TANGAZO


Thursday, November 8, 2012

Rais mstaafu Benjamin Mkapa asisitiza kuheshimu masharti ya mikopo

Rais mstaafu wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Afrika Tanzania, Ammish Owusu-Amoah, wakati wa uzinduzi wa tawi la benki hiyo la Mtibwa, Morogoro jana.  Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Mtibwa Sugar Estate Ltd,  Seif Nassoro (wa pili kulia) na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo,  Jerome Harel.

Rais mstaafu wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa akizindua rasmi Benki ya Afrika Tanzania, tawi la Mtibwa, Morogoro jana.  Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Hassan Mtaka. 


Rais mstaafu wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa akiangalia jambo katika tawi jipya la Mtibwa la Benki ya Afrika Tanzania, wakati wa uzinduzi wa tawi hilo Morogoro jana.  Wengine katika picha ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Ammish Owusu-Amoah (kushoto) na wa pili ni Mwenyekiti wa Bodi wa benki hiyo, Balozi Fulgence Kazaura.

Na Mwandishi wetu, Morogoro
Wito umetolewa kwa watanzania kuwa na utamaduni wa kurejesha mikopo ili kuziwezesha benki kuongeza wateja kwa kuwapatia mikopo wateja wengine.
Wito huu umetolewa na Rais mstaafu, Mhe. Benjamin Mkapa alipokuwa akiongea wakati wa uzinduzi wa Benki ya Afrika Tanzania tawi la Mtibwa, Morogoro Jumatano wiki hii.
Tawi hilo linalokuwa la 17 la benki hiyo hapa nchini limefunguliwa katika eneo la Mtibwa Sugar Estates Ltd.
“Hakuna mkopo ambao ni wa bure,” alisema katika uzinduzi huo, na kuongeza kuwa mikopo yote ina riba na lazima kurejesha.
Alisema mtu anaeweza kuchukua mkopo na akaweza kuurejesha kwa wakati ataona faida na mabadiliko ya kasi katika biashara yoyote anayoifanya na pia kutoa picha nzuri ya kuaminika katika vyombo vya fedha.
“Ushauri wangu kwawananchi wote ni kwamba wale wanaopata mikopo kupitia benki wajue ni lazima kurejesha ili kuiwezesha benki kuongeza wateja kwa kuwapatia mikopo wateja wengine,” alisema.
Pia alisisitiza kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba na kujiweka katika mazingira ya kukopesheka ili kuweza kupanua shughuli za kiuchumi.
“Watu wenye hulka ya kujiwekea akiba wanakuwa na nafasi kubwa ya kuzitumia akiba zao katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo,” alisema.
Pamoja na kusifu uamuzi wa benki hiyo kufungua tawi hilo, aliitaka benki hiyo kuangalia uwezekano wa kuanzisha dirisha la mikopo midogo midogo katika mji wa Mtibwa ili kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi ambao katika mazingira ya kawaida ya kibenki inakuwa vigumu kukopesheka.
“Kwa utaratibu huo, benki itajiwekea fursa ya kuandaa na kuwapata wateja wakubwa wa baadaye pamoja na kuchangia shughuli za kiuchumi na kijamii,” alisisitiza.
Aliwakumbusha wananchi wa Mtibwa kuchangamkia fursa ya kuwa na benki hiyo katika eneo lao na kuitumia ipasavyo.
“Kikubwa zaidi ni kuhakikisha kuwa mnapanua wigo wa shughuli zenu za kiuchumi, biashara na kilimo,” alisema.
Pia alitoa wito kwa vikundi vya akiba na mikopo na taasisi mbalimbali hapa nchini kushiriki na kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa kutumia huduma za benki.
Alisema makampuni mbalimbali, vikundi vya uzalishaji mali, wafanya biashara ndogo ndogo na wadau wengine wana nafasi kubwa ya kushiriki katika kuliletea taifa maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Ammish Owusu-Amoah aliuita uamuzi wa kufungua tawi hilo kama wa kihistoria.
Alisema uzinduzi huo ni matokeo ya ushirikiano wa muda mrefu wa kibiashara kati ya benki hiyo na kiwanda cha Mtibwa.
“Uzinduzi wa tawi hili utazidi kudumisha ushirikiano kati yetu na kiwanda cha Mtibwa na jumuia nzima ya wakazi wa Mtibwa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha sukari cha Mtibwa, Bw. Jerome Harel alitoa shukrani kwa taasisi hiyo ya fedha kwa aumuzi wake kufungua tawi hilo na kusema kwamba hiyo itarahisisha upatikanaji wa huduma za mikopo.
“Benki ya Afrika Tanzania imefanikiwa kufanya kitu kilichoshinda benki nyingine kwa miaka mingi,” alisema.
Tangu ianze shughuli zake hapa nchini, benki hii imekua ikijitahidi kujitanua kwa kuanzisha huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufungua matawi mapya.  
Hadi sasa ina matawi kumi jijini Dar es Salaam pamoja na mengine sita katika mikoa ya Morogoro, Tunduma, Mwanza, Moshi, Mbeya na Arusha. 
Benki hii ni moja ya mtandao wa kibenki unaofanya kazi katika nchi 15 ambazo ni pamoja na Benin, Burkina Faso, Ghana, Ivory Coast, Mali, Niger na Senegal.  Nyingine ni Burundi, Djibouti, Kenya, Madagascar, Tanzania na Uganda.

Pia ina tawi katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

No comments:

Post a Comment