TANGAZO


Sunday, December 30, 2012

Ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Handeni na Kilindi mkoani Tanga

Katibu Mkuu wa Cha cha Wananchi (CUF),  ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na watoto na wananchi mbalimbali, wakati alipofika wilayani Kilindi, Tanga kwa ajili ya kuhutubia mkutano wa hadhara wa Chama hicho.

Watoto na vijana mbalimbali wa Wilaya ya Kilindi, Tanga wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa CUF,   ambaye  pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Wilayani humo.

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad,  ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho, katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Handeni sokoni Mkoani Tanga.

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad,  ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho, katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Handeni sokoni Mkoani Tanga.


Wananchi mbalimbali wa Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa CUF,  ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar,  Maalim Seif Sharif Hamad wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Handeni Sokoni. (Picha zote na Salmin Said, OMKR)


Na Hassan Hamad (OMKR)

Handeni, TANGA                                                     30/12/2012.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema sekta za elimu na kilimo bado hazijapewa umuhimu unaostahiki katika kumkomboa Mtanzania kiuchumi.

Amesema elimu inayotolewa hasa katika shule za vijijini bado ni duni na kwamba shule hizo zimekuwa zikikabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu pamoja na vifaa vya kufundishia.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya za Kilindi na Handeni Mkoani Tanga leo katika mikutano ya hadhara iliyoandaliwa na Chama hicho kwa nyakati tofauti, Maalim Seif amesema wananchi hao wa vijijini pia wamekuwa wakisumbuliwa na ada kubwa ya shule kulinganisha na uwezo wa kipato chao.

Ameishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuangalia uwezekano wa kuzisaidia shule hizo kwa kuzipatia walimu na vifaa vya kufundishia, ili wanafunzi hao wapate elimu sawa na wale walioko maeneo mijini.

Akizungumzia kuhusu kilimo, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar  amesema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na bajeti ndogo ya kuendeleza sekta hiyo.

Amezitaja changamoto nyengine kuwa ni pamoja na elimu duni ya kilimo kwa wakulima, bei kubwa za pembejeo za kilimo pamoja na ukosefu wa soko kwa bidhaa mbali mbali zinazozalishwa na wakulima wazalendo.

Amesema iwapo serikali itaweka mkazo katika sekta hiyo na kuwawezesha wakulima kumudu gharama za uzalishaji, wananchi wengi wataweza kujikomboa kutokana na kilimo ambacho kitawaletea tija.

Amesema Zanzibar kupitia serikali ya umoja wa kitaifa imeshaanza kuona umuhimu wa kuwawezesha wakulima, baada ya kuamua kupunguza bei ya pembejeo za kilimo na gharama za kulimia, na kwamba sasa mahitaji ya pembejeo za kilimo yamekuwa makubwa kwa vile wananchi wengi wanaweza kumudu gharama hizo, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Amefahamisha kuwa iwapo chama hicho kitapata ridhaa ya kuongoza nchi kitaweka mkazo zaidi katika sekta za elimu na kilimo ili kuleta ukombozi wa kweli wa kiuchumi kwa Watanzania.

Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, ameeleza hatua ya Zanzibar kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwa ni yenye mafanikio na ya kupongezwa duniani kote.

Amesema faida za kuwepo kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ni nyingi ikilinganishwa na hasara zake, na kwamba hatua hiyo imeonesha ukomavu wa kisiasa na kukuwa kwa demokrasia visiwani Zanzibar.

Wakati huo huo Chama Cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimepata pigo jengine baada ya wanachama wake 120, wakiongozwa na Katibu wa Vijana wa Chama hicho, wilayani Handeni, Rajab Abdallah Shiza, kujiengua na kujiunga na CUF.

Akizungumza katika mkutano huo, Shiza amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa ndani ya Chama hicho kuna ubabaishaji ikiwa ni pamoja na kuwadanganya na kuwatapeli wananchi wa maeneo mbali mbali.

“Walikuja hapa viongozi wetu wa ADC wakatuambia kuwa watatupatia mikopo ili tuweze kuendesha miradi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya ushirika, lakini hadi leo baada ya kupata usajili hatujaona mkopo wala taarifa yoyote inayohusiana na mikopo” alifahamisha Shiza.

Katika mikutano mitatu tofauti aliyofanya Mkoani Tanga, Maalim Seif aliwasisitiza wananchi kupima sera za vyama, ili kufanya maamuzi sahihi wakati wanapochagua viongozi wa kuwaongoza.

No comments:

Post a Comment