TIMU ya Mtibwa Sugar imekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya leo asubuhi kwa kuizamisha African Lyon mabao 3-1.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, hadi mapumziko Mtibwa Sugar ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 22 na Hillary Kasela. Hassan Kabunda aliisawazishia African Lyon katika dakika ya 53.
Mabao mengine ya washindi yalifungwa na Godfrey Mohamed dakika ya 64 na Juma Lazio akapachika la mwisho dakika ya 87. Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar sasa itacheza mechi ya kwanza ya nusu fainali dhidi ya Azam ambayo nayo leo asubuhi iliilaza JKT Ruvu bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Chamazi.
Bao la Azam lilifungwa dakika ya 46 na Mudathiri Yahya.
Mechi hiyo ya kwanza ya nusu fainali itachezwa Ijumaa Desemba 21 saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. Nusu fainali ya pili nayo itachezwa kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 10 kamili jioni.
Hadi tunakwenda mitamboni, robo fainali ya tatu kati ya Oljoro JKT na Simba na robo fainali ya nne zinachezwa zilikuwa zikiendelea kupigwa kwenye viwanja vya Karume na Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi ya fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili Desemba 23 kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment