Baadhi ya akina mama wa Mkoa wa Kusini Pemba, wakiwa katika chakula cha Futari iliyoandaliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu ya Chakechake Pemba jana.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa, akitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein kwa niaba ya wananchi wa mkoa wake baada ya chakula cha Futari alicho waandalia katika viwanja vya Ikulu ya Chakechake Pemba jana.
Rais Shein Awaandalia, ajumuika katika Futari na wananchi wa Kusini Pemba
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Agost 1, 2012
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana aliungana na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika futari maalum aliyowatayarishia wananchi hao.
Hafla hiyo ilifanyika huko katika viwanja vya Ikulu ndogo ya Chake na kuhudhuriwa na wananchi mbali mbali wa Mkoa huo pamoja na viongozi wa dini, Serikali na vyama vya siasa.
Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Juma Kasim Tindwa, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Mwinyihaji Makame, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih na viongozi wengine.
Akitoa neno la shukurani kwa wananchi waliohudhuria futari hiyo kwa niaba ya Rais Dk. Shein, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Juma Kasim Tindwa alieleza kuwa Dk. Shein amefarajika kwa ushiriki wa wananchi hao katika futari hiyo maalum aliyowaandalia na anawatakia kila la kheri wananchi hao.
Mhe. Tindwa aliwaeleza wananchi hao kuwa Dk. Shein hana cha kuwalipa kwa mahudhurio yao hayo ila MwenyeziMungu ndio atakaowalipa na kusisitiza kuwa upendo katika nchi ndio uliochangia kuwepo mkusanyiko huo sanjari na amani na utulivu iliyopo.
Naye Sheikh Mohammed Suleiman, akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba walieleza shukurani zao kwa Rais na kusisitiza kuwa hatua yake hiyo inaonesha upendo mkubwa kwa wananchi wake.
Alisema kuwa Dk. Shein ana kila sababu ya kusifiwa na kupongezwa katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar pamoja na kuimarisha amani, utulivu na upendo miongoni mwa wananchi.
Katika maelezo yake Sheikh Mohammed Suleiman aliitaka jamii ya Kizanzibari kutokuja mlaumu Rais Dk. Shein kuwa hajawaletea maendeleo kama watakataa oezi la kuhesabiwa yaani Sensa.
Sheikh Suleiman, alisema kuwa maendeleo yoyote hayawezi kupatikana iwapo hapatakuwa na Sensa na kusisitiza kuwa mtu asije ilaumu serikali ama kiongozi wan chi kuwa hajaletewa maendeleo kama atakaa yeye mwenyewe kuhesabiwa.
Alieleza kuwa jambo hilo katika Uislamu sio geni kwani Mtume Mohammad (S.A.W) alikwisha waeleza Waislamu kuwa hataingizwa mtu peponi ama motoni bila ya kuwepo Sensa akiwa na maana ya kuhesabiwa
Pamoja na hayo, alieleza kuwa zoezi hilo la Sensa litaweza kusaidia kujua idadi ya mayatima, walemavu wa aina zote na watu wengineo ambao pia nao ni muhimu katika jamii na wamekuwa wakihitajia mahitaji muhimu lakini baadhi yao wamekuwa hawayapati kutokana na kutojulikana idadi yao.
Wananachi hao walimuombea dua kwa MwenyeziMungu na kumuombea aendelee kongoza nchi kwa salama, amani, utulivu na uvumilivu mkubwa pamoja na kupata maendeleo endelevu huku wakimtaka kuwa na subira katika mitihani iliyotokea nchini.
Katika futari hiyo, Mama Mwanamwema Shein nae alishiriki akiungana na akina mama wenzake kutoka sehemu mbali mbali katika Mkoa huo pamoja na viongozi wa dini, serikali na vyama vya siasa na wananci kwa ujumla.
Leo Alhaj Dk. Shein anatarajiwa kufutari pamoja na wananchi wa Mkanyageni Chokocho huko Chokocho.
Wakati huo huo salamu za rambirambi kufuati kuzama kwa meli ya MV Skagit hivi karibuni zinaendelea kutolewa kwa Rais wa Zanzibar pamoja na wananchi wa Zanzibar ambapo Jumuiya ya African Public Administration anda Management (AAPAM) imetoa mkono wa pole kutokana na ajali hiyo.
Nayo Jumuiya ya Wawekezaji katika sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) imetoa mkono wa pole kwa Rais, familia na wananchi wote wa Zanzibar kufuatia ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment