Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Magazeti na Vijarida ambaye pia ni Mshauri wa Rais wa Zanzibar wa mambo ya Utalii, Issa Ahmed Othman, akitoa maelezo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk (hayupo pichani), kabla ya uzinduzi wa Bodi hiyo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Maelezo Zanzibar, Yussuf Omar Chunda.
Na Mwanaisha Muhammed, Maelezo Zanzibar
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, amesema kuwepo kwa magazeti mengi katika nchi kunasaidia sana kuharakisha harakati za Maendeleo.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, amesema kuwepo kwa magazeti mengi katika nchi kunasaidia sana kuharakisha harakati za Maendeleo.
Aliyasema hayo, huko ofisini kwake Kikwajuni, mjini Zanzibar leo, wakati alipokuwa akibadilishana mawazo na wajumbe wa Bodi ya Ushauri wa Magazeti na Vijarida visiwani Zanzibar.
Waziri alisema kwamba kwa sasa Zanzibar magazeti yaliyopo ni machache mno ukilinganisha na nchi nyengine kama Tanzania Bara, hivyo kutokuwepo kwa Magazeti mengi kunadumaza maendeleo.
Aliitaka bodi hiyo, kutokuwa wakali wakati wa kusajili magazeti hayo na daima wawe wanawafahamisha wenye magazeti pale wanapokosea na wasichoke ila tu wakiona mhusika hafahamishiki ndipo hatua za kisheria zichukuliwe.
Amesema kuwa jukumu kubwa kwa hivi sasa kwa bodi hiyo, ni kuhakikisha inasajili magazeti ya kutosha pamoja na vijarida kwa mujibu wa sheria na taratibu ziliopo, ili Zanzibar iweze kupiga hatua za maendeleo kwa kuwa na magazeti mengi kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Hata hivyo, Waziri alisema bodi ina kazi muhimu katika nchi kwa kuhakikisha kwamba magazeti yatakayo ruhusiwa yawe ni yenye uhakika na sio ya kubahatisha na kuleta mfarakano katika jamii.
Naye kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, ambaye pia ni Mshauri wa Rais wa masuala ya Utalii, Issa Ahmed Othman alisema kuwa madhumuni makubwa ya kuanzishwa kwa Bodi hiyo ni uangalizi wa magazeti na vijarida ili yasikiuke taratibu na sheria zilizowekwa .
Alisema kuwa kwa upande wa Bodi hiyo, huwa hawapitishi gazeti wala kijarida kama vigezo husika vya kisheria havijakidhi haja kama sheria ilivyoelekeza ili kuepusha migogoro kutotokea katika jami.
Mwenyekiti huyo, alisema kuwa bodi inaona choyo kwa Wazanzibari kutokuwa na magazeti mengi, hivyo inakaribisha kwa Watanzania kwa ujumla kuanzisha magazeti ili maendeleo yaweze kupatikana Zanzibar.
Alisema kuwa Serikali imeweka chombo cha kushughulikia vyombo vya Habari, sio kuwabana bali ni kuweka utaratibu ambao utasaidia utendaji mzuri wa kazi za waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment