Meneja wa Benki ya KCB Tanzania, Tawi la Morogoro, Philip Jacob Pilla (kulia), akiteta jambo na washiriki wa semina ya Wajasiriamali na wafanyabiashara wakubwa iliyoandaliwa na benki hiyo ili kuwajengea uwezo wa kukua kibiashara iliyofanyika mjini Morogoro.
Na Mwandishi wetu Morogoro
BENKI ya KCB Tanzania imeendesha mafunzo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SME’s) mkoani Morogoro, ili kuwajengea uwezo wa kukuza na kuendesha biashara zao kuwa zenye tija na maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha washiriki ili kufungua fursa za kibiashara zilizopo miongoni.
Akifungua Semina hiyo Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa KCB Tanzania Christine Manyenye alisema, wajasiriamali wengi wamekuwa wakiendesha shughuli zao bila kuwa na elimu ya biashara, jambo linalopelekea kupoteza nguvu kazi zao bure.
Manyenye ameeleza kwamba, kupitia mafunzo hayo wajasiriamali hao wa mkoa wa Morogoro pia wataweza kuunda umoja wao utakaowawezesha kuaminika na kukopesheka na taasisi zingine za kifedha katika maeneo yanayowazunguka.
“Katika kurudisha kiasi cha faida tunachokipata kwa jamii, kipindi hiki tumeamua kuwajengea uwezo wajasiriamali wa mkoa huu Wadogo na wa Kati katika maeneo ambayo tunatoa huduma zetu. Kupitia mafunzo haya ni matarajio yetu watafungua fursa za kibiashara kupitia uzoefu na elimu waliyoipata,” alisema Manyenye.
Akitoa mada, Mwezeshaji wa Semina hiyo Peace Lumelezi amesema, mafunzo ya mara kwa mara kwa wafanyabiashara na wajasiriamali ni muhimu kwani yanawapa uwezo wa kutambua eneo linalofaa kwa biashara na wakati wa kuifanya.
Akifafanua zaidi, Lumelezi amesema, taasisi nyingi za kifedha zinahofia kuwakopesha Wajasiriamali hao, kwa kutokidhi vigezo vya mikopo mbalimbali na kubainisha kwamba dosari zingine zinachagiwa na uzoefu wa shughuli za kifedha.
Naye Meneja wa KCB Twi la Morogoro Phillip Jacob Pilla, ametoa wito kwa Wajasiriamali waliopatiwa mafunzo hayo kutoziachia fursa za kiuwekezaji zilizopo katika maeneo yao, kwani wao wana nafasi kubwa ya kufanya hivyo hasa katika shughuli za kilimo.
Mafunzo kama hayo pia yatapelekwa kwenye mikoa yote yenye matawi ya Benki ya KCB Tanzania, ikiwamo Zanzibar, Moshi, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam.

No comments:
Post a Comment