Mwenyekiti wa Maandalizi ya Tamasha la Pasaka,
Alex Msama akifafanua jambo, wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam leo, kuhusu maandalizi ya tamasha hilo, lenye kauli mbiu ya Amani na
Upendo. Kulia ni Mdau wa muziki wa Injili, Mcharo Mrutu wa Chanel Ten.
Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya maandalizi ya tamasha hilo.
Alex Msama akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo kuelezea maendeleo ya maandalizi ya tamasha hilo. (Picha zote na Francis Dande)
Na Francis
Dande
WARATIBU wa tamasha la
Pasaka litakalofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Machi 31, mwaka huu,
wamepanga kutumia sehemu ya mapato ya kiingilio cha tamasha hilo, kujenga kituo cha watoto
yatima kama ishara ya shukrani kwa jamii.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam leo, Mwenyekiti wa Kamati maalumu inayoratibu tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama, alisema kituo hicho
kitakachokuwa chini ya kampuni ya Msama Promotions kitajengwa eneo la
Pugu.
Alisema uamuzi huo umefikiwa
kwa lengo la kuwapa faraja watoto yatima ambao nao wana haki ya kupatiwa matunzo
na mahitaji muhimu katika makuzi yao ikiwemo elimu katika kujenga taifa bora la
kesho.
“Tangu kuasisiwa kwa tamasha
la Pasaka mwaka 2000, tumekuwa tukirejesha sehemu
ya mapato ya viingilio kwa
jamii kwa njia ya misaada kwa yatima, wajane na walemavu, lakini safari hii
tumeona twende zaidi ya hapo kwa kujenga kituo cha watoto,”
alisema.
Alisema lengo ni kujenga
kituo hicho cha kisasa ambapo kama mipango itakwenda vizuri, kitakamilika kabla
ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake kwani wangependa ndiye akizindue kwa
kutambua mchango wake kwa tamasha hilo.
“Mwaka 2011, Rais Kikwete
ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wa tamasha letu pale Diamond Jubilee, jijini
Dar es Salaam .
“Kitendo cha Rais kuacha kazi
nyingi na kuja kutuunga mkono kwenye shughuli hii ya kiroho, kwetu ni jambo
kubwa sana ambalo kamwe hatutalisahau, hivyo
tumeona tumpe heshima hiyo ya kuzindua kituo hicho akiwa bado madarakani,”
alisisitiza.
Msama ametoa wito kwa
wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa injili kujitokeza kwa wingi kuunga
mkono juhudi za kampuni yake kuandaa tamasha hilo kwa malengo mbalimbali ikiwemo
kueneza injili ya Mungu na kusaidia makundi maalumu.
Kuhusu waimbaji, Msama
alisema wale wa nje wataanza kuwasili wiki ijayo na kuongeza kuwa hadi kufikia
Ijumaa, waimbaji wote watakuwa wamefika tayari kwa tukio hilo, ambalo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda.
Aliongeza kuwa idadi ya
waimbaji imeongezeka baada ya kujitokeza kwa mwingine aliyemtaja kwa jina moja
la Ntutuma kutoka nchini Kenya.
Baada ya kishindo cha tamasha
hilo kutikisa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini
Dar es Salaam , itakuwa zamu ya Dodoma , Iringa, Mbeya, Mwanza kabla ya mashambulizi
kuhimishwa mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment