TANGAZO


Sunday, July 29, 2012

Naibu Katibu Mkuu CUF Bara, Julius Mtatiro alonga

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu masuala mbalimbali yaliyojitokeza nchini na ndani ya Bunge, yakiwemo Wabunge wanaotuhumiwa kwa kula rushwa. Kulia ni Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya. (Picha na Kassim Mbarouk)



Bunge linatia kinyaa - CUF

*Chasema wabunge kuchukua rushwa ili kutetea ufisadi hatari kwa nchi
*Chataka CCM, Chadema kuwachukulia hatua wabunge wala rushwa
*Sasa champa jukumu Selasini kuwataka wabunge mafisadi hadharani
*Walia na mafao ya wafanyakazi, wataka Serikali kuifuta sheria kandamizi
Na Said Mwishehe


CHAMA cha Wananchi(CUF), kimesema kuwa Bunge limewasikitisha Watanzania huku akisisitiza kwa hatua ambayo imefikia sasa linatia kinyaa hasa baada ya kuibuka tuhuma za baadhi ya wabunge kuchukua rushwa ili kutetea ufisadi.


Pia kimevitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) na Chama Cha Mapinduzi(CCM), kuhakikisha vinawachunguza wabunge wake ili kubaini kwa majina nani ambao wamechukua rushwa ili kuwatetea mafisadi na kumkandamiza Waziri wa Nishati na Madini Profesa Muhongo na Katibu Mkuu wake.


Pamoja na mambo mengine CUF imesema kuwa kwa hali ilivyo bungeni ni wazi wananchi watakosa imani na chombo hicho ambacho kazi yake kubwa ni kuisimamia Serikali na baadhi yao kutuhumiwa kwa rushwa ni jambo linalosikitisha ndani ya jamii.


Kauli ya CUF inakuja baada ya kuibuka tuhuma mbalimbali za rushwa wakati wa mjadala wa hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini iliyosomwa bungeni wiki iliyopita ambapo yamebainika madudu ya kutisha na yanayotia aibu kwa Bunge.


Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema kuwa ni wazi Watanzania wanakosa imani na Bunge hasa kutokana na baadhi ya wabunge kutuhumiwa kwa rushwa.


Alisema kwa mazingira hayo, hakuna Mtanzania ambaye anafurahishwa na tuhuma hizo, hivyo jukumu lililopo ni kwamba wote ambao wamechukua rushwa watajwe hadharani na CUF itahakikisha inaungana na wananchi kukemea kwa nguvu zote na haitarudi nyuma katika hilo kwani halivumiliki ndani ya jamii ya Watanzania.


CUF tumesikitishwa sana na taarifa za baadhi ya wabunge kuchukua rushwa ili kutetea mafisadi. Tumekuwa tukiwaangalia bungeni wanatumia nguvu nyingi kuzungumza kumbe wamevuta mlungula ambao huwa unawawasha na kujikuta wakitoa maneno bungeni hadi jasho linawatoka.


"Tunaomba wabunge wote ambao wametajwa kuchukua rushwa watajwe ili umma ujue. Kwa bahati nzuri mbunge wa Rombo Jeseph Selasini ameweka wazi kuwa waliochukua rushwa wanafahamika . Hivyo hakuna sababu ya kutochukua hatua dhidi yao. Hatutakubali kuona wanakaa kimya wakati wabunge wanafanya kazi ya kutetea mafisadi," alisema Mtatiro.


Pia alisema Selasini amerahisisha kazi ya kutambua wabunge ambao wamechukua rushwa  kwani katika wakati anachangia bungeni alitaja baadhi ya wabunge wa CCM na Chadema kuwa ndiyo ambao wamechukua fedha hizo na hakutaja wabunge wa CUF.


Aliongeza kuwa kuna kila sababu kwa vyama ambavyo wabunge wake wanatajwa kuchukua rushwa ili kutetea ufisadi wakachukua hatua za kuwachunguza na kuwabaini ili kuchukua hatua badala ya kukaa kimya kwani haitaeleweka ndani ya jamii.


Aliongeza kuwa kwa CCM tuhuma za ufisadi zimekuwa kama kawaida yao lakini kibaya zaidi ni kuona hata wabunge wa Chadema baadhi yao wanahusishwa katika tuhuma hizo nzito na za aibu kwa Vyama vya siasa na ndio maana wanaona haja kwa Chadema kumtumia huyo huyo Selasini kuwatajia wabunge wao waliochukua rushwa, kwani anawajua kwa majina.


Pia alisema wabunge wengi, wamekuwa na miradi ama uhusiano na kampuni mbalimbali nchini na ndiyo maana wanapochangia hoja wanachangia kwa kuangalia maslahi yao na si maslahi kwa Watanzania na kilichotokea kwa waliokuwa wanataka kumkandamiza Waziri wa Nishati na Madini ni matokeo ya wabunge wanataka kutumia nafasi zao kujinufaisha wao na kuacha kundi kubwa ambalo limewatuma kuwawakilisha katika chombo hicho.


"Kwa muda mrefu, tumekuwa tukishuhudia wabunge ambao wanapiga vikumbo kwa ajili ya kusaka miradi kwasababu watakwenda kuitetea bungeni. Kwa hatua hii, hatutakuwa na uwakilishi mzuri wa wabunge kwani tafsiri yake hawapo kwa ajili ya kutetea wananchi bali wanapigania maslahi yao," alisema.


Kuhusu vitambulsho vya Taifa, Mtatiro alisema kuwa inasikitisha kuona inapitishwa sheria kandamizi ya kuwataka wafanyakazi kuchukua mafao yao uzeeni wakati wakijua fika umri wa wastani wa kuishi kwa Mtanzania ni miaka 47 na kuhoji wabunge walikuwa wapi wakati sheria hiyo inafanyiwa marekebisho.


Hata hivyo aliitaka Serikali kufuta sheria hiyo ili kuhakikisha mfanyakazi anapoacha kazi anachukua mafao yake badala ya kusubiri hadi afe maana hali ya uchumi wa wafanyakazi wa nchii ni hatari na kitendo cha kumnyima mafao ni kutaka kumuua kabla ya wakati.


Alisema kwa tafsiri nyingine Serikali inataka wafanyakazi wachukue fedha zao baada ya kuwa marehemu kwani kwa hali ilivyo hakuna Mtanzania ambaye anaweza kufika umri ambao wao wanasema eti ndiyo sheria inavyotaka.


Hata hivyo alisema kuwa kama Serikali haitakubali kufanya marekebisho ya sheria hiy basi CUF wataungana na Watanzania wote kupinga marekebisho ya sheria hiyo ambayo wameiita kandamizi na isiyojali maisha ya Watanzania.


Wakati katika suala la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa, Mtatiro alisema kuna mambo mengi yanayoendelea ikiwemo vitendo vya rushwa kwa baadhi ya maofisa waliopewa jukumu hilo, lakini pia wamesema kutumia wajumbe wa CCM kuandikisha majina nalo halifai na kutaka waondolewe.


Pamoja na mambo mengine alitumia nafasi hiyo, kufafanua zaidi kuwa, NIDA na Serikali wahakikishe wanaondoa vitendo vya rushwa na kwamba bila kufanya hivyo imani ya wananchi kwa Serikali katika mchakato huo utaharibika.


Hata hivyo alisema kuwa muda ambao umetolewa kwa jiji la Dar es Salaam hautoshi hivyo wanaomba NIDA waongeze ili kutoa nafasi kwa wakazi wengi kushiriki katika mchakato huo muhimu na wenye tija kwa Taifa.



No comments:

Post a Comment