TANGAZO


Sunday, August 19, 2012

Misamaha ya kodi iangaliwe upya - Pinda

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
 Na Mwandishi wetu, Dodoma.

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema kuna haja ya kulitazama upya suala la misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali kwa mashirika ya dini na taasisi za kijamii ili kuhakikisha kuwa misamaha hiyo haiwaongezei gharama za malipo kwa mizigo yao kukaa bandarini kwa muda mrefu.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Agosti 18, 2012), wakati akizungumza na wakazi wa Dodoma waliohudhuria Sherehe za Miaka 10 ya Kijiji cha Matumaini kilichopo Kisasa nje kidogo ya mji wa Dodoma.

“Misamaha inatolewa lakini hatuna mfuko ulioatengwa maalum kwa ajili huduma kama hizi, tunawasamehe lakini pia tunamtaka Waziri wa Fedha akusanye fedha. Iko haja ya kulitazama upya suala hilo ili kuondoa tatizo walilolieleza,” alisema.

Alikuwa akijibu risala ya kituo hicho ambayo iliiomba Serikali ifikirie kuruhusu mizigo iliyoombewa misamaha ya kodi itolewe bandarini chini ya utaratibu maalum wakati taratibu za kiofisi za kuandika hundi zikiendelea kwa vile uhakika wa Mamlaka  ya Bandari kulipwa na Serikali upo.

Katika risala yao, kituo hicho kilimweleza Waziri Mkuu adha wanazopata kwa kusubiri mizigo iliyoombewa msamaha wa kodi itoke kwa vile huchukua muda mrefu na malipo ya kutunza mizigo (storage) huongezeka kila siku.

”Wakati tunasubiri hundi ziandikwe kutoka HAZINA kwenda TRA na Bandari, malipo ya kuweka mizigo bandarini yanakuwa yanaongezeka kila siku na huu ni mzigo ambao hatuwezi kuubeba kwa sababu dawa na viinilishe tunavyotumiwa ni misaada tu kutoka kwa wafadhili walio nje ya nchi,” walisema katika risala hiyo.

Adha nyingine waliyoieleza ni ucheleweshaji wa dawa na viini lishe kwa watoto wanaouhudumiwa na kituo hicho ambao baadhi yao wanaishi na virusi vya UKIMWI.

Waliiomba pia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iangalie uwezekano wa kukipatia ruzuku kituo cha afya kilichopo  kwenye kijiji hicho kwa vile kinahudumia wakazi wa vijiji jirani na

Mapema akitoa mahubiri katika ibada maalum ya shukrani kwa kutimiza miaka 10 ya kituo hicho, Askofu Mstaafu, Mhashamu Mathias Isuja Joseph alisema jamii haina budi kuwalea watoto katika imani na maadili mema ili wajifunze kumpenda Mungu.

”Jamii imepewa jukumu la kulinda uhai wa mtoto na kisha kuwalea vema ili wawe wacha Mungu na raia wema wa baadaye,” alisisitiza.

Kijiji cha Matumaini kilianzishwa Agosti 17, 2002 kikiwa na watoto watatu tu na familia moja ambaypo ilikuwa ikiwatunza watoto hao Hassan, Amani na Neema ambao pia walikuwepo katika maadhimisho hayo.

Kituo hicho ambacho kinatumia mfumo wa malezi ya watoto yatima kifamilia, hivi sasa kina watoto 163 wanaoishi kwenye familia 13 chini ya uangalizi wa baba na mama kwa kila nyumba. Kati ya hao, 95 wako shule za msingi, 10 wako sekondari, wanane wanasoma kwenye vyuo vya ufundi na waliobakia ni wadogo zaidi na wengine wako shule za awali.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu aliendesha harambee ya papo kwa papo na kukusanya jumla ya sh. milioni 20 zikiwa ni ahadi na fedha taslimu kwa ajili ya kukisaidia kituo hicho kujiendesha. Pia waliahidiwa magunia matano ya mahindi, kilo 100 za mchele, mafuta ya alizeti lita 20, unga wa mahindi mifuko 50 na mchele mifuko 20.

No comments:

Post a Comment