TANGAZO


Friday, August 3, 2012

Ofisi ya Taifa ya Takwimu yatoa taarifa ya hali ya uchumi nchini

Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Morrice Oyuke akiongea na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam kuelezea hali ya ukuaji wa Pato la Taifa kwa 7.1% katika kipindi cha robo mwaka 2012. (Picha na Aron Msigwa - MAELEZO)


*Pato la Taifa lakua 

Na Aron Msigwa – MAELEZO.
3/8/2012. Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imetoa taarifa ya hali ya uchumi nchini na kufafanua kuwa  pato la taifa  la Tanzania limekua kwa  asilimia 7.1 katika kipindi cha robo ya mwaka 2012  ikilinganishwa  na asilimia 6.1  za mwaka jana.
Ukuaji huo wa asilimia 7.1 unatokana na ongezeko la uzalishaji katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo za kilimo, Uvuvi, Viwanda, Ujenzi na zile za utoaji wa huduma mbalimbali za jamii.
Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa lengo la  utoaji wa taarifa hizo kwa vipindi vifupi vya vya  robo mwaka unalenga kuwapatia wadau wa Takwimu za Pato la Taifa uwezo wa kutathmini mabadiliko ya ukuaji wa uchumi nchini.  
Amesema kuwa jumla ya thamani ya pato la Taifa katika kipindi cha robo ya mwaka 2012 ni shilingi 4,220,535 milioni ikilinganishwa na kiasi cha shilingi milioni 3,940,261 za mwaka 2011.
Amefafanua kuwa ukuaji wa shughuli uzalishaji katika shughuli za kilimo nchini ulifikia asilimia 1.4 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2012 zikilinganishwa na asilimia 1.2 katika kipindi hicho kwa mwaka 2011 kutokana na upatikanaji wa mvua za kutosha nchini katika mikoa inayozalisha mazao kwa wingi.
 Amesema ukuaji katika shughuli za uvuvi ulikua  asilimia 2.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2012 huku shughuli za uchumi katika sekta ya viwanda na Ujenzi ambayo inahusisha uchimbaji wa madini na kokoto ikikua kwa asilimia 14.3 ikilinganishwa na 0.8% za mwaka 2011.
Bw. Oyuke ameongeza kuwa ongezeko hilo  la uzalishaji wa madini ya dhahabu linatokana na uzalishaji wa wa madini ya dhahabu kutoka kilo 8,140 kwa mwaka 2011 hadi kufikia kilo 16,736 kwa mwaka 2012.
Pia amebainisha kuwa  shughuli za utoaji wa huduma za biashara za jumla na rejareja, ukarabati wa magari na pikipiki na vifaa vingine vya majumbani katika kipindi hicho zilifikia asilimia 9.0 huku shughuli za upangishaji nyumba na biashara zikiwa 8.2 %, uchukuzi na mawasiliano 16.4%, hoteli na migahawa 3.8%, Benki asilimia 15 shughuli za uendeshaji  serikali 6.4%, Elimu 6.1% na utoaji wa huduma za Afya nchini zikikua kwa kasi ya asilimia 5.1.

No comments:

Post a Comment