![]() |
| Rais wa Zanzibar, Dk. Shein |
Na Said Ameir, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Wazanzibari watamkumbuka msanii Bibi Fatma Baraka Khamis, maarufu Bi. Kidude kwa kujijengea sifa na heshima kubwa kwa kuwa alitumia muda mwingi wa maisha yake kuenzi na kukuza mila, desturi na silka za Wazanzibari.
“Tutamkumbuka kutokana na umahiri wake katika sanaa ambayo aliitumia kukuza silka zetu, mila zetu na desturi zetu hivyo alikuwa mtu muhimu katika Taifa letu na tutamkubuka pia kwa mema yake” kwa huzuni, Dk. Shein aliiambia familia ya marehemu na kuongeza kuwa marehemu aliweka mbele utu wa Wazanzibari.
Dk. Shein aliwaeleza wanafamilia na watu waliohudhuria msiba huo kuwa yeye binafsi alishakutana na marehemu mara nyingi na kuzungumzia masuala mbalimbali na kutolea mfano mazungumzo yake ya karibu saa mbili wakati akiwa mgombea urais wa Zanzibar mwaka 2010.
“kwa hakika alikuwa mtu wa watu aliyejenga mlahaka na kila mtu “ alimuelezea marehemu na kuwaomba waombolezaji kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi.
Dk. Shein aliwakumbusha kumcha Mwenyezi Mungu kwa kujiandaa na safari ya milele kwani kama yanavyoeleza mafundisho ya Quran tukufu kila roho itaonja mauti hivyo kifo cha msanii huyo iwe ni fundisho kwetu sote.
![]() |
| Marehemu Bi. Kidude wakati wa uhai wake |
Mbali ya viongozi wakiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein walikuwepo pia Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Sheif Shariff Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.
Mazishi hayo yalihudhuriwa pia na wasanii wa mbali mbali na wadau wa sanaa wa hapa Zanzibar na wengine kutoka Tanzania Bara. Wadau hao ni pamoja na wasanii kutoka Tanzania wakiwemo Nasib Abdul maarufu ‘Diamond’, Farid Kibanda ‘Fid Q’ na bwana Ruge Mutahaba ambaye ni mdau mkubwa wa sanaa ya muziki.
Katika mazishi hayo serikali imesema itamuenzi marehemu kwa kuweka katika makumbusho kazi zake mbalimbali za kisanii alizozifanya msanii huyo.
Risala ya serikali iliyosomwa na Bwana Hassan Vuai ilieleza kuwa Bi Kidude atakumbukwa kwa kuitangaza Zanzibar tangu wakati alipoanza sanaa ya muziki wa taarab na kuhamia huko Tanzania Bara ambako aliimbia kikundi cha taraab cha Egyptian Musical Club.
Aidha, marehemu ambaye amefariki akiwa na umri upatao miaka 90 imeeleza risala hiyo kuwa katika uhai wake amesafiri na kuonyesha sanaa katika nchi zipatazo 50 na kushiriki maonyesho yapatayo 100 ambapo miongoni mwao aliwahi kupewa tuzo kwa kazi zake.


No comments:
Post a Comment