TANGAZO


Monday, May 27, 2013

Rais Dk. Shein awataka wanafunzi kurudi nyumbani wamalizapo masomo yao nchini China kuongeza kasi ya maendeleo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na mkewe, Mama Mwanamwema Shein pamoja na ujumbe aliofuatana nao, wakiwasili katika Uwanja wa ndege  wa Beijing nchini China kwa ziara ya mwaliko wa Serikali wa Jamhuri hiyo. (Picha zote na Ramadhan Othman, China)
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Balozi Mdogo wa China nchini Tanzania, anayefanyia kazi zake Zanzibar, Bi. Chen Qiman, mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Beijing nchini China kwa ziara ya mwaliko wa Serikali ya Jamhuri hiyo.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini China katika chumba cha VIP, uwanjani hapo, alipowasili kwa ziara ya mwaliko wa Serikali wa Jamhuri hiyo.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na mkewe, Mama Mwanamwema Shein, wakiwa katika mapunziko mafupi katika chumba cha Viongozi Wakuu VIP, walipokaribishwa na Balozi Mdogo wa China nchini Tanzania, anayefanyia kazi zake Zanzibar, Bi. Chen Qiman (kulia), mara baada ya kuwasili Uwanja wa ndege wa Beijing nchini China kwa ziara ya mwaliko wa Serikali wa Jamhuri hiyo leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na mkewe, Mama Mwanamwema Shein, wakikaribishwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Philip  Marmo pamoja na mkewe, Hoteli ya China World, mjini Beijing nchini China akiwa katika ziara ya Kiserikali kwa mwaliko wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
 Baadhi ya Watanzania waliohudhuria katika mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alipofanya mazungumzo na nao  katika ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania nchini China, mjini Beijing, akiwa katika ziara ya Kiserikali nchini humo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Watanzania waliopo nchini China leo. Wengi wao wakiwa ni wanafunzi wanaosomea fani mbalimbali, mazungumzo hayo, yalifanyika katika ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania, nchini China mjini Beijing. 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka Watanzania wanaosoma nje ya nchi kurudi nyumbani wamalizapo masomo yao, ili wasaidie kujenga mazingira mazuri ya kuharakisha maendeleo.


Dk. Shein amesema hayo leo, mjini Beijing China wakati alipokuwa akizungumza na watanzania walioko nchini humo mwanzoni mwa ziara yake ya kikazi ya siku saba nchini China.


“Mkimaliza mrudi nyumbani kuitumikia nchi yenu kwa bidii kwani hakuna atakayetujengea nchi yetu” aliwaeleza watanzania hao ambao wengi wao ni wanafunzi katika vyuo mbalimbali nchini humo.


Alifafanua kuwa mipango mikubwa ya Maendeleo ya taifa kama vile Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020 na Dira ya Mendeleo ya Tanzania Bara 2025 pamoja na mipango ya kupambana na umasikini ya MKUKUTA na MKUZA haiwezi kufanikiwa bila ya jitihada za watanzania wenyewe.


“China ni mfano mzuri kwetu, tujifunze kutoka kwao wanafanya kazi kwa bidii na sasa nchi yao imepiga hatua hadi kuwa nchi ya pili yenye uchumi mkubwa huku ukikua kwa kasi ya asilimia 10 kwa mwaka”alifafanua.


Amewataka watanzania hao kuthamini mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China wa kuwapa fursa za masomo katika nchi hiyo kwa  kujifunza kwa bidii ili sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya China na Tanzania.


“Mwaka jana watanzania 900 walipata nafasi za masomo nchini humu na Serikali ya China imeahidi kutuongezea hivyo tuzitumie vyema fursa hizi kuendeleza nchi yetu” aliwaambia.


Dk. Shein amesema ziara yake nchini China ina lengo la kuimarisha uhusiano mzuri wa kindugu na kirafiki uliopo kati ya Tanzania na China na kwamba ziara kama hizo zinazofanywa na viongozi ni muhimu kuziweka karibu Serikali na wananchi wa Tanzania na China.


Alibainisha kuwa changamoto mojawapo hivi sasa ni kupunguza pengo la kibiashara kati ya nchi mbili ambapo upande wa Tanzania unaagiza zaidi bidhaa kutoka China huku ikisafiri bidhaa chache nchini humu


Kuhusu hali ya uchumi nchini aliwaleza kuwa kwa ujumla uchumi mwelekeo wa uchumi wa Tanzania kwa kuwa umekuwa kwa asilimia karibu 7 mwaka jana kutoka asilimia 6.3 mwaka 2011 huku mfumuko wa bei ukishuka hadi asilimia 6.8 mwaka jana kutoka asilimia 19.8 kmwaka 2011.


“Kwa upande wa Zanzibar mwenendo wa uchumi wetu umekuwa mzuri kwa mfano mwaka 2011/2012 kiwango cha ukuaji kilikuwa asilimia 6.8 na matarajio kwa mwaka 2012/2013 ni asilimia 7 hadi kufikia asilimia 7.5 mwaka 2013/2014”alifafanua.


Juu ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba Dk. Shein aliwaeleza watanzania hao kuwa mchakato huo unakwenda kama ulivyopangwa na kuwahakikishia kuwa unafanyika kwa uwazi na kufuata taratibu zilizowekwa za kuendesha mchakato huo.


"Mchakato unaendelea vyema kama ulivyopangwa na Tume inatekeleza majukumu yake kama hadidu za rejea zilizovyoelekeza na inafanya hivyo kwa uwazi "alieleza


Wakati huo huo Balozi wa Tanzania anayemaliza muda wake nchini China Balozi Philip Marmo ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kudhamini wanafunzi wengi kuchukua masomo mbalimbali nchini China.


Balozi Marmo alieleza kuwa hivi sasa kuna wanafunzi wa kitanzania wengi nchini humo wakiwemo wanaodhaminiwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya Watu wa Chia na wanaojisomesha wenyewe.


“Tuna wanafunzi 249 wanaosomeshwa kupitia Serikali ya China, 31 wanaodhaminiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wengine wanajisomesha wenyewe” alisema Balozi Marmo ambaye alitoa wito kwa Serikali ya Tanzania nayo kudhamini vijana wake kusoma nchini humo.


Balozi Marmo ambaye katika mabadiliko ya hivi karibuni alimehamishiwa nchini Ujerumani alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na China hivi sasa ni mzuri na kuongeza kuna haja ya kuongeza watumishi katika ubalozi hapa China kwa kuwa kumekuwa na mahitaji mengi kwa vile watanzania wengi hivi sasa wanakuja China kufanya shughuli mbalimbali kama masomo na biashara.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kesho pamoja na mambo mengine anatarajiwa kuwa na mazungumzo rasmi na Rais wa China Bwana Xi Jinping na Makamu wa Rais Bwana Li Yuanchao.

No comments:

Post a Comment