Treni za kisasa Kenya
Shirika la reli nchini Kenya limezindua treni mpya ambayo ina
mwendo wa kasi ili kutoa huduma kwa wakaazi wa viungani mwa mji wa Nairobi.
Ni treni ya kwanza ya aina yake kuzinduliwa tangu Kenya kujipatia uhuru mwaka
1963.Treni hiyo inanuiwa kupunguza msongamano wa magari mjini Nairobi ambao ni mojawapo ya miji unaokuwa kwa kasi barani Afrika ukiwa na watu zaidi ya milioni tatu.
Rais Kibaki aliyefungua rasmi kituo hicho, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuipanda treni hiyo.
Kituo cha treni cha Syokimau ni cha kwanza cha aina yake nchini Kenya, kikiwa na mashine za elektroniki zinazokagua vyeti vya usafiri, pamoja na skirini kubwa ambazo zinatangaza safari za treni.
Kila behewa lina uwezo wa kubeba abiria sabini pamoja na miamoja na ishirini watakao simama.
Huduma hiyo itakuwa ya kasi na bora zaidi ikilinganishwa na treni za hapo nyuma na pia zitatumia njia tofauti ya reli.
Safari ya kutoka mtaa wa Syokimau inachukua dakika kumi na tano kwa treni hizo huku ikiwa mtu atakwenda kwa gari itamchukua hata masaa mawili. Itamgharimu abiria shilingi miambili kwenda na kutoka mjini.
No comments:
Post a Comment