TANGAZO


Saturday, February 23, 2013

Majangili watatu wa meno ya Tembo wauawa mkoani Dodoma

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habri, kuhusu tukio la vifo vya watu watatu, wanaodhaniwa kuwa ni majangili, waliouawa na wananchi katika kijiji cha Miganga, Mvumi Dodoma. Pembeni yake ni gari aina ya Noah lenye namba za usajili T 983 BZJ, walilokuwa wakilitumia na kukutwa na meno 73 ya Tembo. (Picha zote na John Banda)
Baadhi ya meno 73 ya Tembo, waliyokuwa nayo majangili hao kwenye gari lao hilo yakiwa mbele ya Kamanda Misime.

Na John Banda, Dodoma

MAJANGILI watatu wa nyara za Serikali, wameuawa kwa mishale yenye sumu na kisha miili yao kuchomwa moto na wananchi katika purukushani na polisi walipokuwa wakijaribu kukimbia ili kutorosha meno  ya tembo.

Tukio hilo lilitokea jioni ya Alhamis wiki hii katika kijiji cha Miganga, Kata ya Mvumi, wilayani Chamwino, mkoani Dodoma, ambapo miili yao ilikutwa ikiwa imeharibika kutokana na kuchomwa moto.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema kuwa majangili hayo, yaliuawa na wanachi wenye hasira kali kwa zana mbalimbali za kijadi, walipokuwa wanakimbilia porini ili kujiokoa na mkono wa polisi.

Misime alisema jeshi hilo, lilipokea taarifa kutoka kwa wananchi wema kuwa kulikuwa na gari, likitokea Manda likiwa na meno ya Tembo na kisha kuweka mtego katika kijiji cha Mwitikila ambapo waliona gari hilo, aina ya NOAH T 983 BZJ na kulisimamisha na Dereva wa gari hilo, alifanya kama anapunguza mwendo na kisha kuondoka kwa mwendo wa kasi.

‘’Polisi wakishirikiana na wananchi walianza kulifukuza, walipofika kijiji cha Miganga Mvumi, Polisi walifanikiwa kupiga risasi tairi moja ya kushoto na hivyo watu watatu waliokuwemo ndani gari hilo, waliruka na kutawanyika, wananchi waliojichukulia sheria mkononi waliwashambulia kiasi cha kupoteza maisha yao’’, alisema.

Aidha, Kamanda Misime, alisema baada ya kulipekua gari hilo, walikuta meno 73 ya Tembo, yenye uzito wa kilo 255.9, yakiwa na thamani ya zaidi ya Tsh. 225 mil. pamoja na hati ya mashitaka (Charge Sheet), ambayo ni kesi ya kuhujumu uchumi namba 4/2012, iliyokuwa imefunguliwa katika Mahakama ya Mpanda, mkoani Katavi na leseni ya udereva namba 4000692535 ya Aboubakar Peter, huku wakihisi ni mmoja ya waliouawa.

Alisema kuwa walikuwa wameshitakiwa kwa kosa la kupatikana na meno 3 ya Tembo, tarehe 17.06.2012 na Maofisa wa wanyama pori  katika eneo la Msaginya, Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi.

Majina ya waliokuwa wameshatakiwa ni pamoja na Joseph Marius (Ngondo) 59, mkazi wa maili mbili Dodoma, Aboubakar Mhina 25, mkazi wa Mkuhungu Dodoma, Msafiri Milawa 36, mkazi wa Nkuhungu, Dodoma na Petro Mtipula 55, mkazi wa Mpanda.

Kamanda Misime, alitoa wito kwa wananchi wasijichukulie Sheria mikononi, kwani kwa kufanya hivyo ni kupoteza ushahidi na inawawia vigumu Polisi kupata mitandao, inayohusika na matukio kama hayo.

No comments:

Post a Comment