Na Waandishi wetu-MAELEZO_Dar es Salaam.
Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano kimataifa imeshauri Serikali kutoa fursa kwa watanzania wanaoishi nje ya nchi kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ili kukuza uchumi wetu.
Kauli hiyo imetolewa jana na wajumbe wa Kamati hiyo ilipokutana na viongozi waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano Kimataifa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya bajeti ya mwaka 2013/2014
Walisema wakati umefikwa kwa Watanzania wanaoishi nje ya Nchi kutowekewa vikwazo katika kupata taarifa muhimu zinazohusu sekta mbalimbali za uchumi ili waweze kuja kuwekeza badala ya fedha zao kukaa nazo nje ya Tanzania .
Waliongeza kuwa ni vema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ikaunda Kitengo maalum cha diplomasia ya uchumi kitakachoshirikisha wataalamu wa sekta mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika utangazaji wa fursa za uwekezaji nchini kwa ili kuboresha nyanja za uchumi kupitia Watanzania waishio nje.
Akijibu baadhi ya hoja za wajumbe wa Kamati hiyo Naibu Waziri wa Wizara wa Mambo ya Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Mahadhi Maalim alisema kuwa Serikali hivi sasa inaendelea kutangaza fursa mbalimbali ambazo zipo Tanzania ambapo tayari wawekezaji kutoka Oman wameshaonyesha nia ya kuwekeza nchini.
Alisema kuwa wawekezaji hao wanakusudia kununua nyama ambapo pia watajenga machinjio ya kisasa ambayo yatatumika kuchinjia mifugo kabla ya nyama haijasafirishwa kwenda nje ya Tanzania .
No comments:
Post a Comment