TANGAZO


Friday, February 15, 2013

NEEC na NDC wasaini makubaliano ya ushirikiano wa kuwawezesha wananchi kiuchumi

Mkurugenzi wa Viwanda vya kuongeza Ubora wa Thamani kutoka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Shannel Mvungi akibadilishana hati za makubaliano ya Ushirikiano wa Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Dk. Anaclet Kashuliza (kulia) leo, jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Aron Msigwa - MAELEZO)   


Mkurugenzi wa Viwanda vya Kuongeza Ubora wa Thamani kutoka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Shannel Mvungi akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu namna makubaliano hayo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika maeneo yenye miradi ya NDC, yatakavyofanya kazi.

Na. Aron Msigwa - MAELEZO.
15/2/2013, Dar Es Salaam.
BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi nchini (NEEC) na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), wameanzisha ushirikiano utakaowawezesha wananchi kunufaishwa kiuchumi na rasilimali zinazowazunguka katika maeneo ambayo NDC ina miradi ya maendeleo.

Hayo, yamebainishwa leo, jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa pamoja wa utiaji saini wa makubaliano kuwawezesha wananchi kiuchumi kati NDC na NEEC  yenye lengo la kutoa fursa kubwa za ushiriki wa kiuchumi kwa wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo yenye miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Akizungumza mara baada ya utiaji saini wa makubaliano hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa NDC Bw. Shannel Mvungi amesema kuwa miradi watakayonufaika wananchi ni pamoja na uchimbaji wa Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga Wilayani Ludewa unaotekelezwa na Kampuni ya ubia ya Tanzania China International Minerals Resources Limited ambao inayotarajia kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 5000 kwa wananchi wa  Ludewa.

Amesema kuwa lengo kubwa la  NEEC na NDC ni kuwaendeleza na kuwawezesha wananchi kiuchumi hasa wale walio katika maeneo   ambayo tayari miradi imeanza kutekelezwa  kwa kutoa mafunzo ya ujengaji uwezo na ujuzi katika kutambua fursa zilizopo na jinsi ya kuzitumia, kuhamasisha fursa na miundo mbinu ya kiuchumi, kuwahamasisha wananchi kujiunga katika mitandao ya Vikundi na Masoko.

Fursa nyingine watakazopata wananchi ni pamoja na uwezeshwaji wa upatikanaji wa mitaji na kuunganishwa na Taasisi za Fedha, kuainisha na kuendeleza maeneo huru ya Kufanyia Biashara na kuhamasisha umuhimu wa wananchi kujiunga na Ushirika.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji wananchi kiuchumi Dkt. Anaclet Kashuliza amesema kuwa taasisi hizo zinatarajia kushirikiana vema katika  kuwaunganisha wadau mbali mbali wa maendeleo katika maeneo husika hususani wawekezaji wa sekta binafsi,mashirika yasiyo ya kiserikali,wadau wa maendeleo na serikali za mikoa na wilaya. 

"Ni matarajio ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kuona kuwa rasilimali asilia zikiwanufaisha wananchi katika maeneo yao kwa kuwawezesha kushiriki kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kiuchumi na kubadili hali zao za maisha kupitia ongezeko la kipato na kuboreka kwa miundombinu" Amesema Dkt. Kashuliza. 

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya taasisi hizo Dkt. Kashuliza  amesema kuwa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi hilo lilianzishwa chini ya kifungu cha nne (4) cha Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kazi rasmi mwaka 2005 likiwa ni chombo cha juu cha kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi huku shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linalomilikiwa  kwa asilimia 100 na Serikali liloanzishwa mwaka 1965 kwa lengo la kusimamia  maendeleo ya nchi kupitia viwanda katika sekta zote za uchumi.


No comments:

Post a Comment