TANGAZO


Tuesday, May 14, 2013

Kamati ya Uchunguzi wa Hesabu za Serikali Zanzibar, wakaa kikao na wadau wake

 
Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza Hesabu za Serikali (P.A.C), Omar Ali Shehe, akizungumza na wadau mbalimbali wakiwemo wandishi wa habari kwa lengo la kupata mashirikino na ufanisi katika utendaji wa kazi zao. Kikao hicho kilifanyika Baraza la Wawakilishi Mbweni, nje kidogo ya mji Zanzibar leo. (Picha zote na Makame Mshenga - Maelezo Zanzibar)

Mwandishi wa habari, Salum Vuai, akitoa mchango wake kuhusu majukumu ya Kamati ya Kuchunguza Hesabu za Serekali wakati wa kikao hicho, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar leo.


Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim akichangia mada katika kikao cha Wadau mbalimbali wakiwemo wandishi wa habari wa vyombo tofauti kwa lengo la kupata mashirikino na ufanisi katika utendaji wa kazi zao. Kulia ni Mhasibu Mkuu wa Serikali, Omar Hassan.



Na Ramadhani Ali-Maelezo Zanzibar                         
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Ibrahim Mzee  Ibrahim amesema Serikali inawajibu wa kuyafanyia uchunguzi wa kina mapendekezo ya Kamati  za Baraza la Wawakilishi na haipaswi kuwachukulia hatua moja kwa moja watu waliotajwa ndani ya taarifa kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa Umma.

Mkurugenzi huyo ameeleza hayo leo, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa pamoja kati ya Kamati ya Uchunguzi wa Mahesabu ya Serikali na Mashirika  (PAC) na wadau wa Kamati hiyo kwenye Ofisi za Baraza la Wawakilishi Chukwani.

Amesema katika kuyapitia na kuyafanyia uchunguzi mapendekezo ya kamati, wahusika wanaotajwa hupewa nafasi ya kujitetea kabla ya kuyatolea uamuzi na kazi hiyo  huchukua muda kukamilika.

“Serikali haiwezi kuyachukulia hatua mapendekezo yote yanayotolewa na Kamati  ya Baraza bila ya kuwapa nafasi ya kujitetea  watuhumiwa  na kubaini wanaostahiki ili kuchukuliwa hatua za kinidhamu na wengine kupelekwa mahakamani  kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma”, alieleza Ibrahim Mzee.

Ameitaka Kamati ya PAC kuelewa kwamba kuna mchakato mkubwa unaotekelezwa na Serikali  kabla ya kuchukua hatua zinazostahiki kwa wahusika na haipaswi kupewa shinikizo na chombo chochote.

Amesema kazi ya Kamati ya PAC ni kuchunguza na kuishauri Serikali bila ya kutumia vitisho wala kutoa hukumu na kuipa muda Serikali kufanya wajibu unaostahiki ikiwa ni pamoja na kuwachukuliwa hatua waliobanika na makosa.

Mkurugenzi wa Mashtka alieleza kwamba kumekuwa na muingiliano wa kazi kati ya kamati moja ya Baraza la Wawakilishi na Kamati nyengine na hivyo kupelekea kamati mbili kuhoji jambo moja.

“Kamati mbili ama zaidi kuhoji kitu kimoja ni kasoro kubwa hivyo inafaa mujipange vizuri  ili kila kamati ijuwe wajibu wake”, alisisitiza Mkurugenzi wa Mashtaka.

Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo Khamis Mussa Omar ameitaka kamati ya PAC wanapowasilisha  taarifa katika Baraza  kupunguza hamasa kwani mara nyingi hujenga picha kwa jamii kuwa  wahusika ni wizi na mafisadi.

Akiwashukuru wadau wa PAC Mwenyekiti wa Kamati hiyo Omar Ali Shehe ameomba kujenga mashirikiano ya karibu kati yao na wadau wengine ili kufanikisha majukumu yao yao ya kazi.

Amewahakikisha wadau hao kwamba  Kamati ya PAC haina nia ya kumuonea Mtendaji yeyote wa Serikali lakini kubwa wanalofanya ni kuhakikisha rasilimali chache zilizopo Nchini zinawanufaisha Wananchi wote kwa mujibu wa nafasi zao.

Wadau walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa mahesabu ya Serikali, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Muhasibu Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashtaka na Vyombo vya Habari.

No comments:

Post a Comment