober house) ziliopo katika shehia za Bububu, Nyarugusu, Uzi meli nne na katika Jumuiya ya ‘Zanzibar Youth Forum’ wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali kama njia moja wapo ya kuwasaidia kuanza maisha yao ya kawaida katika jamii.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Fereji aliyasema hayo leo, alipokuwa akijibu swali la mwakilishi wa viti maalum wanawake Wanu Hafidh Ameir ambaye alitaka kujua iwapo serikali inatoa msaada wowote kwa vijana hao ili kuhakikisha hawarejei katika vitendo hivyo baada ya kutoka katika nyumba hizo.
Fereji alisema wizara yake kwa kusirikiana na Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi kiuchumi na Ushirika kupititia mpango wake wa ‘kazi nje nje’ waliwapatia mafunzo mbali mbali ya kazi za ujasiriamali ili waweze kujitegemea, mafunzo ambayo yalifadhiliwa na jumuiya ya kimataifa ya Youth Forum ya Canada.
Aidha alisema kuwa taasisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) kanda ya Africa yenye makao makuu yake nchini Kenya imefikia makubaliano na wizara yake ya kuisaidia mradi wa ufugaji ng’ombe wa maziwa katika shehia ya Limbani kisiwani Pemba na kuitaka jamii kuacha kuwabagua na kuwanyanyapaa badala yake kuwasaidia kujenga mustakabali mzuri wa maisha yao ya baadae na kuachana na vitendo viovu.
Aliongeza kuwa bado wizara yake kwa kushirikiana na wamiliki wa nyumba na vituo hivyo wanaendelea na mpango wa kurekebisha imani za vijana wanaotunzwa katika nyumba hizo kwa kualika viongozi wa dini tofauti ili kuwahubiria na kuwaonya ili kuwajenga kiamaadili na na kuachana na vitendo viovu wanaporudi katika jamii.
Akijibu swali la nyongeza kama serikali haioni haja ya kuziwezesha nyumba hizo na kuanzisha kituo chake kwa lengo la kukusanya vijana wengi zaidi lililoulizwa na Amina Juma Mbarouk (Viti Maalum wanawake), Ferji alisema wizara yake ilitenga kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano kwa kila kituo lakini kutokana fedha hizo kuelekezwa katika ununuzi wa meli ya serikali fedha hizo hazikupatikana na kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha fedha hizo zimeombwa.
“Tulipanga kila kituo kukipatia kiasi cha shilingi milioni moja na nusu lakini hadi mei fedha hizi tulikuwa hatujazipata na tunazitegemea katika mwaka ujao wa fedha”, alisema Fereji na kuongeza kuwa kiasi cha shlingi milioni 100 kimetengwa kwa ajili ya kujenga kituo cha serikali kwa ajili hiyo.
Kuhusu mkakati wa wizara yake katika kukomesha biashara za kulevya nchini alisema kutokana nakuwepo takribani vijana 8000 walioathirika na dawa za kulevya wizara yake kupitia tume ya kuratibu dawa za kulevya imekuwa ikitoa elimu kwa vijana katika maeneo mbali mbali nchini ili kuwanusuru vijana ambao hawajaanza kutumia na wale ambao wameshathiriwa na dawa hizo kwa lengo la kubadili tabia.
“Hizi nyumba hazipo kwa ajili ya kuchochoa ongezeko la watumiaji wa dawa za kulevya bali kuwarekebisha wale walioathirika na kuwazuia wale ambao bado hawajaanza”, alisema na kuwataka wajumbe wa baraza hilo na wananchi kwa ujumla kushirikiana katika kupiga vita dawa za kulevya kwa kuwafichua waingizaji na wauzaji wa bidhaa hizo.
Swali hilo liliulizwa na mwakilishi wa jimbo la Kwahani CCM Ali Salum Ali aliyetaka kujua mkakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya vita dhidi ya dawa za kulevya kwa lengo la kuwanusuru vijana wa Zanzibar ambao ndio waathirika wakubwa.
No comments:
Post a Comment