TANGAZO


Friday, May 10, 2013

Wizara yatoa ufafanuzi kuhusu kupitiwa upya kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka


1

Dk. Shukuru  Kawambwa

Mnamo tarehe 03 Mei, 2013 Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Wiliam Lukuvi (Mb) ilitoa Kauli ya Serikali Bungeni Kuhusu Taarifa ya Awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Sababu za kushuka kwa ufaulu wa Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012.

 Kauli ya Serikali ilielekeza kuwa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yafutwe na yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011 ili Wanafunzi hao wawe  katika  mazingira  yanayofanana na ya wenzao wa  miaka  iliyopita kwa kuwa mfumo uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia.
Kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume na Maelekezo ya Baraza la Mawaziri, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania, kifungu cha 20, sura 107 ameliagiza Baraza la Mitihani la Taifa kupitia upya Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012. Aidha, imeagizwa kwamba matokeo hayo yaandaliwe kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011. Serikali haikuagiza kufanyika upya kwa mitihani hiyo na wala haikuagiza kusahihishwa upya.

 Hivyo, Serikali inapenda kuwahakikishia wananchi kwamba hapatakuwa na zoezi la kurudia usahihishaji wa mtihani huo kwa sababu hakuna dosari zilizobainishwa kwenye usahihishaji wa mitihani hiyo. Alama za watahiniwa ambazo zimehakikiwa zipo tayari, kitakachofanyika ni kwa Baraza la Mitihani kutumia alama hizo kuchakata matokeo upya kwa kutumia viwango vya ufaulu vilivyotumika mwaka 2011.

 Utaratibu ambao umekuwa ukitumika tangu mwaka 1973 wakati Baraza lilipoanzishwa, ni wa kuweka viwango vya ufaulu kila mwaka kwa kuzingatia ufaulu wa somo husika na ufaulu katika mwaka uliotangulia.

 Kutokana na maelezo hayo, ni dhahiri kuwa zoezi la kupitia upya matokeo ya Kidato cha Nne 2012 litachukua muda mfupi na matokeo yatatangazwa hivi karibuni..
Selestine Gesimba
KAIMU KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
10/05/2013

No comments:

Post a Comment