Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amahoro katika kijiji cha Mgaraganza, Wilaya ya Kigoma Vijijini jana.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mgaraganza Wilaya ya Kigoma Vijijini, kabla ya kukagua ujenzi wa Shule yao ya Sekondari ya Amahoro.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wafuasi na wapenzi wa Chama hicho, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kigoma mjini jana.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na wafuasi na wapenzi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kigoma mjini jana. (Picha zote na Hassan Hamad, OMKR)
Na Hassan Hamad, OMKR, Kigoma18/11/2012.
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema shule
nyingi za vijijini bado zinakabiliwa na upungufu wa walimu pamoja na vifaa vya kufundishia.
Amesema hali hiyo inapelekea kutolewa kwa elimu isiyo bora ambayo husababisha vijana wengi kushindwa kupata ajira baada ya kuhitimu masomo yao.
Maalim Seif ameeleza hayo katika ziara yake ya kutembelea ujenzi wa Shule ya
Sekondari ya Amahoro katika kijiji cha Mgaraganza Wilaya ya Kigoma Vijijini.
Amesema ili kuwajenga vijana kitaaluma ni lazima waandaliwe kwa kupatiwa elimu bora ambayo itaweza kuwasaidia katika maisha yao ya baadae.
Katika risala yao iliyosomwa na mjumbe wa kijiji hicho bwana Said Seif Wagara, wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia ili waweze kukamilisha jengo la utawala, ili hatimaye shule hiyo, iweze kufunguliwa na kuanza kazi.
Wakati huo huo Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF amehutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya Kigoma Mjini, na kuwashauri wale waliokihama chama hicho kurejea ili waweze kuongeza nguvu ya kutetea haki za wananchi.
Amewaambia wananchi wa Kigoma kuwa Chama cha CUF bado kipo na kinaendelea kuimarika katika maeneo mbali mbali ya Tanzania, hasa baada ya kuzinduliwa kwa operesheni mchakamchaka hadi mwaka 2015.
Amesema CUF ni chama chenye malengo ya kuwakomboa Watanzania kiuchumi,
kisiasa na kijamii na kuwaomba wananchi wa Kigoma kuendelea kukiunga mkono chama hicho ili kiweze kufikia malengo yake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba amewataka vijana wa Kigoma kusoma na kuifahamu historia ya nchi yao ili kujua malengo halisi ya kupigania uhuru kutoka kwa wakoloni.
Amesema Mikoa ya Magharibi ya Tanzania ikiwemo Tabora na Kigoma ilichukua nafasi kubwa katika kubigania uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, lakini bado imeachwa nyuma
kimaendeleo, na kuwataka vijana kuweka mikakati maalum ili waweze kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi katika mikoa hiyo.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya kiuchumi katika mikoa hiyo ya Magharibi, Prof. Lipumba ameelezea haja ya kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara na reli ili kurahisisha hughuli za kilimo na biashara.
Amesema iwapo miundombinu hiyo itakuwa imara, Mkoa wa Kigoma unaweza kuwa kituo kikukuu cha biashara na kuweza kuwaunganisha kibiashara wananchi wa Kigoma na
Kongo ya Mashariki yenye idadi ya watu wapatao milioni 30.
Amefahamisha kuwa Mkoa wa Kigoma una fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo jiografia ya mkoa huo, na kwamba iwapo zitatumika vizuri zinaweza kuwanufaisha wananchi wa eneo hilo na kuweza kuondokana na ukosefu wa ajira.
No comments:
Post a Comment