Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete, akitoa hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Januari. |
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, akitoa hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Januari.
|
Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete, akifafanua jambo wakati alipokuwa akitoa hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Januari.
|
Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada naomba tuanze kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye Rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuzungumza
kwa mara nyingine kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri wa mawasiliano baina ya
Rais na wananchi wa Tanzania kila mwisho wa mwezi. Siku ya leo nitazungumzia safari yangu ya Ufaransa, Uswizi
na Ethiopia. Pia nitazungumzia ujenzi
wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Safari za Kikazi
Nje ya Nchi
Ndugu Wananchi;
Safari yangu
ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia ilikuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu. Nchini Ufaransa licha ya kuimarisha uhusiano
wa kirafiki baina ya nchi zetu, tumepata wawekezaji wengi wakubwa wenye nia
thabiti ya kuja kuwekeza hapa nchini.
Pia tumekubaliana kuanza mazungumzo ya kuwa na mpango mwingine wa
ushirikiano. Mpango wetu wa sasa
ulioanza mwaka 2006 uliisha mwaka 2010.
Mpango ule ulitusaidia sana kuboresha huduma za maji katika miji ya
Utete mkoani Pwani na Mpwapwa mkoani Dodoma.
Katika
mkutano wa Kongamano la Uchumi wa Dunia uliofanyika Davos, Uswizi,
tumehakikishiwa ushirikiano katika kuendeleza juhudi zetu za kuleta mapinduzi
ya kijani ili tujihakikishie usalama wa chakula na kupunguza umaskini vijijini
na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Aidha, tulipata bahati ya kushirikishwa katika mjadala wa kuanzishwa kwa
programu kubwa ya kuzisaidia nchi za Afrika kutatua matatizo ya upatikanaji wa
umeme. Naamini programu hiyo
ikitekelezwa na wakubwa kuheshimu kauli na ahadi zao itakuwa msaada mkubwa kwa
maendeleo ya nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ndugu Wananchi;
Nchini
Ethiopia tulishiriki katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa
Afrika na katika kikao cha African Peer Review Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya
tathmini ya utawala bora ya Tanzania na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa. Kwa jumla hatuna mahali tuliponyooshewa
kidole kuwa tunafanya vibaya. Tumepongezwa
katika mambo mengi na tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo waliyoona hatuna
budi kuyaboresha. Nilipata nafasi
ya kusema ambayo niliitumia kufafanua baadhi ya mambo yaliyokuwamo kwenye
taarifa. Niliwashukuru na kuahidi
kuufanyia kazi ushauri uliotolewa.
Tathmini ya nchi yetu ilipitishwa kwa kauli moja.
Vurugu za Kupinga Gesi Kusafirishwa
Kutoka Mtwara
Ndugu wananchi;
Kama mtakavyokumbuka tarehe 8 Novemba,
2012 kule Kinyerezi, Wilaya ya Ilala hapa Dar es Salaam, niliweka jiwe la
msingi la ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara na Songosongo
kuja Dar es Salaam. Karibu na mwishoni
mwa Desemba, 2012 kukafanyika maandamano mjini Mtwara kupinga ujenzi wa bomba
hilo. Katika maandamano yale na
baadaye kwenye kauli za wanasiasa na wanaharakati yakatolewa madai kuwa gesi
hiyo itumike kwa maendeleo ya Mtwara na kwamba yale yanayotakiwa kufanyika Dar
es Salaam yafanyike Mtwara. Pia, zilitolewa
shutuma nyingine dhidi ya Serikali eti kuwa kwa miaka mingi imewasahau na
haiwajali wananchi wa Mikoa ya Kusini na ujenzi wa bomba hilo ni muendelezo wa
hayo. Kauli mbalimbali za wanasiasa na wanaharakati ni kama vile ziliongeza
mafuta kwenye kaa la moto na kuuchochea mpaka kukatokea matukio
yaliyotusikitisha na kutshtua sote.
Baadhi ya ndugu zetu wamepoteza maisha na mali za watu na Serikali kuharibiwa.
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya kuaga mwaka 2012
na kuukaribisha mwaka 2013, tarehe 31 Desemba, 2012, nililisemea jambo
hili. Leo mwezi mmoja baadae,
napenda kusisitiza mambo mawili.
Kwanza kwamba, si kweli kuwa Serikali inapuuza Mikoa ya Kusini. Na pili, kwamba kujenga bomba la kuipeleka
gesi Dar es Salaam hakuinyimi Mikoa ya Mtwara na Lindi fursa ya kunufaika na
gesi iliyopo Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Serikali
imefanya, inafanya na ina mipango ya kufanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya
kuleta maendeleo katika Mikoa ya Mtwara na Lindi. Ipo mipango ya kuboresha miundombinu, huduma za kiuchumi na
kijamii pamoja na kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vikubwa na
vidogo. Serikali ya Awamu ya Tatu
chini ya uongozi wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ilijenga daraja katika
Mto Rufiji maarufu kama Daraja la Mkapa.
Hii ilikuwa ni hatua kubwa ya awali katika safari ya kutatua matatizo ya
usafiri ya Mikoa ya Kusini. Serikali
ninayoiongoza mie iliachiwa kazi ya kukamilisha ujenzi wa barabara za lami
kufikia darajani na kuunanisha Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Ruvuma. Kazi hiyo, tumeitekeleza vizuri na sasa
tunakaribia kuimaliza.
Tulikamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Mnazi-Mmoja hadi
Nangurukuru. Mwaka 2009 tukaanza
ujenzi wa barabara ya kilomita 56 kutoka Somanga hadi Ndundu (darajani). Ujenzi wa kilometa 36 za mwanzo
ulienda vizuri. Bahati mbaya
ujenzi wa kilomieta 20 za mwisho umechelewa sana kwa sababu ya mmiliki
wa kampuni iliyokabidhiwa kufanya kazi hiyo kufariki. Kwa sababu hiyo, kampuni ilipata mtikisiko kiasi na
kusababisha kazi kutotekelezwa kwa kasi tuliyoitarajia. Sasa mambo yametengemaa na kazi
inaendelea kwa kasi nzuri.
Matumaini yetu ni kuwa ifikapo mwezi Desemba, 2013 kazi hiyo itakuwa
imekamilika.
Hali kadhalika, Rais Mstaafu, Mzee
Benjamin Mkapa alituachia jukumu la kumaliza ujenzi wa Daraja la Umoja katika
mto Ruvuma na ujenzi wa barabara ya lami kuanzia Mikoa ya Mtwara na Ruvuma. Tumelikamilisha Daraja hilo na ujenzi
wa barabara ya lami kutoka Masasi hadi Mangaka umekamilika. Mchakato wa kujenga barabara ya kwenda
Songea na kwenda Darajani umefikia
mahala pazuri. Tenda ya ujenzi
wa barabara kutoka Tunduru hadi Mangaka mpaka Darajani imeshatangazwa. Kama mambo yataenda sawa miezi mitatu
ijayo mjenzi atapatikana. Wakati
huo huo ujenzi wa barabara kutoka Namtumbo hadi Songea – Mbinga na Namtumbo –
Tunduru unaendelea. Hivyo basi, kwa
barabara ya “Mtwara Corridor” kazi iliyobaki ni kutoka Mbinga kwenda Mbambabay ambayo
tutaifanya wenyewe kama tulivyofanya kwa Mnazi Mmoja – Nangurukuru na Somanga –
Ndudu na Daraja la Umoja.
Ndugu Wananchi;
Ipo pia mipango ya kuipanua na kuijenga
upya bandari ya Mtwara ili iweze kuhudumia mahitaji ya utafutaji na uchimbaji
wa gesi baharini, kuhudumia na kuvifanyia matengenezo vyombo vinavyotumika
katika utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi. Pia iweze kuhudumia shughuli za kiuchumi zitakazotokana na
uchumi wa gesi pamoja na zilizopo sasa. Nilipozungumza na makampuni ya utafutaji gesi pale Mtwara
tarehe 25 Julai, 2011 waliomba nikubali bandari ya Mtwara iwe mahali pa
kuhudumia vyombo vyote vinavyofanya shughuli ya utafutaji na uchimbaji wa gesi
na mafuta katika pwani ya Afrika ya Bahari Kuu ya Hindi. Pia waliomba kuwa sehemu hiyo ya bandari
iwe bandari huru. Niliwakubalia
bila ya kusita na tayari eneo la hekta 110 zimeshatengwa na
kutangazwa rasmi kuwa bandari huru.
Vile vile waliomba wapewe sehemu ya bandari ya sasa kuendeshea shughuli
na eneo la kujenga kituo cha mitambo ya kuchakata gesi na kusafirisha nje.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kuzungumza na makampuni ya utafutaji
gesi na mafuta na kuelezwa mahitaji yao nilibaini kuwa bandari ya Mtwara
inahitaji kupanuliwa na kujengwa upya.
Bahati nzuri viongozi wa Mamlaka ya Bandari walikuwepo na
walinihakikishia kuwa watafanya hivyo.
Tayari eneo la bandari limeongezwa
kutoka hekta 70.68 hadi 2,693.68. Eneo la bandari huru limeshatengwa hivyo
hivyo na eneo la kampuni ya Dangote na makampuni ya gesi yaliyopo. Aidha, mchakato wa kupanua bandari
iliyopo, kujenga gati mpya na kuendelea na ujenzi hadi maeneo ya Msanga Mkuu
ipo katika hatua mbalimbali za matayarisho na utekelezaji.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa Mkoa wa Lindi mipango ya kupanua na kuijenga upya bandari ya Lindi
imefikia hatua nzuri. Naibu Waziri
wa Uchukuzi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba alithibitisha hayo tarehe 1 Desemba, 2012
nilipotembelea bandari hiyo wakati wa ziara yangu ya Mkoa wa Lindi ya tarehe 1 mpaka
5 Desemba, 2012. Hali kadhalika
mipango ya kujenga bandari ya Kilwa iko mbioni. Tena kwa upande wa Mkoa wa Lindi moja ya makampuni
yaliyogundua gesi baharini wameamua kujenga bandari na kituo cha kuchakata na
kusarifisha gesi nje ya mkoa huo kama ilivyo kwa Mtwara. Naambiwa wametambua maeneo matatu,
kilichobakia ni kuamua mojawapo ili ujenzi uanze.
Ndugu Wananchi;
Nilipotoka
bandari ya Mtwara, siku ile nilitembelea Chuo cha VETA na kuzungumza na
viongozi wa VETA taifa na wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu kuwa
na mitaala ya kutoa mafunzo mahsusi yanayohitajika na sekta ya gesi na
mafuta. Nilisisitiza kwamba tuwapatie
vijana wetu mafunzo yatakayowawezsha kuajiriwa na makampuni ya gesi na yale
yatakayokuwa yanatoa huduma kwa makampuni hayo. Nilisema tusipofanya hivyo, makampuni hayo yataajiri watu
kutoka nje na hatutakuwa na sababu ya kuwalaumu wala kulalamika.
Nafurahi kwamba agizo langu hilo
limefanyiwa kazi ipasavyo. Hivi
sasa katika chuo cha VETA Mtwara mafunzo hayo yanatolewa. Kampuni ya PetroBrass ya Brazil
inaendesha mafunzo ya sekta ya gesi kwa vijana 25 kutoka mkoani Mtwara. Aidha, chuo cha VETA kwa kushirikiana
na Kampuni ya Gesi ya Uingereza (British Gas) na Volunteers Service Overseas ya
Uingereza, kinatekeleza programu ya miaka mitatu iitwayo Enhancing
Employerbility Through Vocational Training. Programu hii inalenga kutoa kozi zitakazowafanya wahitimu
kuweza kuajiriwa katika sekta ya gesi.
Programu hii ilifunguliwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed
Gharib Bilal, tarehe 26 Novemba, 2012.
Ndugu Wananchi;
Chini ya programu hii, walimu wa masomo
yanayohusiana na gesi wanaongezewa ujuzi ili waweze kufikia viwango vya
kimataifa. Vile vile, Wizara ya
Nishati na Madini imetoa upendeleo maalum wa kudhamini wanafunzi 50 kutoka mkoa
wa Mtwara kusoma chuoni hapo ambao tayari wameshahitimu mafunzo ya msingi ya
uunganishaji vyuma viwandani.
Mchakato wa kuwapata wanafunzi 50 kwa ajili ya mafunzo kama
hayo kutoka mkoa wa Lindi unaendelea.
Nimeambiwa mpaka wameshawapata vijana 25 bado 25.
Hali
kadhalika, Wizara ya Nishati na Madini inadhamini wanafunzi 10 kupata mafunzo katika
Chuo Kikuu cha Dodoma ambako kozi za mafuta na gesi zinatolewa. Kipaumbele kwa udhamini huu unatolewa
kwa wanafunzi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wenye sifa za kudahiliwa katika
mafunzo haya. Wamepatikana
watatu. Wataalamu hawa na wengine wa
fani mbalimbali za gesi na mafuta watafundishwa kwa kiwango cha shahada ya
kwanza na baadae uzamili na uzamivu ili nchi yetu ijitosheleze kwa wataalamu wa
sekta hii.
Kupanga Mji wa Mtwara
Ndugu Wananchi;
Baada
ya kutembelea bandari ya Mtwara na Chuo cha VETA, nilikaa na kuzungumza na
viongozi wa Serikali na Manispaa ya Mtwara. Katika mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu wa kuwa
na mpango kabambe wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan) Mpango ambao
utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji wa uchumi wa
gesi. Niliwataka wahakikishe kuwa
kuna maeneo ya viwanda, biashara, makazi, mahoteli, huduma za afya, elimu,
mapumziko na burudani, viwanja vya michezo na kadhalika. Kazi ya kutayarisha Masterplan hiyo imeanza
na Manispaa ya Mtwara inashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi.
Kwa upande wa uwekezaji nafahamu kuwa
mpaka sasa makampuni 51 yameonyesha nia ya kuwekeza Mtwara katika
viwanda, hoteli, shughuli za uchukuzi na huduma hasa kwa sekta ya gesi. Wanachosubiri ni kutengewa maeneo ya
kujenga, waanze. Hivyo kukamilika mapema
kwa Masterplan ya mji wa Mtwara kutasaidia kuongeza kasi ya uwekezaji
huu kufanyika. Viwanda hivi vyote
vitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Mtwara na Watanzania kwa jumla. Nimeambiwa kwa mfano, wakati wa ujenzi
wa kiwanda cha saruji watu zaidi ya 7,000 wataajiriwa.
Ndugu Wananchi;
Kabla hata ya
ugunduzi wa gesi iliyoko baharini, tulikuwa na mipango ya kutumia gesi ya
Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kuzalisha mbolea na kutumika
katika kiwanda cha saruji. Kwa
upande wa umeme kulikuwa na mpango wa kujenga mtambo wa kuzalisha Megawati
300
kwa kushirikiana na mwekezaji binafsi.
Bahati mbaya wakati wa matatizo ya kifedha ya dunia mwaka 2009 mwekezaji
huyo akashindwa kupata mkopo, hivyo mradi ukasimama kutekelezwa. Haukufa wala haukuhamishiwa Dar es
Salaam au Bagamoyo kama ambavyo imekuwa inapotoshwa kwa makusudi. Mradi huo bado upo, tena mpango wa sasa
ni kujenga Megawati 600 zitumike Mtwara na zingine kuziingiza kwenye
gridi ya taifa kupitia Songea.
NduguWananchi;
Kwa upande wa kiwanda cha mbolea,
wawekezaji wengi wameshajitokeza tangu mwaka 2008 mpaka sasa. Mchakato umefanyika wa kuchambua
wawekezaji wenye sifa na kutambuliwa.
Mambo mawili yamechelewesha utekelezaji kuanza. Jambo la kwanza ni wawekezaji na
kampuni ya Artumas iliyokuwa mbia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(T.P.D.C) wakati ule, kushindwa kukubaliana nao juu ya bei ya kuwauzia
gesi. Wawekezaji walitaka bei ya
gesi ipunguzwe, lakini kampuni ya Artumas na T.P.D.C. hawakuwa tayari kupunguza
zaidi ya kiasi walichopunguza, ambacho wawekezaji bado waliona hailipi kwa
kuzalisha mbolea.
Sababu ya pili ni matatizo ya kifedha yaliyoikumba kampuni ya
Artumas katika kipindi hicho. Kufuatia
machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa uchumi wa dunia mwaka 2008/2009 kampuni
ya Artumas iliathirika na kulazimika kuuza hisa zake kwa wawekezaji
wengine. Katika kipindi hicho ilichopitia
kampuni, mazungumzo na uwekezaji wa kiwanda cha mbolea hayakuweza kupewa kipaumbele. Mtazamo wa sasa wa wabia wapya na T.P.D.C.
ni kuwa wao wenyewe sasa wawekeze katika ujenzi wa kiwanda cha mbolea. Serikali
imekubali rai yao hiyo na wanaendelea na matayarisho.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa
kiwanda cha Saruji kitakachojengwa na kampuni ya Dangote ucheleweshaji ulikuwa kwa
sababu mbili. Kwanza, kampuni ya
Dangote iliomba eneo zaidi ya ililokuwa imeomba na kupewa. Hoja yao ilikuwa kwamba eneo la ziada
walilokuwa wanaliomba ndilo lenye malighafi nyingi na bora kwa utengenezaji wa
saruji. Hivyo, waliamua kusubiri
mpaka watakapopewa eneo hilo.
Bahati mbaya eneo hilo lilikuwa
linamilikiwa na mtu mwingine na alikuwa na hati miliki nalo. Halmashauri ya Mtwara iliomba Serikali
eneo hilo litwaliwe na baadaye ipewe kampuni ya Dangote. Serikali
ilikubali. Hata hivyo, mchakato
ulichukua muda na hata pale ulipokamilika mwenye eneo aliupinga uamuzi wa
Serikali Mahakamani. Kesi ilichukua
muda kusikilizwa na kumalizika. Bahati
nzuri Serikali ikashinda na mara baada ya uamuzi wa Mahakama ndipo kampuni ya
Dangote ikamilikishwa eneo hilo.
Kampuni nayo ilichukua muda
kuanza. Hivi sasa, timu yake ipo kwenye
eneo na mradi uko tayari kuanza kutekelezwa. Niliambiwa kuwa katika magari yaliyopigwa mawe katika fujo
za Mtwara ni pamoja na lile la mradi huu.
Huo ndiyo ukweli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote. Madai kuwa kiwanda hicho kimehamishiwa
Bagamoyo si ya kweli. Ni uzushi wa makusudi wa watu wenye nia
mbaya na Serikali. Huwezi kudai
kuwa mtetezi wa wananchi wa Mtwara kwa hoja za uongo na kufanya upotoshaji wa
makusudi kabisa.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa
bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu. Zilijengwa hisia kuwa gesi yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba
Mtwara itakosa gesi na maendeleo yatayotokana na gesi hiyo. Na, wengine wakasema gesi inapalekwa
Bagamoyo ili kuzidisha chumvi na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya
Serikali kwamba Rais anapeleka gesi kwao. Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo
Bagamoyo. Pili, ukweli ni kwamba
pale Mtwara kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji ya Mtwara, Lindi na Dar es
Salaam na kubaki. Gesi
itakayoletwa Dar es Salaam ni asilimia 16 tu ya gesi yote
iliyoko Mtwara kwa miaka ishirini ijayo.
Hivyo asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara kwa ajili ya kuuzwa
nje ya nchi na kupelekwa kwingineko nchini.
Kwa
sababu hiyo, ndugu zetu wa Mtwara hawana sababu ya kuwa na wasiwasi. Ipo gesi
ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na ya miaka mingi ijayo. Viwanda vinavyotumia gesi kama mali
ghafi na vile vinavyohitaji gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya
kutosha. Kwa upande wa uzalishaji
umeme hali kadhalika ipo gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi. Hivi sasa tunacho kituo kinachozalisha
umeme wa megawati 15 unaotumika Mtwara, Lindi, Tandahimba, Newala,
Masasi, Nachingwea, Ruangwa, na Mtama. Bado umeme huo hautumiki wote hivi sasa.
Ndugu Wananchi;
Nayaeleza yote
haya kuwathibitishia wananchi wa Mtwara kuwa tunawathamini sana na kuwajali. Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuwapuuza
na kuwatupa mkono wananchi wa Mikoa ya Kusini. Aidha, sitakuwa tayari kuwaruhusu watu au mtu ye yote
Serikalini kuwapuuza wananchi wa Mikoa ya Kusini au mkoa wo wote hapa
nchini. Hiyo haitakuwa sawa. Nilishasema siku za nyuma na napenda
kurudia tena leo kuwa kwangu mimi hakuna mkoa ulio bora kuliko mwingine. Ni kutokana na msimamo wangu huo ndiyo
maana tumeelekeza nguvu na rasilimali nyingi za Serikali katika mikoa iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa. Kazi ya ujenzi wa barabara za lami iliyofanyika
na inayoendelea kufanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma
na Kagera inajieleza yenyewe. Mipango ya kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Mtwara
kufikia hadhi ya kimataifa na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Lindi na
Kilwa ni ushahidi mwingine kati ya mambo mengi tunayoweza kuyataja.
Ndugu Wananchi;
Haya
niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya yale yaliyofafanuliwa na kuelezwa kwa kina
na Mawaziri na Wakuu wa Idara husika
za Serikali na Mashirika ya
Umma pale Mtwara katika mkutano wa Waziri Mkuu na viongozi wa Serikali, dini,
vyama vya siasa na wazee wa Mkoa wa Mtwara tarehe 29 Januari, 2013.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa
pongezi nyingi kwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa kazi kubwa na
nzuri aliyoifanya kule Mtwara.
Uvumilivu wake, usikivu wake na utulivu wake vimesaidia sana kulivusha taifa
katika moja ya mitihani mikubwa ambayo ingeikuta nchi yetu tangu Uhuru. Nawapongeza Mawaziri na Wakuu wa
Mashirika ya Umma na Idara za Serikali kwa mchango wao muhimu walioutoa,
uliosaidia kufafanua masuala ambayo yalikuwa hayaeleweki vizuri. Kwa wao nawasisitiza na kuwakumbusha
wajibu wao wa kuelimisha jamii kuhusu shughuli wazifanyazo. Wakifanya hivyo mara kwa mara migongano
haitakuwepo na wapotoshaji hawatapata nafasi.
Ndugu Wananchi;
Nitakuwa mwizi
wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, madhehebu
ya dini, viongozi wa jamii, wazee, wana-Mtwara na makundi mbalimbali ya jamii, kwa
muda waliotumia kuzungumza na Waziri Mkuu na kuwasikiliza wasaidizi wake
wakifafanua masuala mbalimbali.
Uvumilivu wao na uelewa wao ndivyo vilivyosaidia kurejesha hali kuwa ya
kawaida. Nawaomba nao sasa, wote
kwa pamoja washirikiane na Serikali kuelimisha umma kuhusu ukweli wa mambo. Pia watumie nafasi hiyo kutahadharisha jamii
na kuwataka watu kuwa waangalifu na kupima maneno wanayoambiwa na watu. Wajiepushe na maneno au vitendo vinavyofarakanisha,
kuchonganisha na kupandikiza chuki dhidi ya watu au Serikali. Waambieni kuwa
ghasia hukimbiza wawekezaji kwani wakipata hofu kuwa hali ya amani na usalama
ni ya mashaka, watatoka kwenda kuwekeza kwingine. Vyema iwe hapa hapa nchini, lakini wanaweza kwenda nchi
nyingine na sisi kupoteza kabisa.
Ndugu Wananchi;
Nawapa
pole wananchi wa Mtwara na Masasi kwa usumbufu walioupata kutokana na ghasia
zilizofanywa. Nawapa pole
waliofiwa na kujeruhiwa. Nawapa
pole waliopoteza au kuharibiwa mali zao.
Kwa kweli inasikitisha na kufadhaisha kuona watu wanafanya vitendo vya kuua,
kuchoma moto nyumba za watu na majengo ya Serikali pamoja na , kuharibu na
kuiba mali za watu. Huu ni uhalifu
ambao hauna maelezo na haukubaliki.
Tunaviachia vyombo husika vya dola na sheria kutimiza wajibu wao. Kwa waliohusika iwe fundisho kwao na
kwa wengineo kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu wengine siku zijazo. Sasa wameachwa pekee yao wakati wenzao
wako huru na kufaidi maisha
Ndugu Wananchi;
Hili sakata la bomba la gesi limefika
mahali pazuri. Yaliyopita si
ndwele tugange yajayo.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni Sana kwa Kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment