Maafisa wa utawala nchini Afrika Kusini wanasema kuwa rais mstaafu Nelson Mandela anaendelea vyema na matibabu baada ya kulazwa hospitalini kwa siku ya pili akiwa na maradhi ya kifua.
Taarifa kutoka rais wa nchi hiyo Jacob Zuma ilisema kuwa hali ya Mandela inaendelea kuimarika na kwamba hata aliweza kula vyema kiamsha kinywa chake.
Katika mahojiano na BBC , bwana Zuma alisema kuwa watu hawapaswi kuwa na wasiwasi kwani Mandela anaendelea kupokea matibabu.Mapema leo Jacob Zuma,
aliwahakikishia wananchi wa Afrika Kusini kuwa rais mstaafu Nelson Mandela anatibiwa ugonjwa wa mapafu ambao umekuwa ukitokea mara kwa mara.
Mandela mwenye umri wa miaka 94 alilazwa hospitalini kabla ya Jumatano usiku.
Alikuwa hospitalini kwa siku 18 mnamo mwezi Disemba, akipokea matibabu ya mapafu na kibofu.
Katika taarifa yake iliyotolewa mapema, Zuma alisema kuwa Mandela anaendelea kupokea matibabu.
Rais Zuma hata hivyo hajaelezea alikolazwa Mandela.
Miaka muhimu katika maisha ya Mandela
- 1918 Alizaliwa mkoa wa Eastern Cape
- 1943 Ndipo alijiunga na chama cha African National Congress
- 1956 Alishtakiwa kwa kosa la uhaini , ingawa mahakama ilitupilia mbali mashtaka hayo
- 1962 Alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la hujuma na kufungwa jela kwa miaka mitano.
- 1964 Alishtakiwa tena na kufungwa maisha jela
- 1990 Aliachiliwa huru kutoka jela
- 1993 Ashinda tuzo ya amani ya Nobel
- 1994 Alichaguliwa rais wa kwanza mwafrika mweusi nchini Afrika Kusini
- 1999 Aling'atuka mamlakani kama kiongozi kwa hiari
- 2004 Astaafu
- 2005 Atangaza kuwa mwanawe alifariki kutokana na maradhi ya ukimwi
Akiongea na mwandishi wa BBC Lerato Mbele, bwana Zuma alisema kuwa watu wanapaswa kuwa watulivu.
"ndio, nimekuwa nikiwambia watu kukubali kuwa Mandela sio kijana tena na ikiwa atakwenda hospitalini mwara kwa mara kwa ukaguzi wa kiafya, sidhani hilo linapaswa kuwaweka watu wasiwasi.
Ningependa kusema kuwa watu hawapaswi kuwa na wasiwasi hata kidogo,'' alisema Zuma.
Mandela anasifika na kujulikana kama Madiba jina la utani.
Alipohojiwa kuhusu ikiwa watu wa Afrika Kusini wajiandae kwa lolote , Zuma alijibu kusema kuwa ''ikiwa mzee anafariki, watu husema kuwa ameenda nyumbani.
Nadhani hayo ndio baadhi ya mambo ambayo tunapaswa kutafakari.''
Lakini alisisitiza kuwa bwana Mandela ameweza kupokea matibabu vyema.
Bwana Mandela anatazamiwa na wengi kama baba wa taifa kwa kupambana dhidi ya enzi ya ubaguzi wa rangi.
Ni mara ya nne kwa Mandela kulazwa hospitalini katika muda wa miaka miwili.
Aliugua kifua kikuu mapema miaka ya themanini, alipofungwa jela katika kisiwa cha Robben Island, kwa miaka 18.
Mapafu yake inaarifiwa yaliathirika pakubwa kwa sababu ya kufanya kazi katika machimbo ya mawe alipokuwa anahudumia kifungo chake.
Licha ya kufungwa kwa miaka mingi ,Mandela aliwasamehe maadui wake wa zamani alipokuwa rais na kuwataka wanachi wote wa Afrika kusini licha ya rangi yao, kusameheana.
No comments:
Post a Comment