Sheikh Mkuu, Mufti Issa Bin Shaaban Simba, akiwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salim
TAMKO LA BAKWATA JUU YA
HABARI ZINAZOTOLEWA NA VYOMBO VYA HABARI KWA TASWIRA YA “MGOGORO BAINA YA
WAISLAMU NA BAKWATA”
Hivi karibuni nilitoa indhari juu ya njama na hila za kutaka kuvamia
ofisi za Bakwata Makao Makuu kwa madai ya kutaka kuung’oa uongozi, zinazoasisiwa
na kuratibiwa na kikundi kinachojiita JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU
kinachoongozwa na Bw. Ponda Issa Ponda.
Hii si mara ya kwanza kwa kikundi hiki kutishia kuvamia Makao makuu ya
BAKWATA kwa nia ya kuundoa madarakani kwa nguvu uongozi halali uliopo. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1992
wakati wa uongozi wa aliekuwa Mufti wa Tanzania marehemu Sheikh Hemed bin Jumaa
bin Hemed kwa madai kama haya haya kwamba uongozi umeshindwa kuwaongoza
Waislamu na kuwaletea maendeleo.
Ni kwa kufuatia ghasia hizo
ndipo Serikali ilipoamua kuingilia kati na kuidhinisha kuandikishwa hilo
linaloitwa BARAZA KUU LA JUMUIA NA TAASISI ZA KIISLAMU ili liweze kufanya
maendeleo makubwa zaidi inayodai kuwa BAKWATA imeshindwa kuwaletea Waislamu. Ni jambo la kustaajabisha hadi sasa ni
miaka 20 tangu Baraza hilo lilipoandikishwa na hakuna jambo lolote la
kuwaendeleza Waislamu walilolifanya, wameshindwa hata kujenga ofisi ambayo
Baraza hilo litaendeshea shughuli zake.
Hatujawahi kushuhudia toka kwa Baraza Kuu la Jumuia na Taasisi na Tawi
lake linalojiita Jumuiya na Taasisi jambo lolote la maendeleo ya Kiislamu zaidi
ya ghasia za maandamano, kupora Misikiti na kudandia matukio na kuwachangisha
Waislamu fedha mwishoni mwa maandamano kwa kuwatapeli Waislamu fedha zao ambazo
huishia mifukoni mwa Ponda na wenzake.
Habari mbalimbali zinazoendelea kuripotiwa katika kadhia hii zinajaribu
kujenga taswira inayoonyesha kwamba mgogoro uliopo ni baina ya “WAISLAMU NA
BAKWATA”. Taswira hii si sahihi ni
potofu.
Napenda kuchukua fursa hii kuufahamisha umma wa kiislamu ukweli na hali
halisi ya kadhia hii kama ifuatavyo:
1.
Kikundi hiki kinachojitambulisha kwa jina la JUMUIYA NA TAASISI ZA
KIISLAMU si kikundi kinachowakilisha Waislamu wote wa nchi hii bali ni KIGENGE
CHA WATU WACHACHE wenye kufuata madhehebu ya MAWAHABI ambao kwa mujibu wa
ITIKADI yao wanaamini kwamba Muislamu yeyote asiefuata ITIKADI yao basi huyo
sio MUISLAMU na hafai kuwa kiongozi kwa ngazi yoyote ile.
2.
Kikundi hiki ambacho kimejivika vazi la kuendesha wanachokiita Harakati
za Kiislamu ni kikundi cha watu wachache ambao hawataki kufuata UTARATIBU uwe
wa kidini wala kutii mamlaka ya dola na wanataka matakwa yao yawe ndio
utaratibu na wanalazimisha watu wote wayafuate.
3.
Vurugu, chokochoko na ghasia za uvamizi hazikuanzia BAKWATA, wamekuwa
wakifanya hivyo sehemu mbalimbali Mikoani
kwa kuvamia na kuteka Miskiti na kuwaondoa viongozi waliochaguliwa
kihalali kwa nguvu na udhalilishaji mkubwa sana na hatimae kupora na kuhodhi
rasilimali za Misikiti hiyo.
4.
Wamekuwa wakiendesha mafunzo ya KARATE kwenye Misikiti hiyo waliyoiteka
na kuikalia kimabavu kwa vijana wao ili waweze kuendeleza dhulma yao ya uporaji
wa Misikiti na vituo vingine vya Kiislamu.
5.
Nikiwa kiongozi Mkuu wa Waislamu katika nchi hii nawataka Waislamu wa
Tanzania kutambua ya kwamba vitendo vya vurugu na ghasia na vya uvunjaji wa
sheria vinavyofanywa na Ponda na kikundi chake kamwe havina uhusiano wowote na
dini ya Kiislamu. Ni vitendo
vinavyokiuka maadili ya Uislamu na kuupa sura mbaya Uislamu miongoni mwa jamii
na mataifa. Kwa sababu hiyo
nawaonya na kuwatahadharisha Waislamu wa madhehebu zote kujitenga mbali na
matendo ya uvunjaji sheria wa kikundi hiki cha watu wachache.
6.
Kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu kila kundi la kidini lina haki ya
kuendesha kwa Uhuru shughuli zake za kidini. Na tunashuhudia katika nchi yetu madhehebu yote ya kidini
yakiendesha shughuli zao bila kuingilia madhehebu nyingine mfano Shia
Ithaashiria, Bohora, Ibadh, Hannafii na mengineyo. Madhehebu yote hayo yamekuwa yakiendesha shughuli zao bila
kuingiliana na wenzao isipokuwa kikundi hiki cha watu wachache ambao madhehebu
yao ni WAHABI na wakati mwingine wanajiita ANSAR SUNNA.
7.
Nawatahadharisha Waislamu wote nchini kwamba Ponda Issa Ponda si
mwanachuoni, si Sheikh, hakusoma elimu ya msingi ya kidunia wala ya kidini,
hata Qur’an hajui kusoma.
Anajaribu kuwatumia Waislamu kwa manufaa yake binafsi.
8.
Mwisho tunavipongeza vyombo vya dola na Serikali kwa ujumla kwa namna
walivyoshughulikia ghasia za kikundi hiki kwa busara, hekima, na subira kubwa
waliyotumia pale Wizara ya Mambo ya ndani. Nakitahadharisha kikundi hiki kinachojishughulisha na
harakati za vurugu na ghasia wasiutumie vibaya uvumilivu wa hali ya juu
ulioonyeshwa na vyombo vya dola wakati wa maandamano ya kuvamia Wizara ya Mambo
ya Ndani tarehe 07/09/2012.
Kitendo kile kilikuwa ni kuvunja sheria za nchi na UISLAMU unatutaka
Waislamu kuheshimu mamlaka iliyoko madarakani.
9.
Natoa wito kwa vyombo vya dola kwamba viangalie utaratibu wa
kuwashughulikia watu wanaoleta vurugu kwa kujifanya viongozi wa taasisi hewa na
kutumia taasisi hizo hewa kutoa matamko ya kutishia kuwaondoa viongozi halali
wa taasisi zinazosajiliwa na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria za
nchi.
10.
Naviomba vyombo vya dola vielewe kwamba si kila linalofanywa kwa
kisingizio cha dini kwamba jambo hilo ni la dini. Kwa msini huo tunaomba vyombo vya dola visisite kuchukua
hatua dhidi ya mtu, kikundi kinachojaribu kutumia anuani ya Uislamu katika
kutenda matendo ya uvunjaji wa sheria na hivyo kuhatarisha hali ya amani na
utulivu iliyopo hapa nchini.
Uislamu ni AMANI. Hata jina
lenyewe linatafsirika kuwa ni amani.
11.
Nazikumbusha taasisi zote za Kiislamu nchini kila moja kuheshimu na
kutekeleza madhumuni ya kuanzishwa kwa taasisi husika kwa mujibu wa malengo
yaliyoainishwa katika Katiba zao.
Hakuna taasisi yoyote iliyosajiliwa nchini iliyo na haki ya kuondoa,
kuweka au kubadilisha uongozi wa Taasisi nyingine.
12.
Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania halitosimama kutetea kundi lolote
litakalojinasibisha na Uilsmau katika vitendo vyovyote vile vinavyokiuka
misingi ya dini, sheria za nchi, kusababisha vurugu na kuvunja amani katika
nchi.
Wabillah
Tawfiq,
Sheikh Issa bin Shaaban
Simba, MUFTI NA SHEIKH MKUU
WA TANZANIA
No comments:
Post a Comment