I UTANGULIZI
a) Masuala ya Jumla
1. Mheshimiwa Spika, ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Rehema zake kwa kutuwezesha kufikia siku ya leo tunapohitimisha shughuli zilizopangwa kufanyika katika Mkutano wa Tisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Katika kipindi tulichokuwa hapa takriban siku 11, wapo Waheshimiwa Wabunge ambao walipoteza Wapendwa wao, akiwemo Mheshimiwa John Momose Cheyo, Mbunge wa Bariadi Mashariki aliyepoteza Mtoto wake kwa kuzama majini pale Dar es Salaam. Tunampa Pole Sana! Aidha, tunawapa pole wote waliopoteza Wapendwa wao kutokana na sababu mbalimbali.
b) Maswali
3. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Tisa, jumla ya Maswali 119 ya Msingi na 293 ya Nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge. Maswali mengine 14 ya Msingi na 11 ya Nyongeza yaliulizwa kwa utaratibu wa Maswali kwa Waziri Mkuu kila Alhamisi.
c) Miswada
4. Katika Mkutano huu Miswada ya Serikali ifuatayo ilisomwa na kujadiliwa:
i) Muswada wa Sheria ya Haki za Wagunduzi wa Mbegu za Mimea wa Mwaka 2012 [The Plant Breeders Rights Act, 2012]; na
ii) Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2012 [The Written Laws Miscellaneous Amendments (No.3) Act, 2012].
d) Maazimio
5. Mheshimiwa Spika, aidha, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kujadili na kupitisha Maazimio yafuatayo:
i) Azimio la Bunge la Kuridhia Marekebisho ya Pili ya Mkataba wa Ushirikiano kati ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya pamoja na Nchi Wanachama wa Umoja wa Nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki [Cotonuo Partnership Agreement].
ii) Azimio la Bunge la Kuridhia Kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane;
iii) Azimio la Bunge la Kuridhia Marekebisho ya Mpaka na Upanuzi wa Hifadhi ya Taifa Gombe;
iv) Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Uanzishwaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki [The Protocal on the Establishment of the East African Kiswahili Commission];
v) Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba Mpya wa Umoja wa Posta Afrika, 2009 [The Convention of the Pan African Postal Union (PAPU) of 2009]; na
vi) Azimio la Bunge la Kuridhia Katiba na Mkataba wa Mawasiliano Afrika, wa Mwaka 1999 [Constitution and Convention of the African Telecommunications Union (ATU) of 1999].
e) Kauli za Serikali
6. Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilipokea Kauli ya Serikali kutoka kwa Mawaziri kuhusu masuala yafuatayo:
i) Fao la Kujitoa (Withdrawal Benefit) toka kwa Waziri wa Kazi na Ajira;
ii) Viwango vya Chakula cha Wafungwa Magerezani kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi;
iii) Tatizo la Utengenezaji wa Dawa Bandia ya Kupunguza Makali ya UKIMWI kutoka kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
iv) Mpango Maalum wa Serikali wa Kutatua Tatizo la Maji katika Jiji la Dar es Salaam kutoka kwa Waziri wa Maji; na
v) Tatizo la Mafuta Nchini kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini.
f) Hoja Binafsi
7. Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, Bunge lako Tukufu lilipokea na kujadili Hoja Binafsi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge.
II UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA ROBO YA KWANZA YA MWAKA 2012/2013
8. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba katika Bunge la Bajeti tulipitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/2013 ya jumla ya Shilingi Trilioni 15.19. Kati ya fedha hizo, Fedha za Matumizi ya Kawaida ni Shilingi Trilioni 10.60 na Fedha za Matumizi ya Maendeleo Shilingi Trilioni 4.59. Katika kutekeleza Bajeti hiyo, Serikali ilikadiria kukusanya Mapato ya Ndani kiasi cha Shilingi Bilioni 8,714.7 (bila kujumuisha mapato ya Serikali za Mitaa) kwenye robo ya kwanza, ikiwa ni sawa na Asilimia 18.0 ya Pato la Taifa. Katika Robo ya Kwanza ya mwaka 2012/2013, makusanyo ya kodi na yasiyo ya kodi yalifikia jumla ya Shilingi Bilioni 1,922.3 sawa na Asilimia 91.1 ya makadirio ya kukusanya Shilingi Bilioni 2,111.2. Kiasi hicho cha makusanyo kimeongezeka kwa Asilimia 19.1 ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka 2011/2012.
9. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mapato yanayotokana na uingizaji wa bidhaa kutoka Nje, katika robo ya kwanza ya mwaka, makusanyo ya kodi kutokana na uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya Nchi (ikijumuisha Ushuru wa Forodha, Kodi ya Ongezeko la Thamani na Ushuru wa Bidhaa) ilikuwa Shilingi Bilioni 616.1, ikiwa ni Asilimia 90.2 ya makadirio ya kukusanya Shilingi Bilioni 683.1.
10. Kuhusu Mapato yanayotokana na Mauzo ya Ndani, Makusanyo halisi ya mapato katika robo ya kwanza yalikuwa Shilingi Bilioni 407.4 ambayo ni sawa na Asilimia 90.1 ya makadirio ya kukusanya Shilingi Bilioni 452.1 katika kipindi hicho. Makusanyo kutokana na Kodi ya Mapato katika robo ya kwanza yalikuwa Shilingi Bilioni 691.1 ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 657.6, sawa na Asilimia 105.1 ya kadirio hilo. Kwa ujumla ukusanyaji wa aina zote za kodi ya mapato ulikuwa wa kuridhisha.
11. Mheshimiwa Spika, katika robo ya kwanza ya mwaka 2012/2013, mapato halisi kutokana na vyanzo vinginevyo vya kodi yalikuwa Shilingi Bilioni 183.6 ikiwa ni Asilimia 89.9 ya lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 204.1. Makusanyo kutokana na mapato yasiyo ya kodi yalikuwa chini ya lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 175.5 ambapo Shilingi Bilioni 79.0 zilipatikana, ambayo ni Asilimia 45.0.
12. Wakati huo huo, katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2012, Serikali ilipokea Misaada ya jumla ya Shilingi Bilioni 469.8 sawa na Asilimia 74 ya makadirio ya Shilingi Bilioni 635.8. Kati ya misaada hiyo Shilingi Bilioni 402.6 zilikuwa ni Misaada ya Kibajeti na Shilingi Bilioni 67.1 ni za Miradi ya Maendeleo.
13. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Matumizi ya Serikali, katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2012/13, matumizi yalikuwa Shilingi Bilioni 2,445.1, ikilinganishwa na makisio ya matumizi ya Shilingi Bilioni 3,142.07, ikiwa sawa na Asilimia 77.8. Kati ya matumizi yote, Shilingi Bilioni 1,924.1 ni matumizi ya kawaida na Shilingi Bilioni 521.1 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo zikijumuishwa na fedha za miradi inayogharamiwa na wahisani wa nje. Jumla ya matumizi katika robo ya kwanza yalionesha ongezeko la Asilimia 6.0 ikilinganishwa na matumizi katika kipindi kama hicho katika mwaka 2011/2012.
14. Mheshimiwa Spika, Matumizi kwa ajili ya Mishahara yalikuwa Shilingi Bilioni 824.2 katika Robo ya Kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 679.8 katika robo ya kwanza ya 2011/2012, sawa na ongezeko la Shilingi Bilioni 144.37 au ongezeko la Asilimia 21.2. Ongezeko hili lilitokana na marekebisho ya Mishahara katika Sekta ya Umma kuanzia Julai 2012. Aidha, kwa upande wa Fedha za Maendeleo, katika kipindi cha robo mwaka, matumizi ya maendeleo yalikuwa ni Asilimia 57.4 ya Makadirio.
15. Mheshimiwa Spika, nimeamua kutoa taarifa hii hapa Bungeni, kuonesha kwamba utekelezaji wa Bajeti ya Serikali umeanza vizuri. Aidha, Serikali itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha kwamba, Mapato ya Ndani yanaimarishwa na Misaada na Mikopo yenye masharti nafuu kutoka nje, hususani kutoka kwa Washirika wa Maendeleo (Development Partners) na Taasisi mbalimbali za fedha za Kimataifa, inaendelea kuwa chanzo muhimu cha Mapato ya kugharimia Bajeti ya mwaka 2012/2013. Tayari Serikali imepokea Jumla ya Mikopo ya Shilingi Bilioni 642.5. Kati ya kiasi hicho, mikopo ya nje yenye masharti nafuu ilikuwa Shilingi Bilioni 143.4, sawa na Asilimia 62 ya makadirio na mikopo yenye masharti ya kibiashara kutoka nje ilikuwa Bilioni 46.6, sawa na Asilimia 7.3 na Shilingi Bilioni 452.6, ilikuwa ni mikopo ya ndani.
16. Mheshimiwa Spika, mtakumbuka kuwa kwa mara kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu nimekuwa nikieleza nia ya Serikali ya kubana matumizi yasiyo ya lazima wakati wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali. Nchi yetu ni Nchi Maskini hivyo, hatuna budi kutumia kiasi kidogo cha fedha zilizopo kuondokana na umaskini huo na kuwa Nchi yenye angalau Uchumi wa Kati. Kwa mfano, nimekuwa nikizungumzia kupunguza ununuzi wa Magari ya Kifahari kama vile Toyota Landcruiser VX. Zipo Toyota Landruiser VX 8- High Specifications na Toyota Landruiser VX 8-Standard. Bei ya VX 8- High Specifications ni zaidi ya Shilingi 300,000,000. Kiasi hicho pekee kinatosha kujenga Zahanati moja na Nyumba mbili za Watumishi. Aidha, kiasi hicho kinatosha kujenga Nyumba 6 za Watumishi wa Vituo vya Afya au kujenga Madarasa 17 ya Shule za Msingi. Kiasi hicho hicho kinatosha kununua Madawati 2,500 ya kukaliwa na Wanafunzi watatu watatu, au kununua Vifaa vya Maabara katika Shule za Sekondari, n.k. Hivyo, mtaona kuwa tukiacha kununua gari moja la VX-8 tunaweza kusaidia jamii ya Watanzania kwa kiasi kikubwa zaidi.
17. Mheshimiwa Spika, ili kubana matumizi tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali zifuatazo:
i) Tumekamilisha uchambuzi wa maeneo yasiyo ya lazima kwenye Bajeti yakiwemo Semina, Posho zisizo za lazima na kiasi halisi cha fedha zinazoweza kuhamishwa;
ii) Tumekamilisha uchambuzi wa maeneo au miradi ambayo inahitaji kuongezewa fedha na kiasi cha fedha kinachohitajika;
iii) Hivi sasa tunaandaa Mwongozo wa Ununuzi wa Samani za Serikali; na
iv) Tumeanza mchakato wa kuwa na viwango maalum vya magari ya Serikali kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi na Madaraja ya Watumishi wa Umma.
18. Mheshimiwa Spika, ili kuwe na maendeleo, lazima tulipe gharama ya maendeleo hayo. Hii ni pamoja na kujinyima sasa ili tunufaike zaidi baadaye sisi na watakaotufuatia kwa maana ya Vizazi vijavyo. Tanzania ni Nchi Maskini. Tunalo jukumu la kujinyima zaidi kwa ajili ya Wananchi wetu. Waswahili husema MCHUMIA JUANI HULIA KIVULINI. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge, Viongozi mbalimbali na Wananchi tukubaliane kwa pamoja katika hatua za kubana matumizi kwa manufaa ya Uchumi na Maendeleo yetu. Sote kwa pamoja hatuna budi kujenga utamaduni wa kuendesha Shughuli za Serikali kwa gharama ndogo. Aidha, Maagizo yangu kwa Watendaji wote wa Serikali katika ngazi zote ni kuzingatia Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge na kuendelea kuwa na nidhamu katika matumizi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Matumizi ya Serikali. Aidha, tushirikiane kusukuma shughuli za Maendeleo katika maeneo yetu ili yaende katika kasi inayotarajiwa.
III MAPENDEKEZO YA RATIBA MPYA YA UANDAAJI NA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI
19. Mheshimiwa Spika, kama baadhi yetu tunavyofahamu, yapo mapendekezo na ushauri ambao umekuwa ukitolewa na Bunge kupitia Kamati zake kuhusu Serikali kuandaa na kuwasilisha Bungeni mapendekezo ya Ratiba mpya ya maandalizi ya Bajeti ya Serikali. Lengo ni kuleta ufanisi, tija na ubora wa Mipango na Bajeti za Serikali zinazopitishwa na Bunge na kutekelezwa na Serikali.
20. Katika kuzingatia ushauri huo, Serikali imeandaa mapendekezo ya Ratiba hiyo ambayo imewasilishwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ili Kamati iweze kutafakari na kuishauri Serikali ipasavyo. Hata hivyo, mapendekezo hayo ya Ratiba mpya ya uandaaji na utekelezaji wa Mpango na Bajeti yameainisha changamoto mbalimbali na mapendekezo ya kukabiliana nazo. Katika mapendekezo hayo, Serikali imefanya marekebisho kwa kuandaa Ratiba mpya ya mzunguko wa uandaaji na utekelezaji wa Mipango na Bajeti ya Serikali ambayo yatasaidia kuboresha utaratibu wa uandaaji na utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Serikali. Mambo muhimu yaliyozingatiwa ni pamoja na haya yafuatayo:
i) Kuhakikisha Mwongozo wa uandaaji wa Mipango na Bajeti ya Serikali unatoka mapema zaidi;
ii) Uandaaji wa Mipango na Bajeti kwa Wizara mbalimbali uwe na muda wa kutosha;
iii) Vikao vya uchambuzi wa Mipango na Bajeti kati ya Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango pamoja na Wizara mbalimbali viwe na muda wa kutosha kuchambua Mipango na Bajeti za mafungu;
iv) Vikao vya uchambuzi wa Mipango na Bajeti kati ya Kamati za Kudumu za Kisekta za Waheshimiwa Wabunge pamoja na Mafungu viwe na muda wa kutosha kuchambua Mipango na Bajeti za mafungu;
v) Bajeti ya Serikali pamoja na Miswada ya Sheria ya Fedha (Finance Bill) na Sheria ya Matumizi (Appropriation Bill) zipitishwe na Bunge mwishoni mwa mwaka wa fedha;
vi) Ratiba mpya inazingatia pia ushirikishwaji wa kina wa Kamati za Kudumu za Bunge za Kisekta kabla ya uandaaji wa Mipango na Bajeti kukamilika;
vii) Ratiba mpya ya uandaaji na utekelezaji wa Mipango na Bajeti iwezeshe ushirikishwaji wa Wadau wengi ili kuhakikisha Bajeti inazingatia matakwa ya Wananchi walio wengi zaidi; na
viii) Katika mapendekezo hayo, utoaji wa taarifa za uandaaji wa Mipango Kazi, Mipango ya ununuzi na uratibu wa utekelezaji wa Mipango na Bajeti zimezingatiwa.
21. Mheshimiwa Spika, ni matumaini yangu kwamba, mara makubaliano yatakapofikiwa utaratibu wa kutumia Ratiba hii utaanza kuzingatiwa.
IV UENDELEZAJI WA LUGHA YA KISWAHILI
22. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge walipokea na kujadili pamoja na mambo mengine Maazimio mbalimbali. Niruhusu nirejee Azimio lililonigusa sana kuhusu Uanzishaji wa Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili. Awali, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Chama cha Kiswahili Tanzania (CHAKITA) na Wawakilishi kutoka Uganda walianzisha wazo la kuwa na Mpango wa Kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki. Hata hivyo, Baraza hilo halikuanzishwa, badala yake ikapendekezwa kuanzisha Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili. Azimio la Kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo ya Lugha ya Kiswahili tumelipitisha katika Bunge hili. Nitumie fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao ambayo imetusaidia kupitisha Azimio hilo, lenye nia njema ya kujenga Lugha ya Kiswahili.
23. Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala kuhusu kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo, michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge imeonesha umuhimu wa kutumia fursa zilizopo kwa Tanzania kuwa Dira, Mfano na Kitovu cha Lugha ya Kiswahili. Aidha, Waheshimiwa Wabunge walionesha umuhimu wa kutumia Kiswahili kama nguzo imara ya Mshikamano, Amani na Utulivu miongoni mwa Watanzania. Lakini pia majadiliano yamebaini Changamoto zilizopo.
Moja ya Changamoto hizo ni hoja ya Waheshimiwa Wabunge wengi kwamba, Nchi jirani ya Kenya inatumia fursa zilizopo za Lugha ya Kiswahili vizuri zaidi kuliko sisi. Kutokana na uzito wa hoja hiyo, ndiyo maana ninapenda kuchangia machache.
24. Mheshimiwa Spika, Tanzania ni Mdau Mkuu wa Matumizi ya Kiswahili katika Afrika. Ziko taarifa kwamba Watanzania ndiyo walioanzisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Ghana, Chuo Kikuu cha Port Harcourt, Nigeria na Chuo Kikuu wa Sebha, Libya. Inawezekana upo ukweli pia kwamba leo hii wengi walioko katika Vyuo hivyo ni kutoka Kenya. Japo imekuwa vigumu kupata takwimu za Ajira ya Walimu wanaofundisha katika Nchi hizo kutokana na kwamba ajira iko katika Soko Huria. Hakuna Chombo maalum kinachoratibu Ajira za Walimu hao kwenye Vyuo Vikuu. Nina hakika hii ni moja ya sababu zilizofanya Wachangiaji wengi kutumia “Uzoefu” zaidi katika kujenga hoja hiyo kwamba Walimu wengi wanatoka Kenya. Wakati sasa umefika wa kuwa na Utaratibu Maalum wa upatikanaji wa Walimu wa Kiswahili wenye sifa za kufundisha Nje ya Nchi.
25. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wameainisha mapungufu mbalimbali ambayo yanachangia katika tofauti iliyopo kati yetu na jirani zetu wa Kenya. Pamoja na mapungufu hayo, bado Tanzania imekuwa Kitovu cha Lugha ya Kiswahili Duniani. Walimu wa Kiswahili Nchini Ujerumani, Hamburg, Berlin, Colon, Leipzig na Chuo cha INALCO Ufaransa, walifundishwa na Walimu kutoka Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) Zanzibar na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwalimu wa Siku Nyingi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha London (School of Oriental African Studies - SOAS) anatoka Tanzania, Prof. Farouk Topan ambaye ndiye alikuwa Mkuu wa Kwanza wa Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Walimu wa Kiswahili hadi sasa kule Korea, katika Chuo Kikuu cha Hankuk wanatoka Tanzania. Walimu wa Osaka, Japan walitoka Tanzania, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Zanzibar.
26. Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, yapo mahitaji makubwa ya Lugha ya Kiswahili kwa sasa. Katika Afrika ya Mashariki peke yake, Uganda wanahitaji Walimu zaidi ya 10 kwa ajili ya Vyuo vyao Vikuu. Vilevile, wanataka Walimu katika Shule za Sekondari. Rwanda na Burundi wanahitaji Walimu na Jamhuri ya Watu wa Kongo (DRC) wanahitaji Walimu kwa ajili ya Vyuo vyao vya Lubumbashi na Kalemie. DRC wanahitaji pia Vitabu vya Kiswahili Sanifu.
27. Mheshimiwa Spika, mahitaji ya Kiswahili yako katika Nchi nyingi. Chuo Kikuu cha Kwazulu, Natali, Afrika ya Kusini kimeanzisha masomo ya BA Kiswahili, hivyo, watahitaji Walimu. Chuo Kikuu cha Zimbabwe kinahitaji Walimu wa Kiswahili. Namibia wameomba Walimu kuanzisha Kiswahili katika Chuo chao Kikuu. Jamaica Wanahitaji Walimu wa kuanzisha masomo ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha West Indies. Baadhi ya Vyuo Vikuu vya Marekani kikiwemo Chuo Kikuu cha Lugha cha Monterey, California wanahitaji Walimu wa Kiswahili. Hapa Nchini Vyuo Vikuu zaidi ya 20 kando ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vimeanzisha Masomo ya Kiswahili na vitahitaji Walimu wenye Shahada za Uzamili na Uzamivu katika Kiswahili. Hivyo, mahitaji ni makubwa kupita kiasi na hivyo hii ni fursa kubwa kwa Watanzania wenye sifa kujipatia ajira.
28. Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Desemba 2005, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akifungua rasmi Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema na nanukuu:
“Lugha ya Kiswahili imeanza kupata umaarufu Afrika na Duniani. Umoja wa Afrika umekubali Kiswahili kuwa moja ya Lugha zake Kuu. Aidha, Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu zimekubali kutumia na kuendeleza Kiswahili. Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa juhudi hizi zinaendelezwa na kuhakikisha kuwa Lugha ya Kiswahili inakua Nje ya Mipaka ya Afrika”. Mwisho wa Kunukuu.
29. Kwa maneno haya ya Mheshimiwa Rais, ni dhahiri kwamba, Serikali inajali umuhimu wa kuendeleza Lugha ya Kiswahili, kwa vile ina nafasi nzuri ya kupanuka na kushiriki katika ujenzi wa Jamii ya Watanzania na Jamii mpya ya Afrika ya Mashariki na hata Duniani kote.
30. Mheshimiwa Spika, tunayo Changamoto ya kukifanya Kiswahili kiwe Lugha ya Dunia. Lakini pia tunalo jukumu la kuhakikisha kwamba Lugha ya Kiswahili inafundishwa na kutumika Mashuleni, ikiwa ni pamoja na Shule za Msingi, na kwamba inafundishwa katika Shule za Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Juu. Aidha, tunahitaji kuhakikisha kwamba Lugha ya Kiswahili inatumika vizuri na kwa ufasaha katika Shughuli za Serikali, hapa Bungeni, katika Mahakamani na maeneo mengine kwa faida ya Wananchi wetu na Taifa kwa ujumla. Hata hivyo, pamoja na msisitizo huo, yapo maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi zaidi. Kwa mfano:
Moja: Bado kuna maeneo mengi yanayohusu Taaluma ya Kiswahili ambayo hayajafanyiwa utafiti wa lugha. Utafiti ndio uhai wa Taaluma na chimbuko la maarifa mapya. Ni kazi ya Wanataaluma wa Kiswahili kufanya tafiti za kina ambazo zitakifanya Kiswahili kitumiwe Kimataifa.
Pili: Vyuo Vikuu vilivyoanzishwa, pamoja na kuweza kufundisha somo la Kiswahili kwa Wanachuo wa Shahada ya Kwanza, bado havina Wahadhiri wa kutosha wa kufundisha mafunzo ya Uzamili na Uzamivu. Tunalo jukumu la Kuanzisha Programu za Shahada za Uzamili na Uzamivu zitakazokidhi mahitaji makubwa ya uhaba wa Wataalamu wa Kiswahili Ndani na Nje ya Nchi.
Tatu: Hapa Nchini hakuna Chuo Kikuu kinachotoa mafunzo ya Ukalimani. Watu wanaohitaji stadi hii ya ukalimani wanalazimika kwenda kusomea katika Vyuo Vikuu vya Nje ya Afrika Mashariki. Mimi najiuliza, hivi hili nalo tunalikubali wakati Lugha ni yetu? Ninaamini tunao uwezo wa kutumia Vyuo Vikuu na Vyuo vingine tulivyonavyo kufanya kazi hii ya kufundisha Wakalimani. Ni vizuri Vyuo vyetu Nchini vianzishe Idara za Mafunzo ya Ukalimani ili kupunguza tatizo hilo.
Nne: Imebainika pia kwamba, hata kama kukiwepo na Wakalimani, bado hakuna Kumbi za kisasa zenye vifaa vya kusikilizia Tafsiri za Lugha mbalimbali. Kumbi nyingi tunazofanyia Mikutano tukiacha Ukumbi wa Kimataifa wa Arusha (AICC) hazina Vifaa hivyo. Changamoto tulio nayo kama Nchi na hasa Wawekezaji wa Kumbi za Mikutano ni kuhakikisha Kumbi zinazojengwa na zilizopo zinakuwa na Vifaa vya kutoa huduma ya Ukalimani. Lengo ni kutumia fursa hiyo katika kukuza Lugha yetu ya Kiswahili.
31. Mheshimiwa Spika, mimi napata shida sana kuona Warsha yenye Wageni wasiozidi Kumi (10) na Waswahili 200 inaendeshwa kwa lugha ya Kiingereza, tena bila kujali kama Waswahili hao wanaelewa Kiingereza au la. Wanachojali ni kuwafurahisha Wageni Watano. Kwa maoni yangu hii ni kasumba isiyo na maelezo. Changamoto iliyo mbele yetu ni kuondoa kasumba hii kwa kupenda kutumia lugha yetu ya Kiswahili wakati wote. Tuondoe wasiwasi katika matumizi ya Lugha ya Kiswahili. Tumeshuhudia Kiswahili kikikuzwa na kutandazwa katika Mifumo ya Kompyuta ya Linux na Microsoft. Tumesikia pia kwamba, kama njia mojawapo ya kuboresha matumizi ya Kiswahili sanifu, tayari Wataalamu wa lugha kwa kushirikiana na Wataalamu wa Kompyuta wameweza kutengeneza Programu Maalum ya Kisahihishi cha Lugha ya Kiswahili katika Kompyuta ambayo inatumiwa kusahihisha maneno ya Kiswahili. Haya ni maendeleo makubwa yaliyofikiwa ya kukiingiza Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Duniani.
32. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba Lugha ya Kiswahili imekua sana. Wote ni mashahidi kwamba Mashirika makubwa ya Utangazaji Duniani yanatangaza Kiswahili. Tunajua sana Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Sauti ya America, Radio ya Ujerumani Deutsche -Well na Radio France International. Wako pia Al Jazeera, Radio Vatican, Radio Japan na Radio ya Umoja wa Mataifa. Aidha ziko Nchi zenye Vituo vya Radio vinavyotangaza kwa lugha ya Kiswahili, kwa mfano, China, India, Syria, Misri, Sudan n.k. Hii pia ni ishara kwamba Kiswahili kinakua kwa kasi sana.
33. Mheshimiwa Spika, tunaweza kuongea mengi ya nadharia kuhusu lugha yetu nzuri ya Kiswahili kwa muda mrefu. Tunatakiwa sasa tuanze kutekeleza hayo mengi kwa vitendo. Napenda kuhimiza Taasisi mbalimbali Nchini, ziweke juhudi zote katika kukuza Lugha ya Kiswahili ili iweze kutumika katika Nyanja zote za mawasiliano ikiwemo Sayansi na Teknolojia. Vilevile, natoa Rai kwa Watanzania wote wakiwemo Waheshimiwa Wabunge kujitahidi kila tunapozungumza Kiswahili kuepuka kuchanganya na maneno ya Lugha ya Kiingereza kwenye mazungumzo yetu.
34. Baadhi yetu tunamkumbuka Mwandishi na Mshairi wa Riwaya Bwana Shaban Robert (1909 – 1962) ambaye aliandika kuhusu Lugha ya Kiswahili na kukifananisha na ladha ya Titi la Mama. Katika moja ya Mashairi yake, aliandika na nanukuu:
“Titi la Mama litamu, hata likiwa la Mbwa,
Kiswahili naazimu, sifayo iliyofumbwa,
Kwa wasiokufahamu, niimbe ilivyo kubwa,
Toka kama mlizamu, funika palipozibwa,
Titi la Mama litamu, jingine halishi hamu.
Lugha yangu ya utoto, hata sasa nimekua,
Tangu ulimi mzito, sasa kusema najua,
Ni sawa na manukato, moyoni mwangu na
pua,Pori bahari na mto, napita nikitumia,
Titi la Mama litamu, jingine halishi hamu”. Mwisho wa Kunukuu.
35. Anachosema Bwana Shaaban Robert ni kuonesha thamani ya Kiswahili jinsi kilivyo na utamu wa aina yake katika matumizi. Historia ya Shaaban Robert, tunaambiwa alithubutu kulikataa kabila lake la Kiyao na kujiita Mswahili kuonesha jinsi alivyokipenda Kiswahili. Nasi tujivunie Kiswahili, tukipende, tukitumie, tukienzi na tukithamini. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumechangia katika kuendeleza Lugha ya Kiswahili.
36. Mheshimiwa Spika, Watanzania sasa si wakati wa kulalamikiana na kulaumiana juu ya Matumizi ya Lugha ya Kiswahili, bali sasa tushirikiane kujenga Lugha yetu ya Kiswahili. Njia iko wazi, kazi kwetu!
V KUANZISHWA KWA HUDUMA ZA USAFIRI WA RELI JIJINI
DAR ES SALAAM
37. Mheshimiwa Spika, huduma ya usafiri wa njia ya Reli Jijini Dar es Salaam ni mojawapo ya hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kupunguza tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam. Mwezi Agosti 2012 wakati Waziri wa Uchukuzi alipokuwa anasoma Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, alilieleza Bunge lako tukufu kwamba, Wizara yake inakusudia kuanza kutoa huduma ya usafiri wa njia ya Reli kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari barabarani katika Jiji la Dar es Salaam kuanzia mwishoni mwa mwezi Oktoba 2012.
38. Ili kufanikisha lengo hilo, Wizara ilichukua hatua za maandalizi kwa kukarabati na kuweka miundombinu muhimu ya kuwezesha kuanza kwa usafiri katika njia za Reli zifuatazo:
i) Reli ya TAZARA kati ya Vituo vya Kurasini kupitia Stesheni ya TAZARA, Dar es Salaam hadi Pugu Mwakanga (Km. 24.5); na
ii) Reli ya TRL kutoka Ubungo Maziwa kupitia Tabata-Relini, Tabata – Matumbi na Buguruni – Mnyamani hadi Katikati ya Jiji (Km.12).
39. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Reli ya TAZARA, Miundombinu ya Reli hii haikuhitaji matengenezo makubwa. Hata hivyo, ukarabati mkubwa ulifanywa wa Mabehewa saba na Vichwa viwili vya Treni. Pia maboresho yalifanywa na yanaendelea kufanywa ya ujenzi wa Vituo na sehemu zilizoinuliwa kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria pamoja na vibanda vya kukatia tiketi. Hivyo, usafiri wa Treni ya TAZARA umekuwa wa msaada mkubwa na wa haraka kwa Wakazi wa Dar es Salaam waishio karibu na Reli hiyo hadi Pugu Mwakanga na Kurasini. Wastani wa Abiria 6,000 hutumia huduma ya Reli hii kila siku.
40. Katika Reli ya TRL, kazi ya ukarabati wa miundombinu ilihusisha:
(i) Ukarabati wa Reli yenyewe na ujenzi wa sehemu zilizoinuliwa kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria (platforms);
(ii) Ujenzi wa vibanda vya kukatia tiketi na vibanda vya wasafiri kusubiria Treni;
(iii) Ujenzi wa Stesheni ya Buguruni kwa Mnyamani pamoja na eneo la kupishania Treni;
(iv) Ujenzi wa Stesheni ya Ubungo pamoja na sehemu ya kugeuzia Treni;
(v) Kuweka mfumo wa mawasiliano ya uendeshaji Treni;
(vi) Ujenzi wa vyoo kwenye Stesheni za Dar es Salaam na Ubungo;
(vii) Ujenzi wa Vivuko vya Barabara na Reli (Level Crossings) na vibanda vya Walinzi wa Vivuko hivyo (level crossing attendants); na
(viii) Ukarabati wa Mabehewa 14 na Injini tatu (3).
41. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba 2012, ukarabati wa miundombinu hiyo ulikuwa umekamilika kwa kiasi kikubwa na hivyo kuwezesha Treni moja tu kuanza kufanya safari. Hivyo, ukarabati bado unaendelea ili kuwezesha Treni mbili kufanya kazi kwa wakati mmoja.
42. Mheshimiwa Spika, mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na kuanza kwa huduma hii. Tangu huduma hii ianze kutolewa tarehe 29 Oktoba 2012, imepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wakazi wa Dar es Salaam. Hivi sasa huduma inatolewa kwa kutumia Treni moja yenye mabehewa sita yenye uwezo wa kubeba abiria 600 kwa safari moja. Siku za huduma hii ni kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi isipokua siku za Jumapili na Sikukuu. Aidha, Treni hii hufanya safari mara sita kwa siku, yaani safari tatu Asubuhi na Jioni sawia. Safari huanza saa 12.00 hadi saa tano Asubuhi kutoka Stesheni ya Ubungo Maziwa hadi Stesheni ya Dar es Salaam na kusimama hadi saa 9:40 Alasiri ambapo huanza tena hadi saa 2:00 usiku. Muda wa safari ni takribani nusu saa hadi dakika arobaini (40). Inatarajiwa kwamba usafiri huu utakuwa na ubora zaidi hapo ujenzi wa miundombinu muhimu itakapokamilika kuruhusu Treni mbili kupishana na kuwezesha kichwa cha Treni kugeuza katika Stesheni ya Ubungo Maziwa.
43. Mheshimiwa Spika, Mradi huu unashabihiana kihuduma na Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) utakapoanza huduma ya Mabasi yake. Uhusiano huo unatokana na Vituo vingine vya Treni kuwa karibu na Vituo vya DART na hivyo kuwezesha Miradi hii miwili kutoa huduma ya usafiri wa Abiria kwa ukamilifu zaidi.
44. Napenda kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb.), Waziri wa Uchukuzi na timu yake katika Wizara pamoja na Mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Uchukuzi, hasa Kampuni ya TRL, TAZARA, RAHCO na SUMATRA kwa kuwezesha kuanza kwa usafiri huu. Mmefanya kazi nzuri ingawa najua bado kuna changamoto nyingi. Nawaomba msiridhike na mafanikio hayo kwani mafanikio hayo yameibua pia changamoto nyingi ambazo mnapaswa kukabiliana nazo kikamilifu ili huduma hii iwe endelevu.
45. Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Wananchi wanaotembea kwa Miguu katika njia za Reli na wengine wanaotumia njia za Reli kama sehemu za kufanyia Biashara Ndogo Ndogo kuacha kufanya hivyo. Watambue kwamba matumizi ya njia ya Reli ni kwa ajili ya Treni na kwa hiyo, waone umuhimu wa kulinda usalama wao na wa Abiria wa Treni. Pia waaepuke kuzalisha takataka zinazochafua mazingira katika njia za Reli, Vituo vya Treni na kuziba mifereji ya kupitishia maji ya mvua.
VI YATOKANAYO NA ZIARA YA MIKOA YA SHINYANGA, GEITA NA MWANZA
46. Mheshimiwa Spika, tarehe 09 hadi 18 mwezi Septemba, 2012 nilifanya Ziara ya Kikazi katika Mikoa ya Shinyanga (Kahama), Geita na Mwanza. Madhumuni ya ziara hiyo yalikuwa ni kuona fursa za maendeleo zilizopo katika Mikoa hiyo na jinsi zinavyoweza kutumiwa kwa ajili ya maendeleo ya Wakazi wa Mikoa hiyo na kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla. Aidha, nilitaka kuona jinsi Mikoa hiyo na Wilaya zake inavyotekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, MKUKUTA II, na Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa na katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025.
47. Mheshimiwa Spika, kutokana na Ziara yangu hiyo yapo masuala muhimu yaliyojitokeza, na ambayo nimeona ni vyema kuyawekea msisitizo. Kwa mfano, nikiwa Wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga na Wilaya ya Geita katika Mkoa Mpya wa Geita, nilipokea maombi kutoka kwa Vijana wengi wa maeneo hayo wakitaka wapatiwe ajira Migodini. Hata hivyo, changamoto kubwa inayowakabili Vijana hao ni ukosefu wa ujuzi na stadi stahiki katika Sekta ya madini. Hali hiyo imesababisha nafasi za ajira kuchukuliwa na Vijana kutoka nje ya Mikoa hiyo na Vijana wa maeneo hayo kukosa Ajira katika Migodi iliyoko kwenye Mikoa yao. Kwa ujumla kukosekana kwa ujuzi na stadi kumetokana na kutokuwa na Vyuo au Taasisi zinazotoa mafunzo kuhusu usimamizi au uchanguaji na uongezaji thamani katika Madini yanayotoka katika Migodi hiyo. Aidha, Vyuo vya VETA vya Shinyanga na Mwanza havina kozi stahiki kuhusu Madini.
48. Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto hiyo, niliviagiza Vyuo vyote vya VETA katika Mikoa hiyo vianzishe utaratibu wa kuwa na Kozi fupi na ndefu zitakazowajengea uwezo Vijana katika masuala ya madini ili waweze kupata fursa ya kuajiriwa katika Migodi hiyo au kujiajiri wenyewe. Aidha, kama suluhisho la muda mrefu, Serikali tutaendelea kutoa msukumo kuhakikisha kuwa Vyuo vya VETA vinakuwa na Mitaala maalum kuhusu masuala ya madini hasa katika maeneo ya Kanda ya Ziwa. Kwa mantiki hiyo, napenda kutoa Wito kwa Uongozi wa Vyuo vya VETA Nchini kuanzisha Kozi maalum zitakazosaidia Vijana kuajiriwa au kujiajiri katika maeneo maalum kulingana na fursa zilizopo katika maeneo yao kama vile, madini kwa sehemu zenye Madini na Uvuvi wa Kisasa. Kwa kufanya hivyo, tutasaidia sana Vijana wetu kupata ajira na hata kujiajiri kutokana na fursa zilizopo.
a) Matumizi ya Matrekta Katika Kilimo
49. Mheshimiwa Spika, katika ziara hiyo pia nilibaini kuwa bado tunahitaji kuongeza bidii katika kuwawezesha Wananchi kuongeza Matumizi ya zana bora za Kilimo hususan Matrekta makubwa na madogo. Bado Wananchi kiasi cha Asilimia 70 wanategemea Jembe la Mkono. Hata hivyo, ni wazi kuwa kilimo cha Jembe la Mkono kamwe hakiwezi kumfanya Mkulima kupata mazao zaidi ili aweze kujipatia chakula cha kutosha na ziada ambayo anaweza kuuza na kuinua kipato chake. Ni jukumu letu kumsaidia Mwananchi ili aondokane na hali ya kutegemea dhana duni za Kilimo ikiwemo Jembe la Mkono. Hivyo, naziagiza Halmashauri zote Nchini ziwasaidie Wananchi kuunda Vikundi vya Uzalishaji na kuwawezesha kupata Matrekta ili kukuza Kilimo na kuongeza uzalishaji. Pamoja na mpango huo, kila Halmashauri inapaswa ihakikishe Matrekta hayo yanapatikana na yanakopeshwa kwa Wananchi kwa bei nafuu.
50. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na jitihada za kuagiza matrekta zaidi kwa lengo la kuwafikishia Wananchi wote Nchini. Hivi sasa Serikali inazungumza na Serikali ya India ili kupata tena Matrekta 3,000 kupitia SUMA JKT kutoka Nchini India baada ya Matrekta ya awali kununuliwa yote kutokana na uamuzi wa Serikali wa kuyapunguza bei na ubora wake. Nawashauri Uongozi wa Mikoa kuchangamkia fursa hiyo mapema kwani kwa mwenendo huu, Matrekta hayo yanaweza pia kwisha mapema kutokana na mwamko mkubwa ambao Wananchi wameupata. Aidha, nawaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kufuatilia kwa karibu matumizi ya Matrekta hayo kwani lengo ni kuongeza tija na uzalishaji katika Kilimo cha Mazao. Haitakuwa na maana kwa Mkoa au Halmashauri yoyote kuwa na Matrekta mengi wakati hayatumiki kwa shughuli za kumwondolea Mwananchi Umaskini.
b) Kilimo cha Umwagiliaji
51. Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa ili kumkomboa Mwananchi sharti kuwe na mikakati ya kumwezesha Mkulima kuwa na Kilimo cha Uhakika kisichotegemea misimu ya mvua. Hata hivyo, katika ziara yangu nilibaini kuwa maeneo mengi yanayofaa kwa ajili ya Kilimo cha Umwagiliaji hayatumiki ipasavyo. Kilimo cha Umwagiliaji kina nafasi muhimu ya kuwaletea Wananchi maendeleo. Hivyo, naziagiza Halmashauri zote Nchini kuandaa na kutekeleza Programu za Umwagiliaji kwa kutengeneza Skimu za Umwagiliaji ili ziweze kufikia angalau nusu ya eneo linalofaa kwa Umwagiliaji. Siyo lazima kuanza na Teknolojia ya hali ya juu na ambayo ni ghali. Tunaweza kuanza na Teknolojia rahisi na za bei nafuu za Umwagiliaji.
c) Wawekezaji Wazalendo
52. Mheshimiwa Spika, katika ziara yangu niliweza pia kuzindua Miradi ya Wawekezaji Wazalendo ukiwemo Mradi wa Kilimo cha Mboga katika Kampuni ya Ngongoseke Holticulture Farm - Kijiji cha Nsola, Wilaya ya Magu na Mradi wa Supermarket ya Kimataifa Mjini Kahama. Nimefarijika sana kuona jitihada hizi kubwa zinazofanywa na Watanzania wenzetu na Wananchi wazawa katika kuwekeza katika maeneo ya nyumbani kwao. Huu ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na Watanzania wengine wanaoishi nje ya Mikoa au Wilaya zao kwa kuwekeza Miradi ya maendeleo katika maeneo wanakotoka. Jambo la kutia moyo zaidi katika Miradi hiyo ni kuzalishwa kwa ajira nyingi kwa Wananchi wa maeneo hayo.
d) Hali ya Ununuzi wa zao la Pamba kwa Msimu wa Mwaka 2012/2013 na juhudi za Serikali
53. Katika ziara yangu pia nilipokea malalamiko ya Wananchi wakitaka kujua kwa nini zao la Pamba kwa Msimu wa mwaka 2011/2012 lilikuwa na bei ya chini kuliko msimu uliopita na pia chini ya matarajio yao. Nami nilitumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi wa suala hilo. Hata hivyo, napenda kutumia Bunge hili kutoa tena ufafanuzi kuhusu Bei ya Pamba.
54. Mheshimiwa Spika, kimsingi bei ya pamba inapangwa na Soko la Dunia. Hata hivyo, katika Msimu wa mwaka 2011 bei ya pamba ilikuwa juu ambapo hapa Nchini ilifikia Shilingi 1,100. Kupanda kwa Bei hiyo kulisababishwa na uhitaji mkubwa wa Pamba Duniani na kutokana kwamba Nchi zinazozalisha Pamba kwa wingi Duniani hazikuweza kuzalisha kwa sababu ya mafuriko. Katika Msimu wa mwaka 2012, Nchi hizo hazikukumbwa na mafuriko na zimezalisha Pamba kwa wingi na hivyo, dunia kuwa na Ugavi (Supply) mkubwa wa Pamba ikilinganishwa na mahitaji (demand) na hivyo bei kushuka. Kimsingi, bei halisi ya Pamba ilikuwa Shilingi 420 kwa kilo, lakini baada ya Serikali kuingilia kati ilipandisha bei hadi kufikia Shilingi 660 kwa kilo.
55. Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa makali ya madhara ya kuyumba kwa bei ya Pamba Duniani yanadhibitiwa. Moja ya hatua hizo ni kuuza Pamba inayolimwa hapa Nchini katika Soko la ndani. Lengo likiwa ni kuboresha Viwanda vya ndani vya nguo na pia kumpatia Mkulima uhakika wa Soko kwa mazao yake. Kama mnavyokumbuka katika Mkutano wa Bunge uliopita tuliwaeleza kuwa Serikali imeridhia kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa viwanda vya nguo Nchini ili viweze kuongeza uzalishaji wa nguo kama vile kanga, vitenge, n.k na kupunguza bei za nguo zinazozalishwa na Viwanda hivyo ili kumnufaisha Mwananchi.
56. Naomba kutoa Wito kwa Viwanda vya Nguo Nchini kuona uwezekano wa kuzalisha Sare (Uniforms) mbalimbali zinazotumiwa Nchini ikiwemo Shule pamoja na Sare za Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kutumia Pamba tunayozalisha. Hali hii itaongeza matumizi na bei ya Pamba tunayozalisha na kumnufaisha Mkulima badala ya kutegemea bei ya Pamba katika Soko la Dunia ambayo haina uhakika.
e) Fursa ya Ziwa Victoria
57. Mheshimiwa Spika, Ziwa Victoria ni rasilimali ambayo inatosha kabisa kuipandisha Kiuchumi Mikoa inayozunguka Ziwa hilo pamoja na Wananchi wake kutoka kwenye umaskini. Ziwa hili lina jumla ya Kilomita za Mraba 68,800. Kati ya hizo, Kilomita za Mraba 35,088, sawa na asilimia 51 ya ukubwa wa Ziwa lote zipo Tanzania. Kilomita za Mraba 29,584, sawa na Asilimia 43 zipo Uganda, na Kilomita za Mraba 4,128, sawa na Asilimia 6 zipo Kenya.
58. Ziwa Viktoria ni fursa kubwa kwa Wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa katika Sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji, Uvuvi na Utalii na lina nafasi kubwa ya kuongeza kipato cha Wananchi. Pamoja na fursa zilizopo katika Ziwa hilo, bado hazijaweza kutumika ipasavyo. Vilevile, zipo Changamoto nyingi zinazojitokeza. Changamoto hizo ni pamoja na kupungua kwa kiasi cha samaki kunakotokana na kutozingatiwa kwa Kanuni bora za Uvuvi. Takwimu zinaonesha kuwa Uvuvi Haramu unaongezeka siku kwa siku. Uvuvi haramu una athari kubwa kwa masalia ya samaki na ukuaji wake na unaharibu uwiano kati ya ukuaji wa Samaki na uvunaji wake. Uvuaji wa Samaki wachanga, matokeo yake ni kupungua kwa Samaki kwa kasi kubwa.
59. Napenda kuwakumbusha kuwa, Utafiti uliofanywa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) unaonesha kuwa kwenye Ziwa Victoria Samaki aina ya Sangara wamepungua kwa Asilimia 60 hadi kufikia mwaka 1999, Asilimia 32 katika kipindi cha 1999-2007 na Asilimia 16 kipindi cha 2007 - 2009.
60. Naomba nitoe rai kwa Wananchi wa Kanda ya Ziwa kuwa, utajiri wa Samaki uliopo leo katika Ziwa hili, si wa kudumu iwapo wataendelea na Uvuvi Haramu. Rasilimali hii ni ya kutunzwa ili fursa hii iweze kutumika na Kizazi hiki na vijavyo.
g) Maendeleo ya Sekta ya Mifugo
61. Mheshimiwa Spika, Azma ya Serikali katika Sekta ya Mifugo ni kutaka kuondokana na kuchunga Mifugo mingi isiyokuwa na tija na ambayo haiendani na eneo la ardhi inayotosheleza kwa malisho ili pia kuepuka uharibifu wa mazingira. Nikiwa katika ziara, nilibaini kuwa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa kama ilivyo Mikoa mingine Nchini kuna Mifugo mingi ambayo haiendani na uwezo wa malisho (Carrying Capacity). Kwa takwimu za Kitaifa inashauriwa kuwa Ng’ombe mmoja hutumia Ha 4.03 za malisho kwa mwaka.
62. Naomba kutoa Wito kwa Wafugaji kutumia Mifugo mingi waliyonayo kama fursa ya kumnufaisha Mfugaji na kumwingizia kipato, kwa kuuza kubakiza kiasi ambacho kinaendana na eneo lililopo. Nawahimiza wachukulie Mifugo kuwa ni shughuli ya kuwaondolea Umaskini na waachane na mazoea ya kuwa na makundi makubwa ya Mifugo yenye tija ndogo.
63. Natoa wito kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuwaelimisha Wananchi kuhusu suala hili. Aidha, Halmashauri zote ziwasimamie kikamilifu Watumishi wa Sekta ya Mifugo ili watekeleze majukumu yao ipasavyo kwa kufungua Mashamba Darasa ya Mifugo ya kuwaelimisha Wafugaji.
64. Upo umuhimu wa kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi na kutenga maeneo maalum ya malisho ya mifugo. Katika maeneo hayo lazima kuzingatia uwiano baina ya ardhi na idadi ya mifugo iliyopo. Aidha, maeneo hayo yawekewe miundombinu muhimu ya kufugia ikiwemo Malambo, Majosho, n.k. Kwa kufanya hivyo tutaepuka migogoro mingi inayojitokeza kati ya Wakulima na Wafugaji.
VII TAARIFA KUHUSU MPANGO WA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZA SERIKALI KWA UWAZI (OPEN GOVERNMENT PARTNERSHIP)
65. Mheshimiwa Spika, nilishawahi kuliarifu Bunge lako Tukufu juu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujiunga rasmi na Mpango wa Uendeshaji Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership – OGP) tarehe 21 Septemba, 2011. Uamuzi wa kujiunga na Mpango huo ulilenga katika kuimarisha utekelezaji wa Mipango mingine ya maboresho ambayo Serikali inayatekeleza na faida ambazo Mpango huu utatuletea kama tukiutekeleza kwa umakini.
66. Mheshimiwa Spika, Mpango huu unajikita katika maeneo makuu manne ambayo ni; Moja, Kuweka Uwazi zaidi katika uendeshaji wa Shughuli za Serikali. Pili, Ushirikishwaji wa Wananchi katika kuweka Mipango na utekelezaji wa Shughuli za Serikali. Tatu, Kuimarisha Uwajibikaji katika Utendaji na Kuimarisha Juhudi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa, na Nne, Kuweka umuhimu wa Matumizi ya Teknolojia na Ubunifu.
67. Mheshimiwa Spika, Tanzania imeamua kutekeleza Mpango wa OGP katika Sekta tatu (3) za huduma za Jamii ambazo ni Afya, Maji na Elimu. Pamoja na Mpango kujielekeza kwenye Sekta hizo, pia umejikita katika maeneo ya Uwazi, ushirikishwaji wa Wananchi, Uwajibikaji na Uadilifu na Teknolojia na Ubunifu.
68. Mheshimiwa Spika, vipaumbele vilivyopo kwenye Mpango huu vitatekelezwa na Wizara na Taasisi za Serikali kwa kutumia Rasilimali zinazosimamiwa na Makatibu Wakuu. Sekta zinazohusika moja kwa moja na utekelezaji zitaweka kwenye Bajeti na Mipango yao utekelezaji wa Mpango wa OGP. Wizara husika zimeandaa Mpango mkakati wa utekelezaji unaoainisha muda wa kutekeleza, wahusika (watakaotekeleza) na Bajeti.
69. Mheshimiwa Spika, tayari Kamati ya Kitaifa imeshaandaa “Roadmap” ya shughuli zitakazotekelezwa hadi kufikia Juni, 2012 ukionesha “Commitments” za kila Sekta. Mpango Kazi umeainisha shughuli zitakazotekelezwa, viashiria, muda na bajeti za utekelezaji. Sekta zimeandaa pia Mpango Kazi na kuziwasilisha kwenye Kamati. Asasi zote Zisizo za Kiserikali zilizo elekezwa kuandaa Mipango Kazi bado hazijatekelezwa kufanya hivyo. Tunaendelea kuwakumbusha.
70. Mheshimiwa Spika, Taarifa za utekelezaji wa Mpango huu za Robo Mwaka ya Kwanza (Julai – Septemba 2012) zimeanza kupokelewa kutoka katika Sekta za Utekelezaji. Tumeweza kuandaa Mkakati wa Mawasiliano kuhusu utekelezaji wa Mpango wa OGP Tanzania (OGP Communication Strategy) kwa ajili ya kutangaza zaidi kwa Wananchi Mpango huu. Pia Kamati inashirikiana kwa karibu na Wakala wa Serikali Mtandao (e-Government Agency) kuhakikisha Tovuti ya Wananchi (Citizen portal) inaanza kazi mapema iwezekanavyo ili itoe huduma na maelekezo kwa Wananchi.
71. Mheshimiwa Spika, toka tujiunge na tulipoanza utekelezaji wa Mpango Kazi wetu tumepata changamoto mbalimbali. Bado Wananchi wana uelewa mdogo kuhusu Mpango wa OGP. Hivyo kuna haja ya kuutangaza zaidi Mpango huu. Aidha, taarifa kuhusu Mpango wa OGP ilichelewa kufika katika Sekta zinazotekeleza Mpango huu. Kutokana na hali hiyo, Wizara hazikuweza kujiandaa vya kutosha na hivyo baadhi ya Wizara na Taasisi kushindwa kutenga fedha za kutosha za kutekeleza Mpango wa OGP. Kiasi kidogo cha fedha zilizotengewa kwa baadhi ya Sekta hazikidhi mahitaji.
72. Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto hizo, Serikali imejipanga kutekeleza Mpango huo kwani una manufaa kwa Nchi yetu. Tunapenda kutoa shukrani zetu kwa Wadau wote na Wananchi kwa ujumla kwa kutoa maoni yao wakati wa kuandaa Mpango Kazi wetu. Tutaendelea kushirikiana na Wadau wote katika kuhakikisha utekelezaji wa Mpango Kazi huu. Aidha, tunatoa wito kwa Taasisi zote za Kiserikali, Wizara na Asasi Zisizo za Kiserikali ambazo zinatekeleza Mpango Kazi huu kuutekeleza kikamilifu ili kuleta faida ambazo zinaletwa na utekelezaji wa vipaumbele tulivyojiwekea.
VIII UTEKELEZAJI WA MPANGO WA LISHE
73. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa tarehe 12 Juni, 2011 nilikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na Naibu Waziri Mkuu wa Ireland ambapo niliahidi kwamba Serikali itatekeleza Azma yake katika kupambana na tatizo la Lishe Nchini. Aidha, Mwezi Septemba 2011 Mkakati wa Taifa wa Lishe Ulizinduliwa rasmi.
74. Katika kutekeleza ahadi hiyo, Mpango wa Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Lishe wa mwaka 2011/2012- 2015/2016, umeandaliwa na sasa uko kwenye hatua ya mwisho ya kukamilishwa. Mpango huo umeainisha kwa kina kazi zitakazofanyika katika Miaka Mitano ijayo ikiwa ni pamoja na kuandaliwa Bajeti ya utekelezaji.
75. Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Bajeti wa mwaka 2012/13 umetoa maelekezo maalum ya msisitizo kwa Sekta husika na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa kipaumbele katika suala la Lishe. Aidha, Wizara ya Fedha imeanzisha Kasma maalum ya Lishe ili Wizara zinazohusika na masuala ya Lishe zianze kukasimia Fedha kwa ajili ya shughuli za Lishe.
76. Hata hivyo, imebainika kwamba katika mwaka huu wa fedha (2012/2013), Wizara na Halmashauri nyingi hazikutenga fedha za Lishe kwa kutumia Kasma zilizoanzishwa. Napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba katika Bajeti ya 2013/2014, tutaendelea kufuatilia ili fedha zaidi za Mpango huu zitengwe kwa kutumia Kasma zilizoanzishwa.
77. Mheshimiwa Spika, vilevile, ili kuhakikisha kwamba utekelezaji wa Mkakati huu unakwenda vizuri kama ilivyopangwa, Halmashauri zote zimeanzisha Madawati ya Lishe na Maafisa husika walipewa Semina Elekezi ya jinsi ya kupanga na kubajeti masuala ya Lishe. Katika mchakato huo, Halmashauri zote za Mikoa 19 kati ya Mikoa 25 zimeanzisha Kamati za Kuratibu Lishe. Aidha, Wizara zinazohusika na utekelezaji wa masuala ya Lishe moja kwa moja zimeteua Wataalam watakaoratibu masuala hayo kwenye Wizara zao. Wizara zinazohusika ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Maji, Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto na Tume ya Mipango.
78. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Halmashauri 106 kati ya 168 na Mikoa 14 kati ya 25 tayari zimeajiri Maafisa Lishe ambao watakuwa kiungo muhimu katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa Lishe Nchini. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia Kanuni za kuweka Virutubisho kwenye Chakula “Food Fortification” zilizotangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali mwezi Julai 2011, na kuanza kutekelezwa na Wafanyabiashara na katika Halmashauri za Mikoa iliyokabiliwa na Utapiamlo mkali kwa lengo la kuboresha Lishe Nchini. Tutaendelea kusimamia utekelezaji wa Azma ya Serikali ya kupambana na tatizo la Lishe Nchini kama ambavyo tumedhamiria. Nitoe Wito kwa Halmashauri zote Nchini kuhakikisha kuwa Azma ya Serikali kuhusu kupambana na tatizo la Lishe inatekelezwa kama ilivyopangwa.
IX HALI YA AMANI NCHINI
79. Mheshimiwa Spika, katika miezi ya Septemba na Oktoba 2012, Nchi yetu ilikumbwa na machafuko yaliyosababishwa na baadhi ya Wananchi kufanya Maandamano na Vurugu kwa visingizio vya Imani za Dini na masuala ya Siasa. Maandamano ambayo kimsingi hayakuwa na vibali vya Mamlaka husika. Kama tunavyoelewa, kabla ya kufanya Maandamano yoyote na Mikutano ya hadhara, ni lazima wahusika watoe taarifa Polisi ambao ndiyo Mamlaka iliyopewa jukumu la kuruhusu au kuzuia kufanyika kwa Maandamano na Mikutano hiyo. Lengo likiwa kuratibu masuala yote ya usalama wa Wananchi na mali zao katika mikusanyiko ya aina hiyo.
80. Mheshimiwa Spika, kufanyika kwa vurugu hizo kwa kiasi kikubwa kulisababishwa na Wahusika kutokutii Mamlaka halali ambayo ni Jeshi la Polisi. Kwa mfano, kwa matukio yaliyotokea katika Mikoa ya Morogoro pamoja na Iringa, ni baada ya Polisi kukataza Maandamano na Mikutano ya hadhara kutofanyika kutokana na kuwepo kwa zoezi la Sensa lililokuwa likiendelea kwa wakati huo. Aidha, matukio mbalimbali huko Zanzibar na katika Jiji la Dar es Salaam kwa nyakati tofauti pamoja na mambo mengine yalishinikizwa na hisia za Imani za Kidini miongoni mwa Waandamanaji. Nitumie nafasi hii kuwaomba Wananchi wote waelewe kuwa, Nchi yetu inaendeshwa na Utawala wa Sheria. Hivyo, ni vyema tukazingatia na kutii Mamlaka zilizopo na amri zake. Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa, Wananchi wanapata madhara ikiwemo majeraha, upotevu wa mali na wengine kuwekwa ndani (Mahabusu) kwa kitendo tu cha kushindwa kutii Mamlaka za Nchi, likiwemo Jeshi la Polisi.
81. Mheshimiwa Spika, kwa vile hali hii ambayo imejitokeza inaonekana kushika kasi, ninawahimiza Viongozi wenzangu wa Siasa, Viongozi wa Dini na Taasisi mbalimbali tushirikiane kuwaongoza Wananchi kwa kuwaelimisha umuhimu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu ili kudumisha Amani na Utulivu katika Nchini yetu. Tukiwaelimisha tutasaidia kuwaepusha na madhara yanayoweza kutokea baada ya Mamlaka husika kuchukua hatua.
82. Mheshimiwa Spika, kimsingi, mwenendo huu wa kutotii Mamlaka unachangiwa pia kwa kiasi kikubwa na mmomonyoko wa maadili hasa kwa Vijana wetu ambao bado tuna wajibu wa kuwaelimisha masuala mbalimbali, yakiwemo utii wa Sheria na Mamlaka za Nchi. Kwa kuwa zoezi la kutoa Elimu kwa Umma kuhusu utii wa Sheria ni shirikishi, napenda kutoa wito kwa Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini, Wanahabari na Taasisi zisizokuwa za Serikali zishiriki kikamilifu katika uenezi wa Elimu ya Utii wa Sheria na Elimu ya Uraia kwa ujumla Nchini. Aidha, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haina budi sasa kuweka Programu mahususi ya Elimu ya Uraia Nchini katika Mitaala yake ili kujenga uzalendo na kukuza maadili kwa Vijana wetu wa ngazi zote tukianza na Shule za Msingi, Sekondari hadi Vyuo Vikuu.
83. Mheshimiwa Spika, kila Mtu ana uhuru wa Kuabudu kama Katiba yetu inavyoelekeza, wakati huo huo kila Mtu ana wajibu wa kuheshimu Dini na Imani za Watu wengine. Kufanya mihadhara ya kukashifu Dini nyingine ni makosa kwa mujibu wa Sheria zetu. Napenda kusisitiza tena kwamba, Serikali haitawavumilia watu ambao wanajaribu kuvuruga Amani na Usalama Nchini. Aidha, itahakikisha wale wote wanaoleta uchochezi wa kujaribu kuvuruga Amani na Utulivu Nchini, wanachukuliwa hatua stahiki. Kwa vile, Jeshi la Polisi Nchini ni Chombo muhimu katika Ulinzi na Usalama wa Raia na mali zao, nawahimiza Wananchi wote wakiwemo Vyama vyote vya Siasa Nchini na Taasisi za Dini kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu haya kwa faida yetu wote.
84. Mheshimiwa Spika, natoa tena wito kwa Wananchi wote kuithamini Amani tuliyonayo ambayo ni Tunu tuliyoachiwa na Waasisi wa Taifa hili. Ninawasihi Wananchi, Viongozi wa Kisiasa pamoja na Viongozi wa Dini kuilinda Amani tuliyonayo kwa ustawi wa Taifa letu. Taifa hili halina nafasi ya Udini, Ukabila wala ubaguzi wa aina yoyote ile. Napenda kusisitiza umuhimu wa Wananchi kutii Sheria na kutimiza wajibu wao wa kutii Mamlaka za Nchi, kwani hakuna Haki isiyo na Wajibu.
X MATATIZO YA MALIPO KUPITIA MTANDAO WA EPICOR-9
85. Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu niruhusu niongelee jambo moja ambalo limejitokeza katika utaratibu wa Mfumo wa Malipo ya Fedha za Serikali kupitia Mtandao wa Malipo wa EPICOR-9. Hivi karibuni kumekuwa na taarifa za ucheleweshaji wa Malipo mbalimbali kwa Watumishi wa Serikali na wale wa Taasisi na Sekta Binafsi wanaofanya kazi zinazolipiwa kupitia HAZINA. Sababu za ucheleweshaji huo zilitokana na kuzorota kwa Mfumo wa Malipo kulikosababisha kasi ndogo ya malipo mbalimbali ikiwemo Mishahara hasa mwishoni mwa mwezi. Kwa sasa Mfumo huo umefanyiwa maboresho na kurudi katika hali ya kawaida. Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo, bado kuna changamoto kidogo ambazo zimejitokeza kama ifuatavyo:
i) Katika kipindi cha siku mbili mfululizo, EPICOR System iligoma kupeleka malipo ya Wizara ya Katiba na Sheria (JUDICIARY) kwa sababu mbili: Kwanza, ni kutokana na kutokuwepo taarifa ya kutosha kutoka watayarishaji na Pili, kukosea katika uingizaji tarakimu kwa Kanuni ya Kiuhasibu yaani “inakotoka” na “inakokwenda” (Debit and Credit Principle). Tatizo hilo linarekebishwa na Wizara yenyewe kwa kushirikiana na HAZINA.
ii) Lakini pia kumekuwa na tatizo la tofauti ya kumbukumbu (records) za Mishahara, hususan ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambazo ziko Utumishi na zile za Computer Centre. Tofauti hizo zimesababisha ucheleweshaji wa malipo ya Watumishi wa Wizara hiyo, zikiwemo Posho za Askari wetu. Tatizo hili limeshughulikiwa kwa haraka na hakuna Mtumishi wa Wizara hiyo ambaye atakosa malipo yake.
86. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, na Wananchi wote kwa ujumla kwamba Mfumo huu umekwisha kuwa tulivu (Stabilized) baada ya kufanyiwa marekebisho. Aidha, wasidanganyike na taarifa za kupotosha kwamba Mishahara yao imechukuliwa kwa ajili ya kulipia kazi nyingine za Chama na Serikali. Napenda kuwathibitishia kwamba, taarifa hizo hazina ukweli wowote. Kwa sasa nawaomba wawe Watulivu kwa vile tatizo la Mtandao lililojitokeza limepatiwa ufumbuzi wa kudumu.
XI HITIMISHO
87. Mheshimiwa Spika, mwisho na kama ilivyo ada, napenda niwashukuru wote waliofanikisha Mkutano huu wa Tisa wa Bunge. Nikushukuru kwa namna ya pekee wewe Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza vizuri hadi tunapohitimisha siku ya leo. Nimshukuru vilevile, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri waliyoifanya. Niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. Nimshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake kwa huduma nzuri walizozitoa wakati wote tukiwa hapa. Niwashukuru Watumishi wa Serikali na Taasisi mbalimbali kwa michango yao. Niwashukuru Waandishi wa Vyombo vya Habari kwa kuwahabarisha Wananchi yote yaliyotokea katika Mkutano huu na kwa wakati. Wote kwa ujumla nasema, Asanteni Sana!!
88. Mheshimiwa Spika, tunakamilisha Mkutano wa Tisa wa Bunge lako Tukufu ambao ni wa mwisho kufanyika kwa mwaka 2012. Mkutano wa Kumi utafanyika wakati ambapo tutakuwa tumeanza mwaka 2013. Nitumie fursa hii kumuomba Mwenyezi Mungu atupatie afya njema na kutufikisha salama mwisho wa mwaka tuweze kusherehekea Sikukuu Njema ya Kristmas na Mwaka Mpya kwa Amani na Furaha!
89. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nawatakia Safari Njema na kuomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi Siku ya Jumanne tarehe 29 Januari, 2013 Saa 3:00 Asubuhi katika Ukumbi huu hapa Dodoma.
90. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment