TANGAZO


Thursday, August 9, 2012

 Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba akiongea na waandishi wa habari ofisi za Tume leo (Alhamisi, Agosti 9, 2012) kuhusu tathmini ya kazi ya Tume ya kukusanya maoni ya wananchi  kuhusu Katiba Mpya. Kulia ni Katibu wa Tume Bw. Assaa Rashid.


 Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, akiongea na waandishi wa habari Ofisi za Tume leo, Alhamisi, Agosti 9, 2012, jijini Dar es Salaam, kuhusu tathmini ya kazi ya Tume ya kukusanya maoni ya wananchi, kuhusu Katiba Mpya. Kulia ni Katibu wa Tume, Assaa Rashid na kushoto ni Naibu Katibu Casmir Kyuki.



Mwandishi wa habari wa Radio Deutchelle Welle, Hawra Shamte, akiuliza swali katika mkutano huo wa waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba. Mkutano huo umefanyika Ofisi za Tume jijini Dar es Salaam leo. (Picha zote na Omega Ngole, Ofisa habari wa Tume ya Katiba)



MAELEZO YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
JAJI MSTAAFU JOSEPH S. WARIOBA KATIKA MKUTANO WA WAANDISHI WA
HABARI TAREHE 09 AGOSTI, 2012 KATIKA UKUMBI WA
WA MIKUTANO WA TUME, DAR ES SALAAM
_____________________________
Ndugu Wanahabari,
Nichukue fursa hii kuwashukuru sana kwa kukubali mwaliko wetu na nawakaribisheni. Lakini pia niwashukuru sana kwa namna mnavyotoa habari za Tume zikiwemo za mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi iliyofanyika katika Mikoa minane ya awamu ya kwanza.
Ndugu Wanahabari,
Kama mnavyokumbuka tarehe 19 Juni, 2012 nilifanya mazungumzo nanyi kwenye Ukumbi wa Karimjee hapa Dar es Salaam, na siku iliyofuata yaani tarehe 20 Juni, 2012 nilifanya mazungumzo na wenzenu wa Zanzibar, kwenye Ukumbi wa Salama uliopo katika Hotel ya Bwawani. Lengo la mazungumzo yale ilikuwa ni kuzindua rasmi kazi za Tume kupitia kwenu na kuwaeleza jinsi Tume ilivyokuwa imejipanga kutekeleza majukumu yake.
Ndugu Wanahabari,
Pamoja na mikutano hii, Tume iliendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya Tume na kuwahamasisha wananchi wajitokeza kutoa maoni. Tume pia imechapisha na kusambaza machapisho yafuatayo:
1.    Vitabu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar;
2.    Kitabu cha Katiba na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa lugha nyepesi;
3.    Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83;
4.    Kijitabu kinachoelekeza wajibu na Majukumu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
5.    Kipeperushi cha maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu Tume; na
6.    Kipeperushi kinachoeleza majukumu na kazi za Tume.
Nakala zote hizo zilisambazwa kwenye Mikoa, Wilaya na Kata zote kwenye mikoa minane iliyopangwa kufikiwa kwenye awamu ya kwanza.
Ndugu Wanahabari,
Leo nimewaalika ili niwape tathmini ya kazi ya kukusanya maoni katika mikoa minane ya awamu ya kwanza ambayo ni Pwani, Dodoma, Manyara, Kagera, Shinyanga, Tanga, Kusini Unguja na Kusini Pemba. Mikutano katika mikoa hii ilifanyika kuanzia tarehe 2 Julai hadi tarehe 30 Julai 2012.
Nianze kwa kusema kuwa Tume imefika na kufanya Mikutano kwenye Wilaya zote na kwenye vituo vyote ilivyopanga. Katika mikutano hiyo, maoni ya wananchi yalipokelewa kwa njia ya kuzungumza na wengine waliwasilisha maoni yao kwa maandishi.
Idadi ya Mikutano iliyofanyika
Jumla ya Mikutano iliyofanyika kwenye Mikoa yote minane ni 386. Kati ya Mikutano hiyo, Tume ilifanya Mikutano 8 na Makundi maalum yakiwemo Taasisi za Dini na Vyombo vya Ulinzi na Usalama. 
Idadi ya Wananchi waliohudhuria Mikutano ya Tume
Wastani wa wananchi 188,679 walihudhuria mikutano ya Tume. Hii ikiwa ni wastani wa watu 489 walifika kwenye kila Mkutano. Tume inaridhika na idadi hii na inaonesha wananchi wana mwamko wa kutoa maoni yao.
Idadi ya Wananchi waliotoa maoni
Jumla ya wananchi 17,440 walitoa maoni yao kwa njia ya kuzungumza kwenye Mikutano ya Tume. Aidha, jumla ya wananchi 29,180 walitoa maoni yao kwa njia ya maandishi na kuyawasilisha kwenye Mikutano ya Tume.
Ndugu Wanahabari,
Kimsingi, Tume imeridhika na kazi ya ukusanyaji wa maoni katika awamu ya kwanza na imepata mafanikio yafuatayo:
                     i.         Mikutano yote iliyopangwa na Tume imefanyika kwa mujibu wa Ratiba;
                      ii.         Mikutano yote ilifanyika kwa amani na utulivu na wananchi walivumiliana katika kutoa maoni yao;
                       iii.         Mikoa na Wilaya wameipa Tume ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yake;
                        iv.         Baadhi ya Wananchi wametoa maoni yao bila kushawishiwa na vikundi, vyama au taasisi;
                       v.         Katika baadhi ya maeneo, Tume iliweka utaratibu na ilipokea maoni kutoka kwa makundi maalum kama walemavu na wananchi wasioweza kuzungumza kwa lugha ya Kiswahili;
Ndugu Wanahabari,
Pamoja na mafanikio niliyoyataja hapo juu, Tume imekabiliana na changamoto mbalimbali. Changamoto kubwa ambayo Tume imekutana nayo ni ya Vyama vya Siasa kuingilia uhuru wa wananchi kutoa maoni yao. Vyama vya siasa vimekuwa vikitoa kauli na maelekezo kwa wanachama wao kufuata misimamo ya vyama jambo linalowanyima wananchi uhuru wa kutoa maoni yao. Tume inapenda kuvitaka vyama vya siasa viwaache wananchi watoe maoni yao bila kuwashinikiza. Changamoto nyingine ni pomoja na:
                     i.         Wanawake bado hawajitokezi kwa wingi kutoa maoni yao mbele ya Tume ingawa wanahudhuria mikutano hiyo;
                      ii.         Baadhi ya Wananchi kutegemea njia moja tu ya kuwasilisha maoni kwa kuzungumza wakati kuna njia nyingine kama barua pepe, posta n.k
                       iii.         Shughuli za Tume kuingiliana na shughuli nyingine za Kijamii kama vile ibada, magulio n.k
                        iv.         Muda wa saa tatu kwa mkutano mmoja katika maeneo ya mjini umeonekana hautoshi kwa wananchi kuchangia maoni yao;
Ndugu Wanahabari,
Baada ya kuwaeleza mafaniko na changamoto, naomba sasa nitoe wito kwenu kutumia kalamu na kamera zenu kuwaelimisha kwa kuendelea kuwapatia wananchi taarifa sahihi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume. Jiepusheni na kuandika habari zenye lengo la kuwapotosha na kuwakatisha tamaa wananchi. Kama huna uhakika na jambo unalotaka kuandika wasiliana na Ofisi ya Tume utapata ufafanuzi.
                     i.         Taasisi na Asasi mbalimbali zitumie uwezo wao kuwaelimisha wananchi kufika kwenye Mikutano ya Tume na kutoa maoni yao au kuiandikia Tume;
                      ii.         Vyama vya Siasa, Taasisi na Asasi mbalimbali wawaache Watanzania watoe maoni yao kwa uhuru bila kulazimishwa;
                       iii.         Wananachi wanapaswa kutambua kwamba, Katiba inayoandikwa ndiyo nguzo na mwelekeo wa maisha yao ya kila siku, wasikubali kutumiwa kwa namna yoyote ile na kikundi, Taasisi, Asasi au Chama chochote katika kuwasilisha maoni yao kwa Tume;
Ndugu Wanahabari,
Naomba nimalizie kwa kuwaeleza kuwa awamu ya pili ya kazi ya ukusanyaji maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya itafanyika katika mikoa saba ambayo ni Mbeya, Morogoro, Lindi, Ruvuma, Kigoma, Katavi na Mwanza. Kazi ya kukusanya maoni kwenye Mikoa hii inatarajiwa kuaanza rasmi tarehe 27 Agosti, 2012 na kukamilika tarehe 28 Septemba, 2012. Ratiba ya mikutano hiyo itatolewa na Tume hivi karibuni.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
TOA MAONI, TUPATE KATIBA MPYA

No comments:

Post a Comment