Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo, Anicetus Mwesa (kushoto), akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki nakala ya gazeti la matangazo la Dar Metro, linalotolewa na Kampuni ya Jambo Concepts, Dar es Salaam leo. Gazeti la Dar Metro hutoka mara mbili kwa wiki na hugawiwa bure kwa wasomaji. (Picha na Dotto Mwaibale)
VYOMBO vya habari nchini, vimetakiwa kuutangaza utalii uliopo katika jiji la Dar es Salaam ili kutoa fursa kwa wageni kufahamu vivutio vilivyomo ili waweze kuvitembelea.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alitoa mwito huo leo, ofisini kwake, mara baada ya kukabidhiwa gazeti jipya la Dar Metro ambalo ni mahususi katika kuutangaza utalii linalotolewa na Kampuni ya Jambo Concepts (T), ambao pia ndiyo wamiliki wa gazeti hili.
Ambapo alipongeza hatua iliyofikiwa na Kampuni ya Jambo Concepts (T) Ltd kwa kuliona jambo hilo na kuchukua hatua ya kuanzisha gazeti kwa ajili ya kuutangaza utalii uliopo Dar es Salaam.
"Nachukua fursa hii kuishukuru Kampuni ya Jambo Concepts na pia Juma Pinto kwa kuja na wazo hili la kuanzisha gazeti ambalo litakuwa mahususi kuutangaza utalii na shughuli nyingine katika Jiji la Dar es Salaam.
"Kimsingi ni kwamba Dar es Salaam ina vivutio vingi vya utalii, lakini havifahamiki kwa kuwa havijatangazwa sana na vyombo vya habari. Jambo ambalo linawafanya wageni wetu hasa watalii kwenda maeneo mengine hususan katika mbuga za Mikumi, Ngorongoro, Serengeti na kwingineko," alisema Sadiki.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, iwapo utalii wa Dar es Salaam utatangazwa vizuri utawafanya watalii wasitamani kwenda mbali kujionea mambo mbalimbali.
Ambapo alitolea mfano wa Zou ya Kigamboni na kubainisha kuwa ina kila aina ya wanyama ambao watalii ambao ni kivutio tosha kwa watalii wa ndani na wale wanaotoka nje ya nchi.
Sadiki alisema kuwa mbali na zou hiyo, Dar es Salaam kuna hoteli na fukwe nyingi ambazo zote ni sehemu ambazo ni maeneo muhimu katika shughuli za kitalii.
"Hongereni sana Jambo Concepts kwa kuja na wazo hili kwa ajili ya kuutangaza utalii mkoani kwetu, hivyo nachukua fursa hii kueleza kwamba sisi kama viongozi wa mkoa tupo pamoja nanyi. Pia naomba muongeze kopi zaidi ili ziweze kuwafikia watu wengi," alisema mkuu huyo wa mkoa.
Naye Mhariri Mkuu wa gazeti hili, Anicetus Mwesa akimkabidhi mkuu huyo wa mkoa gazeti la Dar Metro kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts (T) Ltd, Juma Pinto alisema kuwa gazeti hilo hutolewa bure kwa wananchi ili waweze kujisomea na kuutambua utalii uliopo Dar es Salaam.
Alisema kuwa kwa kuanza gazeti la Dar Metro limelenga kutangaza shughuli mbalimbali zilizopo katika Jiji la Dar es Salaam zikiwemo za utalii na za uchumi.
"Dar Metro limezinduliwa Desemba 4, mwaka huu, ambapo linatolewa bure kwa wananchi walioko Dar es Salaam ndiyo maana tumeona umuhimu wa kukufikishia hapa ofisini kwako wewe ukiwa kama kiongozi wa mkoa huu.
"Malengo ni kwamba kwa baadaye litasambazwa maeneo mengine ya nchi bure kama ambavyo tumeanza kwa Dar es Salaam. Linachapishwa katika lugha za Kiingereza na Kiswahili," alisema Mwesa.
No comments:
Post a Comment