TANGAZO


Tuesday, May 14, 2013

Wanywaji wa Viroba: Vikipigwa marufuku tutarudi kunywa gongo

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara, wakiangalia uzalishaji walipotembelea kiwanda cha Konyagi cha Tanzania Distilleries Limited (TDL), Dar es Salaam hivi karibuni.

 Na Mwandishi Wetu.
BAADHI ya wananchi jijini Dar es Salaam, wamelalamikia hoja iliyozuka bungeni wiki hii kwamba kinywaji cha Konyagi aina ya Kiroba kipigwe marufuku nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao, walisema endapo serikali itachukua uamuzi wa kupiga marufuku kinywaji hicho, watarudia kunywa pombe aina ya gongo ambayo ni hatari kwa afya zao.

Mkazi wa Mbagala, Faustine Mwiruka aliyekutwa kwenye baa ya Kisuma, aliiasa Serikali kutothubutu kukubali kinywaji hicho kupigwa marufuku, kwani ikifanya hivyo wengi wa wananchi wenye kipato cha chini wataanza tena kunywa gongo na pombe za kienyeji.

Itabidi tufanye kama Zambia  ambao wamezuia viroba, lakini nchi nzima imejaa viroba vya Malawi, Zaire na Burundi, lazima tuiadhibu serikali ikose kodi kote kote, bia hatunywi, viroba vya nje tutakunywa, pamoja na gongo.


Alisema haingii akilini kukihusisha kinywaji hicho na ajali za magari, akidai kuwa hata kabla ya viroba kuingia sokoni ajali zilikuwepo nyingi.

"Sisi tuna imani na viroba kwa vile vina ubora wa uhakika tofauti na pombe ya gongo ambayo inapikwa bila kupimwa ubora hivyo ni hatari kwa usalama wa afya zetu." alisema Mwiruka.

Naye Ali Hassan mkazi wa Kinondoni kwa Manyanya, alisema, wanaotaka viroba vipigwe marufuku hawawatendei haki wananchi wa kawaida ambao kwa asilimia kubwa hawana uwezo wa kununua bia ambazo bei yake ni kubwa.

Mwandishi wetu aliyetembelea maeneo ya Ilala Kota Mchikichini alifanikiwakuhojiana na wakazi wa eneo hilo ambao wengi wao walisema kuwa jambo hilo lililozushwa wiki iliyopita wanaamini ni njama za wafanya biashara toka nchi jirani ambao hawaitakii mema Tanzania  kwa kuwa pombe hiyo kuwepo kwake pia kunakuza pato la Taifa.

Juma Pingu alisema kuwa haoni sababu ya kupiga marufuku viroba kwakuwa ni pombe ya wanyonge na kuwataka wabunge kuthamini bidhaa za nyumbani kwanza.

No comments:

Post a Comment